Jamvi La Siasa

Gachagua ataka Trump amlete balozi ‘asiyebembelezana’ na Ruto

Na KEVIN CHERUIYOT August 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua sasa anamtaka Rais wa Amerika Donald Trump amteue balozi ambaye hapendelei utawala wa Rais William Ruto.

Akiongea wakati wa mahojiano Jiji la Kansas, Amerika, Bw Gachagua alisema Rais Trump atasaidia kusafisha Kenya iwapo tu atamteua balozi ambaye anapigania utekelezaji wa sheria na kuheshimiwa kwa haki nchi inapoelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Kwa mujibu wa Bw Gachagua, Amerika inastahili kutuma balozi mwenye sifa kama Smith Hempstone ambaye alihudumu nchini kati ya 1989-1993.

“Tunamwomba Rais Trump kuwa anapomteua balozi mpya Kenya, amteue yule mwenye sifa kama za Hempstone ambaye alisaidia Kenya wakati utawala wa enzi hizo ulikuwa ukishiriki ukiukaji wa haki za kibinadamu na kulemaza demokrasia. Tutafurahi sana tukimpata balozi kama Hempstone,” akasema Bw Gachagua.

Marehemu Balozi Hempstone alikuwa mwiba wakati wa utawala wa Kanu na ni kati ya walioshinikiza kukumbatiwa kwa mfumo wa vyama vingi katika uchaguzi mkuu wa 1992.

Kauli ya Bw Gachagua hata hivyo ni kama upepo unaopita, ikizingatiwa kuwa uteuzi wa mabalozi wa Amerika hupitishwa kwenye mchakato wa kisheria na hushirikisha kuidhinishwa na Bunge la Seneti Amerika.

Balozi wa Amerika katika nchi yeyote huanza kazi rasmi baada ya Seneti kukamilisha mchakato wa kutathmini kufuzu au kuhitimu kwake.

Kazi ya balozi huyo ni kumwakilisha rais wa Amerika na pia kuimarisha uhusiano katika nchi anakohudumu na Amerika.

Bw Gachagua anadai kuwa serikali ya Rais Ruto imetekeleza ukiukaji mkubwa zaidi wa haki ambao unaweza kuangaziwa tu na balozi wa Amerika pamoja na mabalozi wengine.

Alidai kuwa akichaguliwa rais mnamo 2027, maafisa wa usalama ambao walihusika katika kuwaua vijana watakamatwa na kushtakiwa.

“Nitabuni jopo la uchunguzi kuhusu mauaji ya Juni 25 na mengine ambayo yametokea. Nitahakikisha wote waliohusika na utekaji nyara pia wanachukuliwa hatua kali,” akasema.

Pia aliahidi kuhakikisha kuwa familia ya vijana wote waliouawa au kujeruhiwa zinalipwa fidia.

Kwenye mikutano yake mingi Amerika, Bw Gachagua amekuwa akimwagilia maji baridi utawala wa Rais Ruto na kuusawiri kama ule ambao ni kandamizi na uliofanya maisha yawe magumu kwa Wakenya.

Hata hivyo, Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura amempuuza Bw Gachagua na kusema si mzalendo.

“Anamtaka Rais William Ruto afeli na hata ushabiki wake kwa Harambee Stars ni vuguvugu. Sisi ni nchi moja, taifa moja na watu wamoja,” akasema Bw Mwaura.