Hii Wiper itampa Babu Owino ugavana wa Nairobi?
KWA mara nyingine mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino ameonyesha dalili kwamba atagura ODM kuelekea uchaguzi mkuu ujao hatua ambayo itaathiri pakubwa ushawishi wa chama hicho katika kaunti ya Nairobi.
Wiki hii mbunge huyo, anayepinga Serikali Jumuishi inayoshirikisha chama chake, alionyesha dalili kwamba atawania ugavana wa Nairobi kwa tiketi ya chama cha Wiper Patriotic Front (WPF), japo wadadisi wanasema haitakuwa rahisi kwake kufaulu.
Alihudhuria mkutano wa wanafunzi wa vyuo vikuu na vya kiufundi ulioongozwa na kiongozi wa chama hicho Kalonzo Musyoka jijini Nairobi na kuunga mkono azma yake ya urais akimtaja kama kiongozi wa kipekee anayeweza kuleta uongozi bora nchini.
“Kalonzo alipokuwa katika Azimio alikuwa mtu mzuri. Sasa ambapo anapinga Serikali Jumuishi na kuendesha kampeni ya kumwondoa afisini Rais William Ruto anadaiwa kuwa mbaya. Mimi naona anatosha kuwa rais na sijali nikishutumiwa,” akaeleza alipowahutubia zaidi ya wanafunzi 700 kutoka vyuo hivyo vya elimu ya juu.
Bw Owino aliwataka vijana kuelekeza mkondo wa mustakabali wa taifa hili kwa kujiandikisha kwa wingi kuwa wapigakura ili kuondoa mamlakani utawala wa sasa na kuweka utawala utakaotekeleza sera za kuboresha maisha yao.
Kwa upande wake, Kalonzo aliahidi kuunga mkono ndoto ya ugavana ya mbunge huyo huku akiahidi kumtunuku “cheo kikubwa” endapo atajiunga rasmi na Wiper.
“Babu ikiwa mambo yataenda mrama katika ODM na muungano wa Azimio, nakukaribisha Wiper. Tunapanga kubadilisha katiba yetu na kupanua safu ya uongozi na utapata nafasi moja kubwa,” Bw Musyoka akaeleza.
Lakini wachanganuzi wanasema azma ya Babu kushinda ugavana wa Nairobi kwa tiketi ya Wiper haitakuwa rahisi kufikiwa kutokana na sababu kadhaa.
Kwanza, kwa mujibu wa Bw Martin Andati, viongozi wa upinzani tayari wamekubaliana kuhusu namna watakavyogawana viti vikubwa, kikiwemo kiti cha ugavana wa Nairobi.
“Mpango wa mrengo wa upinzani unaoshirikisha Rigathi Gachagua, Kalonzo Musyoka, Eugene Wamalwa, Justin Muturi na Martha Karua, ni kwamba kiongozi huyo wa Wiper ndiye atapeperusha bendera yao ya urais.
“Kwa hivyo, yule watakayemuunga mkono kwa wadhifa wa Gavana wa Nairobi sharti awe ni mtu kutoka Mlima Kenya. Hiyo inadidimisha uwezekano wa Babu kupata uungwaji mkono kutoka kwa mrengo huo,” anaeleza.
Mnamo Aprili mwaka huu, mbunge huyo anayehudumu muhula wa tatu alisisitiza kuwa atawania ugavana wa Nairobi hata bila kudhaminiwa na chama chake cha ODM.
Hii ni baada ya kiongozi wa chama hicho Raila Odinga kuonekana kuunga mkono kuchaguliwa tena kwa Gavana wa sasa Johnson Sakaja.
“Ninafahamu kwamba ODM haitanipa tiketi kwa sababu Johnson Sakaja aliidhinishwa katika ukumbi wa Bomas. Pili, naelewa kwamba nachukiwa kwa kupinga Serikali Jumuishi,” Bw Owino akasema, akirejelea hatua ya Odinga kumwidhinisha Sakaja katika ibada maalum iliyoandaliwa Bomas of Kenya Februari 5, 2005 kumwomba fanaka katika kinyang’anyiro cha uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
“Ninaikosoa Serikali Jumuishi kwa sababu ni vizuri kufanya hivyo. Kama kiongozi, siwezi kushuhudia mabaya yakitendeka kisha nijitokeze hadharani kuunga serikali. Siwezi kufanya hivyo, hata faraghani,” akaongeza.