Hawa wameiva kweli kurithi Raila?
Wanasiasa wakuu ndani na nje ya Chama cha Orange Democratic Movement (ODM), wengi wao vijana, wameanza mikakati ya siri ya kuwania urithi wa kisiasa wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.
Baadhi ya wanasiasa hawa wanawania kudhibiti chama cha ODM kama njia ya kurithi Raila huku wengine wakijitahidi kujijenga kama viongozi wakuu wa ngome za Raila wanazotoka.
Ndani ya ODM, kuna minong’ono huku baadhi ya wanachama wakijiuliza ni kwa nini sehemu ya Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC) ilimteua kwa haraka kaka wa Raila, Dkt Oburu Odinga, kuwa kiongozi wa muda.
Ni kizazi kipya cha mchanganyiko wa wanasiasa walioteuliwa, wataalamu serikalini, na viongozi wa jamii wanaopigana kurithi ushawishi wa kisiasa wa Raila.
Naibu Kiongozi wa ODM Abdulswamad Nassir amesema kifo cha Raila kimeacha pengo kubwa, si tu ndani ya ODM, ambacho sasa kinaongozwa na Dkt Oburu Odinga kama kaimu bali pia katika eneo la Nyanza.
“NEC ya ODM ilimteua Seneta wa Siaya, Oburu Odinga, kuwa kiongozi wa muda wa chama hadi kamati za juu za chama zitakapochagua kiongozi wa kudumu kujaza nafasi kubwa aliyoacha kiongozi wetu aliyeondoka,” alisema Nassir.
Huku Dkt Oburu akiongoza chama kwa muda, kuna mapambano makali ya kuona ni nani kati ya viongozi wa kizazi kipya atakayerithi Raila kisiasa kama msemaji wa jamii.
Dkt Oburu anafahamu kuhusu ushindani huu, akisema: “Watu wengine wameniuliza kwa kuwa nina zaidi ya miaka 80, nitakuwa na uwezo gani wa kuongoza chama hiki. Pia wameniuliza tutashughulikiaje urithi huu. Niliwaambia kuwa viongozi wote wa sasa wa ODM wana uwezo wa kuongoza chama. Wote wana uwezo, lakini kuna msemo unasema kuwa viongozi huibuka kama uyoga unavyokua. Unaamka asubuhi moja unagundua wako. Hata Raila Odinga, hakukuwa na mahali ambapo jamii ya Waluo ilikusanyika kuteua kiongozi wake,” alisema Ijumaa.
Majina kadhaa ya wanasiasa na wataalamu serikalini yamejitokeza kati ya wale wanaowania kutwaa uongozi wa ODM..
Majina yaliyoibuka ni pamoja na Mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, Mawaziri John Mbadi (Fedha) na Opiyo Wandayi (Kawi), pamoja na watoto wa Raila, Winnie na Raila Jr. ambaye aliteuliwa kama kiongozi wa familia.
Mapambano makubwa ya urithi wa kisiasa wa Raila katika maeneo ya Nyanza, Magharibi na Pwani yameongezeka, huku Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna, Mawaziri Ali Hassan Joho (Madini), Wycliffe Oparanya (Ushirika), na Rais William Ruto wakiwa na nia ya kuendeleza ushawishi wa Raila.
Viongozi wengine kama Simba Arati (Gavana wa Kisii) na Seneta Godfrey Osotsi wa Vihiga pia wanangojea nafasi ya kuongoza chama.
Joho, kwa upande wake, amesisitiza kuwa atamuunga Rais Ruto hadi uchaguzi ujao, ingawa Oparanya anaonekana “ kutofikia uamuzi.”
Rais Ruto alisema katika ibada ya mazishi ya Raila huko Bondo Jumapili:
“Nawahakikishia wanachama wa ODM kwamba tutawaunga mkono, kwa sababu Baba aliamini katika uwepo wa vyama vingi. Nguvu ya ODM ni muhimu kwangu kwani hivi ndivyoi tutajenga demokrasia imara.”
Rais alisisitiza kuwa ODM, “itaunda serikali ijayo au kuwa sehemu ya serikali ijayo. “Sitakubali, kwa heshima ya Odinga, watu kuchezea ODM na kuibadilisha kuwa chama cha upinzani.”
Dkt Raymond Omollo, Katibu wa Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa, ni mtaalamu serikalini ambaye kimya kimya anajipatia ushawishi kisiasa. Ingawa si kiongozi wa kisiasa, ushawishi na mtandao wake umeenea tangu alipojiunga na Serikali. Baadhi ndani ya ODM wanashuku kuwa anaweza kuwa daraja muhimu kati ya Serikali na Nyanza baada ya Raila.
Kwa urithi wa kisiasa katika Nyanza, Profesa Gitile Naituli wa Chuo Kikuu cha Multimedia anasema eneo hilo limekuwa thabiti, kinzani, na hivyo wale wanaotarajiwa kuwa viongozi wake lazima wawe tayari kudumisha moto huo.
Willis Otieno, Naibu Kiongozi wa Chama cha Safina, anasema kuwa bila ushawishi mkubwa wa Raila, ulingo wa kisiasa wa Kenya unaweza kufunguka kwa viongozi vijana.
“Kuna viongozi wengi wanafunzi wa Raila ambao wanaweza kuchukua uongozi, lakini kujaza nafasi yake si rahisi. Bila sauti hiyo, kutakuwa na pengo ambalo hakuna mtu Kenya anayeweza kujaza,” alisema Otieno.
Gladys Wanga, Gavana wa Homa Bay, amepanda cheo ndani ya chama hadi ngazi ya kitaifa. Mnamo 2022, aliweka historia kuwa gavana wa kwanza mwanamke kutoka Nyanza.
Babu Owino, Mbunge wa Embakasi Mashariki, anawakilisha sauti ya kizazi kipya.
Winnie Odinga, kitinda mimba wa Raila na anayejulikana zaidi katika familia kwa kuhusika na siasa, pia amejitokeza. Akiwa mwanachama wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Winnie amekuwa akishughulikia mawasiliano, usafiri na shughuli za kampeni za baba yake kwa miaka mingi. Uaminifu wake na ufahamu wake kisiasa unampa nguvu za kurithi wa Raila.
Akiwahutubu kwenye ibada ya wafu ya Raila Jumapili iliyopita, Winnie alionyesha dalili za kuanza siasa za humu nchini, akiashiria yuko tayari kuchukua kuendeleza mapambano ya babake.“Mheshimiwa Rais, watu wetu wanakushukuru kwa kuheshimu baba yetu. Asante kwa kusimama pamoja nasi. Pia unapaswa kujua, ikiwa unajiuliza, niko tayari kurudi nyumbani,” alisema.
.