Jamvi La Siasa

Jinsi Kamala Harris alivyoingia mitini na kuacha wafuasi kwa mataa alipogundua hatashinda

Na MASHIRIKA November 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MAKAMU wa rais wa Amerika Kamala Harris alionekana kukimya baada ya kugundua kuwa hataibuka mshindi katika uchaguzi mkuu nchini humo uliokuwa na ushindani mkubwa.

Harris alitazamiwa kutoa hotuba Jumanne usiku na hata kuhudhuria karamu ya kusherehekea uchaguzi ila hayo yote hayakufanyika.

Hata hivyo, alilazimika kuahirisha hotuba yake alipoona kuwa mpinzani wake mkuu Donald Trump wa Republican alikuwa kifua mbele katika baadhi ya majimbo muhimu.

Hiyo Jumatano, waandishi wa habari waliopiga simu wakitaka kupata taarifa kutoka kwa timu ya Harris walielezwa kuwa timu hiyo haiwezi kutoa taarifa kwani simu nyingi za serikali zilikuwa zikipokelewa wakati huo.

Wakati huo huo, waandishi wa habari wa CNN katika makao makuu ya kampeni ya Harris Washington DC walisema kwamba hawakupokea taarifa yoyote kutoka kwa timu ya mgombea huyo wa Democratic.

Hata wafuasi wake ambao walikuwa wamekusanyika katika chuo kikuu cha Howard waliachwa kwa mataa.

Mwenyekiti mwenza wake wa kampeni, Cedric Richmond, alihutubia umati akisema Harris atazungumza hadharani siku ya Jumatano.

“Bado tuna kura zinazoendelea kuhesabiwa,” Richmond aliambia wanahabari.

Baadaye, kanda za video kutoka kituo cha uchaguzi cha Chuo Kikuu cha Howard zilionyesha umati wa watu ambao ni wafuasi wa Harris wakiondoka kwenye ukumbi huo kwa wingi baada ya kuona dalili kuwa Harris hangewahutubia.

Kufikia wakati ilipothibitishwa kuwa Kamala Harris hatahudhuria karamu yake ya usiku wa uchaguzi, wafuasi wake wengi walikuwa tayari wamepokea ujumbe huo na walikuwa wakitoka moja baada ya mwingine.

Wakati huo huo, na kwa mujibu wa katiba ya Amerika, mshindi katika uchaguzi wa urais hubainika kutokana na idadi ya kura ambazo mgombeaji hupata kutoka majimbo 52 nchini Amerika wala sio idadi jumla ya kura kitaifa.

Majimbo hayo yako na jumla ya kura 538 na hivyo mgombeaji anahitaji kupata angalau kura 270 za wajumbe ili aibuke mshindi.

Idadi ya kura katika kila jimbo hukadiriwa kulingana na wingi wa wapiga kura katika jimbo fulani.

Chini ya mfumo huu, idadi ya kura za wajumbe katika jimbo fulani ni sawa na idadi ya wabunge wake; moja kwa kila mbunge katika bunge la wawakilishi na maseneta wawili.

Jimbo la California lenye kura 54 za wajumbe ndilo lenye idadi kubwa zaidi la wapiga kura linafuatwa na majimbo kama vile Texas (kura 40) na Florida lenye kura 30.

Kando na majimbo ambayo ni ngome za vyama viwili vikuu, Democratic na Republican, kuna majimbo saba yasiyoegemea mirengo hiyo miwili na ambayo ndio huamua mshindi katika chaguzi za urais Amerika.

Majimbo hayo ni; Pennsylvania, Georgia, North Carolina, Michigan, Arizona, Wisconsin na Nevada.

Katika uchaguzi wa urais Jumanne wiki, Donald Trump alishinda kwa misingi kuwa alimshinda Kamala Harris katika nyingi za majimbo haya saba.

Trump aliyewania kwa tiketi ya chama cha upinzani Republican aliibuka mshindi kwa kupata kura 277 za wajumbe huku Bi Harris wa chama cha Democratic akipata kura 224.

Hii ilitokana na ushindi ambao rais huyo wa zamani aliandikisha katika majimbo ya Pennsylvania (yenye kura 19 za wajumbe), Georgia (16), North Carolina (16) na Michigan yenye kura 15.

Imetafsiriwa na BENSON MATHEKA