Gachagua akataa kuufyata mdomo
ALIYEKUWA Naibu wa Rais Rigathi Gachagua anaonekana kuendeleza juhudi zake za kuikosoa serikali ya bosi wake wa zamani, Rais William Ruto, licha ya kuonywa afyate mdomo kwa maneno na vitendo ikiwemo kuvurugwa kwa mikutano yake.
Jana Jumanne, Januari 7, 2025, Bw Gachagua na washirika wake walishikilia kuwa vitendo vya Wakenya kutekwa nyara na mauaji ya kiholela vinaendeshwa na watu wanaolindwa na serikali.
Taarifa fupi kwenye Facebook
“Hii ndiyo maana vitendo hivyo vya ukiukaji wa haki za binadamu vinapaswa kuchunguzwa katika jukwaa wazi ili ulimwengu uone jinsi utawala huu ulivyojitolea kunyamazisha wakosoaji wake. Unafanya hivyo bila kuzingatia kuwa demokrasia hunawiri katika mazingira kama haya ya ukosoaji. Kenya ni taifa linaloongozwa na utawala wa sheria,” akasema kwenye taarifa fupi kupitia ukurasa wake wa Facebook.
Bw Gachagua alisema hayo dakika chache baada ya wabunge na maseneta washirika wake kupendekeza kuwa tume huru ibuniwe kuchunguza utekaji nyara na maovu mengine waliyodai yanatekelezwa na utawala wa Rais Ruto.
Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi jana, wanasiasa hao pia walipendekeza kuwa tume kama hiyo ichunguze mienendo ya polisi kutumika kuendesha vita vya kisiasa, unyakuzi wa ardhi na kuchipuka kwa makundi haramu kama vile Mungiki.
Viongozi hao walisema vitendo hivyo vya ukiukaji wa haki za binadamu ni tishio kwa usalama, hadhi na haki za kidemokrasia za Wakenya.
Presha kutoka nchini na ng’ambo
“Tunaamini kuwa vijana hao watano waliachiliwa huru jana (Jumatatu) sio kwa mapenzi ya waliowateka, bali ni kutokana na presha kutoka humu nchini na ng’ambo. Ndiyo maana tunataka uchunguzi wa kina na wa uwazi kuhusu vitendo hivi; uchunguzi huo unapaswa kuendeshwa na Tume Huru ya Uchunguzi,” Seneta wa Kiambu Karungo Thang’wah akasema.
“Tume hiyo pia ichunguze maovu mengine katika serikali hii kama vile polisi na asasi nyingine huru kutumiwa kuendeleza ajenda za kisiasa, visa vya unyakuzi wa ardhi na kufufuliwa kwa magenge ya uhalifu kama vile Mungiki,” akaongeza.
Vijana walioachiliwa huru Jumatatu ni pamoja na Billy Mwangi, Ronny Kiplagat, Peter Muteti Njeru, Benard Kavuli na Gideon Kibet, almaarufu Kibet Bull. Vijana hao watano waliotekwa nyara kati ya Desemba 17, na Desemba 25, 2024, waliachiliwa mwendo wa asubuhi katika sehemu mbalimbali nchini.
Hata hivyo, Steve Mbisi aliyetekwa nyara mnamo Desemba 17, katika eneo la Mlolongo, Machakos hakuwa ameachiliwa huru jana jioni. Inadaiwa kuwa vijana hao walitekwa kwa kuweka jumbe, picha na vibonzo vya kuwakosoa viongozi wakuu serikalini na baadhi ya sera za utawala wa Kenya Kwanza.
Kuishambulia serikali
Bw Gachagua na wandani wake waliendelea kuishambulia serikali siku chache tu baada ya Naibu wa Rais, Prof Kithure Kindiki kuwataka kukoma kuwachochea Wakenya dhidi ya serikali.
