Gachagua na Kalonzo wageuka ‘wanaharamu’ wa siasa za ubabe Kenya
NDOA ya kisiasa ambayo kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na aliyekuwa naibu rais Kalonzo Musyoka wanasuka inaonekana kulengwa hata kabla ya wawili hao kuitangaza rasmi huku wakitengwa na mibabe wa siasa za kitaifa.
Wawili hao wamekuwa wakiashiria kuwa wanasuka muungano kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 kumbandua uongozini Rais William Ruto.
Gachagua amesema atatoa tangazo kuu mwaka ujao kupatia mwelekeo wa kisiasa eneo la Mlima Kenya baada ya kutimuliwa kwake ofisini na bunge kupitia hoja ambayo Bw Musyoka aliagiza wabunge wa chama chake kupinga.
Ndoa yao ya kisiasa ilionekana kupata baraka za wazee wa jamii za Mlima Kenya kupitia muungano wao wa Gema ambao walikaribisha wale wa jamii ya Akamba.
Hata hivyo, ukuruba wao unaonekana kuvurugwa kupitia njama kali za mibabe wa siasa za kitaifa na weledi wa kisiasa wa Rais William Ruto ambaye amezika tofauti zake na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta ambaye Gachagua aligeukia baada ya kutofautiana na kiongozi wa nchi
Dkt Ruto ambaye kuridhiana kwake na kiongozi wa ODM Raila Odinga kulisambaratisha muungano wa upinzani wa Azimio la Umoja One Kenya ambao Bw Musyoka na Uhuru ni vinara wenza, ameteua mawaziri na wanasiasa wenye ushawishi kutoka Mlima Kenya hatua ambayo wadadisi wa siasa wanasema inanuiwa kurejesha ushawishi wake ulioshuka baada ya kumtimua Bw Gachagua.
Katika uteuzi huo amepuuza eneo la kusini mashariki ambalo ni ngome ya Musyoka huku akilenga washirika wa Bw Kenyatta na Bw Odinga.
“ Ni wazi kuwa Bw Musyoka na Bw Gachagua wametengwa na mibabe wa kisiasa nchini. Ruto amewaendea waliokuwa mahasimu wake wakuu katika uchaguzi mkuu wa 2022 dhidi ya Raila Odinga na Uhuru Kenyatta. Anacholenga hasa ni ushawishi wao na kuhakikisha hawaungi mkono wapinzani wake wakuu hasa Gachagua na Musyoka wakiungana,” asema mchambuzi wa siasa, Dkt Isaac Gichuki.
Anasema anacholenga Rais ni “ kuharibu mipango yoyote inayoweza kumpokonya kura za Mlima Kenya na kutaka kuonyesha ana shida na wakazi wa Mlima Kenya isipokuwa Gachagua huku akipuuza ngome ya Kalonzo katika uteuzi serikalini ili wakazi wamchukie kiongozi huyo wa Wiper kwa kuwakosesha minofu kama maeneo mengine ya nchi.”
Anasema hasira za Dkt Ruto kwa Bw Musyoka ni kwa kuwa makamu rais huyo wa zamani alikataa kuunga hoja ya kutimuliwa kwa Gachagua na kwa sasa ndiye anaweza kunufaika na kura za Mlima Kenya magharibi eneo ambalo halikufurahishwa na kutimuliwa kwa mwana wao kutoka wadhifa wa naibu rais.
“Anachofanya rais ni kuandaa kikosi cha kuzima ushawishi wa Gachagua mashinani na kwa kufanya hivyo kuvuruga ukuruba wake na Bw Musyoka. Lengo hapa sio Gachagua hasa kwa kuwa ilivyo kwa sasa hawezi kugombea kiti cha urais isipokuwa aoshwe na mahakama katika kesi aliyowasilisha. Anayelenga rais ni ushawishi wa Gachagua unaoweza kumfaidi Bw Musyoka na ndio sababu amevuta wanasiasa wakuu upande wake kwa kuwapa nyadhifa serikalini,” akasema Dkt Gichuki.
Mchambuzi wa siasa Joyce Kibiru anasema kuanzia sasa kampeni inasukwa kusawiri Bw Gachagua na Bw Musyoka kama “wanaharamu wa siasa za Kenya” hasa kufuatia ukuruba wa Rais Ruto na Raila na Rais Ruto na Uhuru.
“Wanasiasa wa vyama vya upinzani walioteuliwa serikalini ndio watatumiwa kwa kampeni hii na dalili zimeonekana kutoka kwa wale wa ODM ambao kwao, serikali waliyokuwa wakikosoa imekuwa nyeupe kama pamba,” akasema.