Jamvi La Siasa

Ikulu yageuka hekalu ya kuvuna mapocho pocho

Na JUSTUS OCHIENG' September 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

Rais William Ruto amekuwa akifungua milango ya Ikulu ya Nairobi kwa makundi mbalimbali kukutana naye moja kwa moja, kuanzia viongozi wa dini, vikundi vya wanawake, vijana na hata viongozi wa kisiasa. Sera hii ya mlango wazi inalenga kuwahusisha wananchi moja kwa moja katika utawala.

Hata hivyo, sera hii imezua malalamishi, hasa kuhusu gharama kubwa inayotumika kuandaa mikutano hii, ambayo inafyonza fedha za walipa kodi.

Jumatano iliyopita, Rais Ruto alikaribisha viongozi wa kaunti ya Murang’a Ikulu, siku moja tu baada ya kukutana na viongozi wa eneo la Gusii, hafla iliyohudhuriwa na kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Rais alisema, “hakuna tena nafasi ya siasa zinazowafaidi wachache kwa gharama za wengi. Tunapanga mwelekeo mpya; uongozi jasiri, wa maono, unaobadilisha maisha na kuunganisha taifa.”

Mkutano mkubwa zaidi unaotarajiwa kufanyika ni leo, Septemba 13, wakati Rais atakapoalika walimu takriban 10,000 Ikulu. Kila mwalimu anatarajiwa kupokea kiasi cha Sh10,000 kwa usafiri, jambo litakalogharimu zaidi ya Sh100 milioni kwa siku moja tu. Vyanzo vya habari vimeripoti kwamba baadhi ya viongozi wa vikundi hupokea hata Sh200,000 kila mmoja huku wengine wakipokea Sh5,000 tu.

Hii imezua malalamishi makali kwamba mikutano hii inalenga kuunda makundi ya kisiasa yanayogawanya jamii badala ya kuleta uongozi wa kweli, wenye busara na wa maendeleo endelevu. Afisa wa chama kikuu cha taifa aliambia Taifa Leo: “Mikutano hii ni ya kujenga makundi madogo ndani ya jamii. Tunahitaji uongozi unaokubalika, badala ya kuchagua viongozi wachache wanaopokea pesa kutoka Ikulu kisha kuondoka.”

Ripoti ya hivi karibuni kutoka kwa Mdhibiti wa Bajeti, Dkt Margaret Nyakang’o, ilionyesha kuwa Wizara ya Fedha ilitoa Sh3.6 bilioni kwa usafiri, mikutano na ukarimu katika kipindi cha siku 42 tu kati ya Mei 14 na Juni 24, 2025 muda mfupi kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha.

Fedha hizi zilipatikana chini ya kifungu cha Katiba cha 223 kinachoruhusu matumizi ya dharura bila idhini ya Bunge. Hata hivyo, Dkt Nyakang’o alionya kwamba matumizi haya kwa shughuli za kawaida yanaonyesha dosari katika upangaji wa bajeti na ni kinyume na sheria ya fedha za umma. Kati ya Sh3.6 bilioni, ni Sh2.3 bilioni tu zilizoidhinishwa rasmi.

Katika kipindi hicho, Rais Ruto alikutana na makundi mengi tofauti Ikulu Nairobi na katika Ikulu ndogo mbali mbali nchini. Mnamo Juni 24, alikaribisha mabingwa wa michezo ya soka na voliboli wa Idara ya polisi, huku akiwapongeza kwa kushinda mataji ya Ligi Kuu ya FKF. Siku moja kabla, alipokea wawakilishi wa Wakenya wanaoishi ng’ambo kutoka nchi 27 ambapo alishukuru Wakenya walioko nje kwa kutuma nyumbani Sh638 bilioni mwaka jana.

Mnamo Juni 18, Gavana wa Kisumu Anyang’ Nyong’o aliongoza viongozi wa kaunti, viongozi wa dini na wataalamu Ikulu, ambapo Rais pia aliahidi kuendeleza mradi wa samaki na uchumi wa majini. Juni 11, alikutana na viongozi wa mashinani kutoka Nakuru pamoja na gavana Susan Kihika na Waziri Lee Kinyanjui, mkutano uliolenga mageuzi ya usalama.

Viongozi wa dini wamekuwa wakizuru ikulu kwa wingi, wakiwemo zaidi ya wawakilishi 600 wa makanisa ya Kipentekoste, na mnamo Mei 23 alikutana na viongozi wa waumini wa madhehebu mengine. Alikutana na wasanii Juni 9, huku viongozi wa Maendeleo ya Wanawake wakimtembelea Mei 22.

Mikutano mingine ilikuwa na muktadha wa kaunti. Mnamo Juni 5, wabunge wa magharibi walikutana Ikulu kujadili mabadiliko ya sekta ya sukari, huku siku hiyo hiyo viongozi wa Siaya wakikutana na Rais, alipotoa ahadi za uwekezaji mkubwa katika bandari, masoko na umeme.

Mnamo Mei 31, alipokea viongozi wa mashinani kutoka Homa Bay, na Mei 27 viongozi wa kanda ya Pwani wakamtembelea kujadili mageuzi kuhusu ardhi na mradi wa uchumi wa majini. Mnamo Mei 21, viongozi kutoka Ukambani walipokea ahadi za kuharakisha miradi ya maendeleo walipozuru Ikulu ya Nairobi.

Rais Ruto amedai mikutano hii ni sehemu ya “utawala unaolenga watu,” lakini wakosoaji wanasema kasi na gharama ya mikutano hii ni siasa za kupendelea zinazotumia fedha za walipa kodi kiholela.

Wachunguzi wa bajeti wanasema mamilioni ya pesa zinatolewa kwa ruzuku, usafiri, chakula na maandalizi ya mikutano. Wakosoaji wanahofia kuwa wakati nchi inalemewa na madeni makubwa na gharama ya maisha inaongezeka, matumizi haya yanaonekana kuvutia kisiasa lakini ni hatari kiuchumi.

Profesa Gitile Naituli wa Chuo Kikuu cha Multimedia anataja mikutano ya Ikulu kama “mikutano inayolipwa.” Anasema, “mikutano hii inafadhiliwa kwa fedha za walipa kodi ili kununua uungwaji mkono.” Profesa Naituli anafichua kuwa baadhi ya viongozi walipata hadi Sh50,000 kila mtu, na kueleza kuwa mikutano hii ni kufyonza rasilmali na serikali inahitaji ushauri bora kuhusu maana ya kuwawezesha wananchi.

Profesa Naituli anataja mikutano hii kama jaribio la kuanzisha upya mbinu za zamani za Kanu kama YK92, ambapo watu walilipwa pesa nyingi kupiga kura, jambo lililopelekea mfumuko wa kutisha.

Upinzani na mashirika ya kijamii wanamkosoa Rais Ruto kwa kutumia pesa za Ikulu kwa siasa za kununua watu, lakini Rais anasimama imara akisema Ikulu ni mali ya wananchi na mikutano hii ni sehemu ya dhamira yake ya “utawala unaolenga watu.”