Jamvi La Siasa

Jaramogi: ‘Baba wa Upinzani’ kabla na hata baada ya Kenya kupata uhuru

Na BENSON MATHEKA September 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 3

KATIKA historia ya siasa za Kenya, jina la Jaramogi Ajuma Oginga Odinga halifutiki kamwe.

Kwa wengi, yeye ndiye baba wa upinzani wa kweli nchini. Alisimama kidete kwa haki, usawa na demokrasia tangu enzi za ukoloni hadi baada ya nchi kupata uhuru.

Jaramogi alizaliwa mwaka wa 1911 katika kijiji cha Nyamira, eneo la Sakwa, Kaunti ya Siaya.

Alipata elimu katika shule ya Maseno na baadaye Alliance kabla ya kuelekea Makerere College nchini Uganda kusomea ualimu.

Akiwa mwanafunzi na baadaye mwalimu, aliibua maswali kuhusu ukandamizaji, ubaguzi na dhuluma za kijamii zilizokuwepo.

Alifundisha katika shule ya Maseno chini ya mkuu wa shule maarufu, Carey Francis. Hata hivyo, msimamo wake mkali dhidi ya ukoloni na matumizi ya majina ya Kikristo ulimletea misukosuko.

Aliacha jina lake la biblia “Adonijah” na kuchukua jina la Kiafrika “Ajuma,” ishara ya kupinga ukoloni wa kiakili.

Baada ya kuacha ualimu, alijitosa katika biashara na uongozi wa kijamii kupitia shirika la Luo Thrift and Trading Corporation na Luo Union, taasisi zilizolenga kuinua jamii ya Wajaluo na kuhimiza mshikamano wa Waafrika katika Afrika Mashariki.

Jaramogi alianza kujihusisha rasmi na siasa mwaka wa 1947 alipochaguliwa katika mabaraza ya ushauri ya wilaya na eneo la Sakwa.

Lakini ilikuwa hadi 1957 alipoingia baraza la kutunga sheria (LegCo), akiwa miongoni mwa Waafrika wanane wa kwanza kuchaguliwa. Katika kundi hili kulikuwa pia na Tom Mboya, Daniel Moi, Masinde Muliro na Ronald Ngala.

Hawa waliunda African Elected Members Organisation (AEMO), Odinga akiwa mwenyekiti na Mboya katibu.Jaramogi alijulikana kwa msimamo wa kijamaa.

Aliamini kuwa ujamaa ungewezesha kusawazisha fursa kwa wote na kuinua maisha ya maskini.

Alikuwa na urafiki wa karibu na viongozi wa kisiasa wa mataifa ya kijamaa kama China, Urusi na India. Katika safari yake rasmi nchini India, alialikwa na Waziri Mkuu Jawaharlal Nehru.

Ziara hiyo ilizua tuhuma kwamba alipanga njama ya kisiasa dhidi ya utawala wa kikoloni, kiasi cha kuhojiwa usiku wa manane na maafisa wa usalama baada ya kurejea nchini.

Baada ya Kenya kupata uhuru mwaka wa 1963, Jaramogi aliteuliwa kuwa Waziri wa Masuala ya Ndani. Mwaka mmoja baadaye, alipokuwa Makamu wa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Kenya, tofauti za kisera kati yake na Rais Jomo Kenyatta zilianza kujitokeza.

Wakati Odinga alisisitiza usawa wa kiuchumi na kugawia maskini ardhi, serikali ya Kenyatta ilielekeza maendeleo zaidi kwa mabwanyenye na matajiri wachache waliounga mkono serikali.

Mwaka wa 1966, aliponyimwa mamlaka ndani ya chama cha Kanu kupitia mabadiliko ya katiba ya chama yaliyoanzisha manaibu wa rais kwa kila mkoa, aliamua kujiondoa serikalini na kuunda chama cha upinzani – Kenya People’s Union (KPU).

Hili lilikuwa tukio la kihistoria kwa sababu Jaramogi alikuwa mwanasiasa wa kwanza nchini kuanzisha chama cha upinzani baada ya uhuru.

Wafuasi wake kama Achieng’ Oneko na Bildad Kaggia walihamia naye KPU, chama ambacho kilikumbana na ukandamizaji mkubwa wa serikali.

Mikutano yao ilizuiwa, viongozi wao waliwekwa kizuizini na chama kikapigwa marufuku mwaka 1969, kufuatia mkutano wa Kisumu ulioishia kwa ghasia kati ya wafuasi wa Odinga na walinzi wa Kenyatta.

Kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10, Jaramogi alifungiwa kabisa katika siasa za kitaifa. Alirejea tena miaka ya 1980 akishinikiza kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi.

Hadi alipofariki mwaka 1994, Jaramogi alibaki kuwa sauti ya upinzani, haki na demokrasia.

Alianzisha chama cha FORD-Kenya kilichoshiriki katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1992.Jaramogi aliishi kama mwanasiasa wa msimamo, asiyeogopa kusema ukweli au kujipendekeza.

Katika kitabu chake cha Not Yet Uhuru, anaandika: “Uhuru haujapatikana kikamilifu, kwani wananchi bado wanakumbwa na njaa, ukosefu wa elimu, huduma duni na umaskini. Uhuru wa kweli utapatikana tu pale kila Mkenya atakapoishi kwa heshima na usawa.”

Leo, jina lake linaenziwa sio tu kwa kuwa baba wa Raila Odinga, kiongozi mashuhuri wa upinzani, bali kwa kuwa alisimama imara wakati ambapo wengi walinyamaza.

Ni vigumu kuzungumzia historia ya Kenya bila kumtaja Jaramogi – mwanasiasa aliyeamini kuwa siasa ni kwa ajili ya kuwatumikia watu, si kujitajirisha.

Kwa hakika, Jaramogi alikuwa na maono ya taifa lenye haki, usawa, na mshikamano. Wakenya wa leo wana mengi ya kujifunza kutoka kwa maisha na falsafa zake.