Jamvi La Siasa

Gachagua anatapatapa katika uchaguzi wa Mbeere Kaskazini au ni ujanja?

Na CECIL ODONGO September 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

BAADA ya kujiondoa kwa mwaniaji wa chama cha DCP katika uchaguzi mdogo wa Mbeere Kaskazini, aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua amejipata katika kona mbaya kudhihirisha kuwa bado yeye ni maarufu katika siasa za Mlima Kenya.

Duncan Mbui ambaye anasemekana alikuwa na umaarufu akinuia kupeperusha bendera ya DCP katika uchaguzi huo ujao, alijiondoa Jumapili.

Aliahidi kugombea kama mwaniaji huru akidai hatua yake imetokana na upinzani kuamua kuunga DP kwenye uchaguzi huo.

Mwaniaji wa DP ni Newton Karish ambaye pia ni diwani wa wadi ya Muminji.

Aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Geoffrey Ruku ambaye sasa ni waziri wa Utumishi wa Umma, alichaguliwa 2022 kupitia kwa tiketi ya DP.

Mbali na Bw Mbui na Karish, Leonard Muthende atapeperusha bendera ya chama tawala cha UDA.

Hatua ya DCP kutokuwa na mwaniaji Mbeere Kaskazini inatazamwa na wadadisi kama upanga wenye ncha mbili – inaweza kumponza Bw Gachagua au ikaondoa hatari kwa upinzani ambao huenda ungegawa kura kwa kusimamisha wawaniaji wengi.

Wachanganuzi wanasema iwapo mwaniaji wa UDA atashinda kiti hicho, basi Bw Gachagua atapoteza umaarufu ikizingatiwa hiyo itadidimiza kauli yake kuwa yeye ndiye kigogo wa siasa za Mlima Kenya.

Wanasema litakuwa pigo zaidi kwa Bw Gachagua iwapo Bw Mbui atashinda kiti hicho kama mwaniaji huru kwa sababu hatakuwa na mamlaka ya kudai ni ushindi wa DCP.

“Gachagua anajaribu kurudi nyuma ili asionekane kuwa na ubinafsi machoni pa vyama vingine. Bw Gachagua anahofia upinzani kusambaratika kwa kuwa mawimbi ya 2027 ni makubwa kuliko chaguzi ndogo,” asema mchanganuzi wa Kisiasa Javas Bigambo.

Aidha, wadadisi wanasema, iwapo Bw Muthende atanufaika kutokana na Bw Mbui kugawanya kura, na UDA ishinde, Bw Gachagua hatakuwa na lake ikizingatiwa amekuwa akisema lengo lake ni kuondoa UDA Mlima Kenya.

Kadhalika, huenda ikachukuliwa kama undumakuwili kwa DCP iwapo itakuwa na mwaniaji Malava huku ikikosa kuwa na mgombeaji Mbeere Kaskazini.

Ikichukuliwa kuwa Bw Gachagua hana umaarufu mkubwa Magharibi mwa nchi, zimekuwapo shinikizo kuwa upinzani ukiachie kiti hicho chama cha DAP-Kenya ambacho kiongozi wake Eugene Wamalwa ni mmoja wa vinara wa muungano wa upinzani.

Katika eneobunge la Malava, DCP imemtaja Wakili Edgar Busia nayo DAP-K inampigia debe Seth Panyako.

Mchanganuzi Martin Andati anasema si uoga kwa Gachagua kuchukua hatua hiyo bali ni mkakati wa kuhakikisha kiti hakiendei serikali.

“Nina hakika kuwa hata Malava, DCP itaondoa mwaniaji wake na kuachia DAP-K na ni wazi kuwa uhusiano kati ya Cleophas Malala na Rigathi si nzuri,” akasema Bw Andati.

Alipobuni DCP, Bw Gachagua alisema ndicho chama cha Mlimani na amekuwa akidai kuwa vyama vingine vidogo vinadhaminiwa na Rais William Ruto kugawanya kura za Mlima Kenya.

“Hiyo ni mbinu yake ya kugawanya kura za Mlima Kenya na sisi tumegundua ujanja wake huo wa kudhamini vyama vidogo vidogo,” akasema Bw Gachagua, Julai 18 mwaka huu.

Hasa amekuwa akionekana kulenga Jubilee na baadhi ya vyama vidogo Mlima Kenya.

DP ni chama huru na kinaongozwa na Justin Muturi kwa hivyo hata ikifanikiwa kuwahi ushindi Mbeere Kaskazini, hautakuwa mtamu kuliko ule wa DCP ambayo ingekuwa na nafasi ya kuwa na mbunge wake wa kwanza tangu kizinduliwe mnamo Mei 17 mwaka huu.