Ichungwah, Osoro wakata rufaa uamuzi kuhusu walio wengi kuokoa kazi zao
MZOZO kuhusu ni mrengo upi ulio wa Wengi na ulio wa Wachache Bungeni umefika katika Mahakama ya Rufaa baada ya wabunge wanne wa UDA kuwasilisha rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu uliofutilia mbali uamuzi wa Spika Moses Wetang’ula aliyeteua Kenya Kwanza kuwa muungano wa walio wengi.
Bunge la Kitaifa pia limewasilisha rufaa tofauti dhidi ya uamuzi huo huo, likisema uamuzi wa Mahakama Kuu ulizua mtafaruku katika Bunge hilo na kuathiri shughuli zake.
Wabunge hao wanne wakiongozwa na Kimani Ichungw’a (Kiongozi wa Wengi) wanahoji kuwa Mahakama Kuu ilishindwa kuzingatia athari kubwa za uamuzi wake kama vile watu waliopewa jukumu la kuhudumu katika afisi za viongozi wa Wengi na Wachache.
Bw Ichungwah aliwasilisha rufaa hiyo pamoja na wabunge Owen Baya (Naibu Kiongozi wa Wengi), Sylvanus Osoro (Kiranja wa Wengi) na Naomi Jillo Wako (Naibu Kiranja wa Wengi).
Bunge la Kitaifa na wabunge hao wanataka Mahakama ya Rufaa isitishe haraka utekelezaji wa hukumu iliyotolewa Februari 7, 2025 na majaji Jairus Ngaah, John Chigitti na Lawrence Mugambi.
‘Tunaomba kwa dharura, kesi hii iwekwe mbele ya rais wa Mahakama ya Rufaa, ateue jopo kesi isikilizwe kwa kuwa shughuli za Bunge zimetatizika sana baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu tunaotaka isitishwe,’ wakili Sandra Nganyi, wa Bunge la Kitaifa, alisema katika barua kwa Naibu Msajili wa mahakama hiyo.
Mkanganyiko
Wanasema kuwa uamuzi huo ulizua mkanganyiko, na mvutano kuhusu Walio Wengi na Wachache na kwamba uliingilia shughuli na utaratibu wa Bunge.
Wabunge hao wameiomba mahakama itambue kuwa afisi zote mbili za uongozi wa walio wengi na walio wachache huwa na watumishi walio na kandarasi ambao kazi zao zinategemea viongozi walio ofisini.
“Hivyo basi, uamuzi wa Mahakama Kuu unahatarisha kazi za watumishi hao iwapo utekelezaji wa uamuzi huo hautasitishwa,” walisema wabunge hao.
Karani wa Bunge la Kitaifa Samuel Njoroge, katika hati ya kiapo ya kuunga mkono rufaa hiyo, anasema kwamba bila maagizo ya kusimamisha uamuzi huo, ‘madhara yatakayotokea kwa shughuli za Bunge hayataweza kurekebishwa.
Bw Njoroge aliongeza kuwa ingawa Spika Wetang’ula alitoa uamuzi mwingine Februari 12 akitangaza muungano wa Kenya Kwanza kuwa Mrengo wa Wengi, mwanachama wa Azimo la Umoja One Kenya Milie Odhiambo alisema Azimio haikubaliani na uamuzi huo na kwamba watachukua hatua zaidi.
Azimio pia iliwaondoa wanachama wake kutoka Kamati ya Shughuli za Bunge na wabunge kadhaa wa chama pia walitoka nje ya Bunge.
‘Ni kwa manufaa ya umma kwamba mkanganyiko na athari mbaya zilizosababishwa na uamuzi wa Mahakama Kuu zinafaa zirekebishwe na mahakama hii,’ alisema Bw Njoroge.
Rufaa inasubiri kusikilizwa.