Akiongea alipohudhuria ibada katika Kanisa la Kamumu Full Gospel, Mbeere, Embu, Prof Kindiki alimsuta Gachagua kwa kuendelea kueneza kile alichokitaja kama uwongo kuhusu serikali na kutowaheshimu viongozi wengine.
“Serikali hii haitavumilia mtu yeyote ambaye lengo lake ni kupanda mbegu ya migawanyiko miongoni mwa Wakenya, bila kutoa suluhu kwa changamoto zinazowakumba,” akasema Naibu wa Rais.
Aidha, mnamo Ijumaa wiki jana, Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah alimshambulia vikali Bw Gachagua akidai kuwa ndiye mhusika mkuu katika visa vya utekaji nyara wa Wakenya kiholela.
Akihutubu katika hafla ya mazishi ya mamake Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, ambayo pia ilihudhuriwa na Rais Ruto, mbunge huyo wa Kikuyu alidai kuwa Bw Gachagua hushirikiana na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya kuendesha vitendo hivyo vya ukiukaji wa haki.
‘Natembeya na rafiki yako Gachagua’…
“Wewe Natembeya na rafiki yako Rigathi Gachagua ndio mnaendesha utekaji nyara wa vijana kisha mnageuka kuilaumu serikali. Tunajua kwamba ulipokuwa Mshirikishi wa Bonde la Ufa wewe ndiwe ulihusika katika visa vya utekaji nyara wa Wakenya ambao baadaye miili yao ilipatikana katika Mto Yala,” Bw Ichung’wah alimfokea Gavana Natembeya, akijibu ombi lake kwa Rais Ruto kuamuru kukomesha kwa vitendo hivyo.
Jana, Bw Thang’wah, na wenzake, walimwondolea Bw Gachagua lawama wakishikilia kuwa wahusika wakuu ni maafisa wa serikali.“Hawa vijana walitekwa kwa kuikosoa serikali na hivyo serikali ndio iliamuru wachukuliwe kwa nguvu, wazuiliwe na kudhulumiwa,” akaeleza Seneta huyo wa Kiambu.
Wandani hao wa Bw Gachagua walisisitiza kuwa kuachiliwa huru kwa vijana watano hakutoshi wakisema watu ambao waliwateka na kuwazuilia kwa zaidi ya siku 15 wanafaa kutambuliwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Hawajui waliohusika
“Inaudhi kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi na Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) wanadai kuwa hawajui waliohusika na vitendo hivi vya ukiukaji wa haki. Lakini ajabu ni kwamba siku chache baada ya Rais William Ruto kuahidi kukomesha vitendo hivyo, vijana waliachiliwa,” akasema Seneta John Methu.
Wengine walioandamana na wawili hao ni wabunge; Gachoni Wamuchomba (Githunguri), Wakili Mureu (Gatanga), Onesmus Ngongoyo (Kajiado Kaskazini), Paul Kihungi (Mathioya), Amos Mwago (Starehe) na Seneta wa Kajiado Seki Ole Kanaar.
Viongozi hao pia waliitaka tume hiyo huru itakayobuniwa ichunguze matukio mawili ambayo Bw Gachagua na wafuasi wake walivamiwa na wahuni mwaka jana katika maeneo ya Limuru, Kiambu na Shamata, kaunti ya Nyandarua.
“Tunataka visa hivi viwili vichunguzwe na tume huru kwa sababu inaonekana wazi kwamba polisi hawako tayari kuchunguza maovu kama hayo,” Bw Methu akaeleza.
Vikao maalum Bungeni
Wandani hao wa Bw Gachagua pia wanataka vikao maalum vya Bunge la Kitaifa, Seneti na Mabunge ya Kaunti viitishwe ili kujadili visa vya uketaji nyara, kufufuliwa kwa kundi la Mungiki na maovu mengine yanayoendeshwa na utawala huu.
Aidha, wameipongeza Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC) kwa kufungua mtandao wake kwa ajili ya kupokea ripoti kuhusu visa vya ukiukaji wa haki za kibinadamu nchini.