Itakuwa nusu mkate na UDA 2027, ODM yaahidi wafuasi
CHAMA cha ODM kimewahakikishia wafuasi wake kuwa hakitapoteza ngome zake za kisiasa licha ya kifo cha aliyekuwa kiongozi wake Raila Odinga na ushirikiano wake na chama tawala cha UDA kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Viongozi wa chama hicho wamesema wanapania kushinda viti vingi vya magavana, maseneta, wabunge na wawakilishi wadi ili kuimarisha uwezo wao wa kujadiliana kuhusu ugavi wa mamlaka katika serikali ijayo.
Akizungumza na wajumbe wa ODM katika Kaunti ya Turkana mjini Lodwar Ijumaa usiku, mwenyekiti wa chama Gladys Wanga alisema chama hicho kimeimarika baada ya kupitia kipindi kigumu kufuatia kifo cha Raila.
Alisema ODM na UDA zinatarajiwa kuunda serikali kwa usawa wa asilimia 50 kwa kila chama, huku UDA ikichukua urais na ODM kupewa nafasi ya naibu wa rais.
“Ni kawaida kupitia misukosuko tuliyopitia. Sasa tumetulia na tumetambua kuwa wengi wa wafuasi wetu bado wako ndani ya chama. Msitishwe na kulazimishwa kuondoka,” alisema Wanga.
Aliongeza kuwa ODM italazimika kushinda viti vingi vya uchaguzi ili iwe na nguvu za kudai nafasi muhimu serikalini, zikiwemo nyadhifa 10 za mawaziri.
Wanga alisema pia chama hicho kinalenga kuhifadhi nafasi ya Waziri inayoshikiliwa na Beatrice Askul, ambaye aliteuliwa kwa ushawishi wa Raila.
Alisema ODM inaendeleza ushirikiano na viongozi wa mashinani ili kuhakikisha kinashinda viti vingi Turkana na kufanya vizuri katika muungano wa serikali jumuishi.
Katibu mkuu wa ODM, Catherine Omanyo, aliwataka wajumbe kuepuka migogoro ya ndani, akisisitiza kuwa chama ni kikubwa kuliko mtu mmoja na kinapaswa kuimarishwa ili kuvutia wanachama wapya.
Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed alisema Turkana bado ni ngome ya ODM, licha ya Gavana Jeremiah Lomorukai kuondoka katika chama hicho.
Alisema chama hicho kinalenga kuhakikisha mmoja wa wabunge wa Turkana Kaskazini, Ekwom Nabuin, au Turkana Kusini, Ariko Namoit, anachukua nafasi ya Lomorukai katika uchaguzi ujao.
“Tumekuwa na gavana wa ODM Turkana tangu 2013, na mwaka 2027 gavana atatoka ODM tena,” alisema Mohammed.
Aliongeza kuwa iwapo UDA itashinda uchaguzi wa 2027, ODM itakuwa na nafasi ya kuwania urais mwaka 2032.
Naibu kiongozi wa ODM Simba Arati alisema chama hicho kitafanya uteuzi wa haki na huru ili kumchagua mgombea wake mapema na kuanza kampeni za kurejesha ugavana Turkana.
Alisema ODM pia itaimarisha miundo yake ya mashinani ili kukabiliana na ushindani kutoka kwa wagombea wenye uwezo mkubwa wa kifedha.
Raila Odinga Junior aliwataka viongozi kubaki pamoja na kuendeleza urithi wa babake wa kutetea maendeleo ya usawa kupitia serikali jumuishi.