Trump ‘alivyopita nayo’ na kuduwaza ulimwengu
RAIS mteule Donald Trump jana alionyesha ushujaa wa kipekee baada ya kuvuka vizingiti vya kisiasa vilivyomkabili na kurejea mamlakani, akimbwaga Makamu wa Rais Kamala Harris kama rais wa 47 wa Amerika katika uchaguzi uliofanyika Jumanne.
Licha ya siasa zake kuwa za utata kutokana na matamshi yaliyofasiriwa kuzua chuki dhidi ya wahamiaji na Waamerika weusi, Trump ambaye ni mfungwa, alipitisha idadi ya majimbo 270 ambayo yanahitajika kwa mshindi kutangazwa rais Amerika.
Kushinda uchaguzi huo wa Jumanne sasa kuna maana kuwa ataapishwa mnamo Jumatatu Januari 2025 pamoja na Makamu wa Rais Mteule JD Vance.
Wengi wanasubiri iwapo Rais wa sasa Joe Biden ataweka uzalendo mbele na kumpokeza rasmi mamlaka.Baada ya kubwagwa na Rais Biden mnamo 2020, Trump hakujitokeza wakati wa kuapishwa kwa Rais Biden ambaye amekuwa hasimu wake mkuu wa kisiasa.
Trump, 78, alikuwa Rais wa Amerika kati ya 2016-2020 na katika uchaguzi wa 2016 alimbwaga Hillary Clinton, mke wa rais wa zamani Bill Clinton aliyekuwa akipigiwa upato kushinda kwa kuwa alikuwa akiongoza kwenye kura mbalimbali za maoni.
Katika uchaguzi wa mwaka huu Harris, 60, na Trump walikuwa sako kwa bako, japo matokeo ya kura mbalimbali za utafiti yalikuwa yameweka Harris mbele kwa asilimia ndogo sana.
Harris alipata nafasi ya kuwania Urais wa Amerika baada ya Rais wa sasa Joe Biden kujiondoa kwenye kinya’nganyiro cha Urais mnamo Julai 24 kutokana na ukongwe.
Kujiondoa kwa Rais Biden pia kulichangiwa na kulemewa kwake kwenye mdahalo ambao walishiriki na Trump mnamo Juni 28.
Trump alikuwa akiwania kupitia Republican na amekuwa akiendesha kampeni ambayo imekuwa na kauli mbiu ya kurejeshea Amerika hadhi yake ya zamani.
Ni hili linakisiwa kumrejesha mamlakani baada ya kupigwa kumbo na Biden kwenye kura za 2020.Akihutubu jana, Trump aliwashukuru wafuasi wake, akisema wakati huu sasa ni wa kuboresha Amerika akionekana kutoka kwenye cheche kali za kisiasa alivyozoeleka.
“Tuna marafiki wengi kwenye vuguvugu hili na tusaidie nchi yetu kupona kutoka kwa siasa kali na uongozi mbaya. Hatutapumzika hadi tuhakikishe kuwa tumeipeleka Amerika mahali ambapo inastahili kuwa,” akasema akiwa ameandamana na makamu wa rais mteule JD Vance na familia yake jimbo la Florida.
“Hakuna kitu ambacho kitanizuia kutimiza ahadi zangu na sote tutahakikisha Amerika inakuwa salama, huru, inaonyesha ubabe wake wa kiutawala na inastawi,” akaongeza.
Kando na kushinda Urais, Trump pia sasa atadhibiti Bunge la Seneti ambapo Republican ilishinda viti 51 kati ya viti vyote 100 hii ikiwa mara ya kwanza chama tawala itakuwa ikitawala bunge hilo baada ya miaka minne.
“Namwomba kila raia katika taifa letu ajiunge nami kwa sababu sasa ni wakati wa kuweka nyuma mgawanyiko ambao umekuwepo kwa miaka minne iliyopita. Ni wakati wa kuungana na kusukuma taifa letu mbele ili sote tufanikiwe,” akasema huku akimwomba Mwenyezi Mungu aibariki Amerika.
Akiendelea kusherehekea ushindi, ufanisi huo haukuja rahisi kwa kiongozi huyo ambaye nusura apoteza maisha yake mnamo Julai 14.
Akihutubia mkutano wa kisiasa jimbo la Pennsylvania alilengwa kwa risasi ambayo ilimpata sikioni akigusia masuala yanayohusu wahamiaji haramu.
Ilibidi azingirwe na walinzi ambao walimuinua damu ikibubujika sikioni mwake naye akiwaambia wafuasi wake wapigane.
Kampeni zake zilionekana kuwa na msisimko zaidi baada ya tukio hilo huku aliyempiga risasi kwa kupanda kwenye paa ya jengo kando na ua alikokuwa akihutubu, akipigwa risasi na kuuawa papo hapo.
“Watu wengi wameniambia kuwa Mungu alinusuru maisha yangu kwa sababu alitaka niokoe taifa letu na kurejesha hadhi ya Amerika. Naahidi kuwa nitatimiza hilo,” akasema.
Jumatano, alimsifu bilionea na mmiliki wa mtandao wa X Elon Musk na Robert F Kennedy Jr ambao walimuunga mkono na kutelekeleza wajibu muhimu kwenye kampeni zake.
Kennedy Jr mnamo Agosti 23 alijiondoa kwenye kinyángányiro cha urais na kutangaza uungwaji mkono kwa Trump.
Kennedy Jr. 70 alikuwa mwanachama wa Democrats kwa miaka mingi ya siasa zake na ni mwanawe Seneta Robert F Kennedy na mpwa wa Rais wa zamani wa Amerika John F Kennedy ambao wote walikuwa viongozi wakuu kwenye siasa za Democrats.
“Ni mtu mzuri sana na anataka kufanya baadhi ya mambo na tutamruhusu afanye hivyo,” akasema Trump akimrejelea Kennedt Jr na jina lake jingine la Bobby.
Musk, mtu tajiri zaidi duniani pia alifadhili kampeni za Trump na kwa kipindi fulani alisema kuwa alikuwa akihatarisha maisha yake kuhakikisha kuwa Trump anarejea Ikulu ya White House.
“Ni mtu mwerevu sana, mweveruvu zaidi na hatuna watu wengi kama yeye ndiposa lazima tumlinde,” akasema Trump.
Musk alikuwa ametumia Sh15.2 bilioni kwenye kampeni za Trump kufikia Oktoba 16. Pia alishukuru naibu wake JD Vance ambaye walishirikiana naye bega kwa bega katika kampeni hizo na kupata ushindi.
Huku Trump akihutubu na kusherehekea ushindi wake, Rais Joe Biden au Kamala Harris hawakuwa wametoa taarifa zozote, ikiwa ni dhahiri kuwa hasimu wao mkuu wa kisiasa sasa ataingia mamlakani.
Wengi pia wanasubiri kuona iwapo Trump sasa atafungwa mnamo Novemba 26 baada ya kupatikana na hatia kwenye mashtaka 34.