Jamvi La Siasa

Gachagua ajikaanga kwa ulimi wake tena

Na CECIL ODONGO, MOSES NYAMORI December 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

KWA mara nyingine aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua amejipata motoni baada ya kutaka viti vyote vitatu vya kisiasa katika Kaunti ya Nairobi katika uchaguzi mkuu wa 2027 viachiwe jamii moja na chama chake cha DCP.

Mnamo Jumapili, Bw Gachagua alizua hasira na mihemko katika upinzani alipodai kuwa ameelewana na Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka kuwa DCP iachiwe ugavana, useneta na mwakilishi wa kike wa Nairobi katika uchaguzi ujao.

Alidai kuwa mpango wao huo pia utawezesha upinzani kushinda viti 16 kati ya 17 vya ubunge katika Kaunti ya Nairobi.

“Tuna makubaliano na Kiongozi wa Wiper ambaye amekuwa akisaidia ODM Nairobi. Makubaliano ni kuwa DCP itakuwa na gavana, mwakilishi wa kike na seneta.

“Pia tumekubaliana na Wiper kuwa tuwe na wabunge 16 kati ya 17 Nairobi kutoka muungano wetu,” akasema Bw Gachagua.

Aidha, Bw Gachagua alijipiga kifua kuwa jamii yake ndiyo yenye wakazi wengi Nairobi kwa hivyo itumie idadi hiyo kudhihirisha ubabe wake katika uchaguzi ujao.

“Sisi ndio wengi Nairobi na tunamiliki biashara nyingi zaidi katika jiji hili. Hakuna vile sisi kama jamii tunaweza kukosa kuwasilisha mwaniaji wa ugavana,” akaongeza Bw Gachagua.

Jana, baadhi ya viongozi wa upinzani walipinga pendekezo la Bw Gachagua huku wakiahidi kuwasilisha wawaniaji kupitia vyama vyao, wakisema hakuna makubaliano ya kuachiana viti.

Viongozi hao walitoa maoni mseto kuhusu kauli ya Bw Gachagua, baadhi wakisema ni njama ya kuwatenga katika siasa za Jiji Kuu.

Seneta wa Makueni Dan Maanzo ambaye ni mwandani wa Bw Musyoka, alisema kauli ya Bw Gachagua inaweza kuchangia upinzani kuporomoka na kusambaratika.

“Ni njama ya kuwatupa wengine nje kwa sababu umoja wa upinzani una zaidi ya vyama vitano. Kuna jamii nyingine ambazo zinaishi Nairobi na lazima tuzishirikishe,” akasema Bw Maanzo.

Katibu wa DAP-K Eseli Simiyu alisema kuwa mtazamo wa Bw Gachagua ulikuwa wa mtu binafsi huku mwenzake wa Jubilee Jeremiah Kioni akisema chama hicho kitasimamisha wagombeaji wa viti vyote Nairobi katika uchaguzi mkuu ujao.

“Huwa wanatuita wilbaro nyekundu lakini ni kupitia kwa kuungana na heshima ndipo tutafanikiwa,” akasema Bw Kioni.

Mwenyekiti wa UPA Nyambega Gisesa alimtaka Bw Gachagua ajifunze kuwavumilia wanasiasa wengine na kuheshimu maoni yao. “Kila chama kina wajibu wa kutekeleza katika muungano wa upinzani,” akasema.

Aliyekuwa Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu aliye mwanachama wa Jubilee alisema hakuna chama kimoja kinachostahili kuvifungia vyama vingine katika siasa za Nairobi.

“Hata kama ilikuwa kutenga au kuachiana viti, mazungumzo hayo hayafai kuwepo ikiwa imesalia miaka miwili kabla ya uchaguzi,” akasema Bw Wambugu.

Hata hivyo, Mbunge wa Embakasi ya Kati Benjamin Gathiru alimuunga Bw Gachagua akisema ni kupitia maelewano ndipo upinzani utashinda viti vingi Nairobi.

“Mwaniaji wa Wiper hafai kushindana na DCP kwenye wadhifa mmoja,” akasema mbunge huyo maarufu kama Mejja Donk.

Hii si mara ya kwanza kwa naibu rais huyo wa zamani kutoa kauli tatanishi inayoonekana kama baguzi.

Mnamo Februari 19, 2023, miezi michache tu baada ya Kenya Kwanza kuingia madarakani, Bw Gachagua alidai serikali ni kama kampuni yenye hisa ambapo walioipigia kura ndio wanastahili kunufaika zaidi kuliko waliochagua upinzani.

“Hii serikali ni sawa na kampuni ya hisa na kuna wale wamiliki ambao wana hisa nyingi, wengine wenye hisa chache na kuna wasiokuwa na hisa yoyote kabisa,” akasema akiwa Kaunti ya Kericho.

“Mliwekeza kwenye serikali hii na lazima mvune. Mlipanda mbegu, kupalilia, kuweka mbolea na kunyunyiza maji, sasa ni wakati wa kuvuna,” akaongeza.

Matamshi ya kikabila na kugawanya nchi ni kati ya sababu ambazo zilichangia Bw Gachagua kubanduliwa afisini mnamo Oktoba mwaka jana.

Aidha, mnamo Mei 12, 2025 aliambia aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i kuwa lazima ajiunge na chama chenye asili yake ni Gusii kisha aunganishe jamii yake kabla ya kufikiria kuwania urais.

“Matiang’i anaonekana amehitimu. Ana kila sifa ya kuwa rais. Lakini je, ana uungwaji mkono wa nyumbani? Iwapo Wakisii hawako nyuma yake, urais wake utaishia wapi?” akasema.