Jamvi La Siasa

Gachagua amcheka Ruto, asema Uhuru hawezi kumsaidia kupata tena Mlima

Na MWANGI MUIRURI December 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua amepuuzilia mbali juhudi za Rais William Ruto za kuridhiana na mtangulizi wake Uhuru Kenyatta, akisema hatua hiyo haitamsaidia kurejesha ushawishi wake Mlima Kenya.

Bw Gachagua anasema mkutano kati ya wawili hao, uliofanyika katika kijiji cha Ichaweri, Gatundu Kusini, Kiambu, hautaathiri kwa vyovyote mwelekeo wa kisiasa anaolenga kutoa Januari kwa wakazi wa Mlima Kenya.

Mbunge huyo wa zamani wa Mathira, ambaye aliondolewa afisini Oktoba, ameahidi wafuasi wake kuwa atatoa tangazo kuu la kisiasa mapema mwakani.

‘Hata sisi tunaongea na watu lakini ni siri’

“Hatuwezi kuwazuia watu kukutana. Hatuwezi kuamua nani anakutana na yupi nyakati hizi. Hatuna mamlaka kama hayo. Ama kwa hakika tunahimiza watu wengi waje pamoja na wazungumze kwa manufaa yao. Sisi pia tunaongezea lakini kuna masuala tunayozungumzia ambayo tumeamua yawe siri,” Bw Gachagua akasema kwenye mahojiano na Taifa Leo, Jumanne.

Akaongeza: “Subiri tangazo la Mwaka Mpya ambalo tutatoa na utagundua kuwa nasi tumekuwa tukikutana.”

Japo wakazi wa Mlima Kenya wamekuwa wakilalamikia sera mbovu za serikali, uasi kamili dhidi ya Rais Ruto ulichangiwa na ukuruba kati yake na Raila Odinga na kutimuliwa kwa Bw Gachagua.

Bw Odinga alikataliwa na wakazi wa Mlima Kenya katika uchaguzi wa 2022, licha ya kupendekezwa na kuungwa na Bw Kenyatta akiwa mamlakani.

Rais William Ruto alipomtembelea Rais mstaafu Uhuru Kenyatta nyumbani kwake Gatundu Desemba 9, 2024. Viongozi hawa walisema walizungumzia masuala ya umuhimu wa kitaifa na kikanda. Picha|PCS

Bw Odinga alipata asilimia 12 pekee za kura katika eneo hilo huku Rais Ruto akizoa asilimia 87 ya kura hizo za urais.

Hii ndio maana wakazi wa Mlima Kenya walikerwa zaidi na kuingizwa serikalini kwa Bw Odinga, kupitia uteuzi wa wandani wake watano kuwa mawaziri.

Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya maandamano ya vijana wa Gen Z waliopinga Mswada wa Fedha wa 2024 na kuishia kuvamiwa kwa majengo ya Bunge.

Hiyo ilitoa taswira kuwa mrengo wa Odinga uliletwa serikalini kuzima maasi hayo.

Nafasi kutunukiwa Kithure Kindiki

Hata hivyo, hatua ya Rais Ruto kudhamini hoja ya kumtimua Gachagua na nafasi yake kutunukiwa Kithure Kindiki ndio iliwafanya wakazi wa Mlima Kenya kumkataa kabisa.

Kutimuliwa kwa Gachagua kulikatiza kabisa uhusiano kati ya Rais Ruto na wakazi huku wandani wake kiongozi huyo wa kitaifa wakifukuzwa na kuzomewa katika mikutano ya hadhara.

Hasira zao zilichemka zaidi kufuatia kisa cha juzi ambapo Gachagua alivamiwa na wahuni eneo la Limuru, kaunti ya Kiambu.

“Rais Ruto ametuonyesha kila mara kwamba, anataka kushiriki vita vya kisiasa nasi. Anatuchukulia kama wageni serikalini na ndio maana tunapanga kulipiza kisasi dhidi yake katika uchaguzi mkuu wa 2027,” akasema Seneta wa Nyandarua John Methu.

Ni katika mazingira kama hayo ya kisiasa Mlima Kenya ambapo, ili kuokoa ndoto yake ya kuchaguliwa tena 2027, ameanza kujenga uhusiano mpya na eneo hilo lenye kura nyingi.

Hata hivyo, licha ya wadadisi wa kisiasa kusema inakuwa vigumu kwa juhudi zake kuzaa matunda, Rais Ruto anaonekana kujikakamua kujaribu bahati yake.

Uhusiano haujakuwa mzuri

Uhusiano kati ya Rais Ruto na Bw Odinga haujakuwa mzuri kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022, Kenyatta alipoamua kuunga mkono Bw Odinga katika kinyang’anyiro cha urais.

Huku mkutano wa Jumatatu kati ya Ruto na Kenyatta ukiendelea kuzua gumzo katika anga za kisiasa, mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Peter Kagwanja alisema “baada ya moshi, subiri uone moto.”

Profesa Kagwanja anaongeza kuwa “hivi karibuni utawaona wandani wa Bw Kenyatta wakitunukiwa vyeo serikalini Rais Ruto akijaribu kurejesha ushawishi wake kisiasa Mlima Kenya.”

Msomi huyo anasema Rais anajaribu kuyeyusha umaarufu mkubwa wa Gachagua katika eneo hilo.

“Rais Ruto alipozomewa mwezi jana katika kaunti ya Embu, aligundua kuwa Bw Gachagua na Bw Kenyatta walishangiliwa. Kwa sababu hawezi kupatana na Bw Gachagua sasa, rais ameona ni hatua ya busara kuzungumza na Bw Kenyatta,” Profesa Kagwanja anaeleza.