Joho, Kingi, Mvurya wawania kuwika Pwani
Siasa za ukanda wa Pwani zimekuwa katika hali ya mabadiliko, hususan baada ya uchaguzi mkuu wa 2022 ambapo viongozi kadhaa walibadilisha misimamo yao ya kisiasa, na wengine wakapata nafasi za juu serikalini.
Katika hali hii ya kisiasa iliyojaa ushindani na mvutano baina ya vyama vikuu — ODM na UDA — swali kuu linaibuka kuhusu ni nani anayestahili kuwa msemaji wa siasa za Pwani.
Kwa muda mrefu, Ali Hassan Joho, aliyekuwa Gavana wa Mombasa, alionekana kama sauti ya Pwani katika siasa za kitaifa. Ukaribu wake wa muda mrefu na kinara wa ODM Raila Odinga, pamoja na nafasi yake kama Naibu Kiongozi wa chama hicho, vilimweka kwenye mstari wa mbele. Joho alikuwa akionekana kama mwanasiasa shupavu asiyeogopa kusema ukweli, hasa alipozungumzia masuala ya Pwani, ubaguzi wa kiuchumi, au masuala ya ardhi.
Kujiunga kwake serikalini kama Waziri wa Madini, Uchumi wa Majini na Masuala ya Baharini kulimfanya mmoja wa viongozi wakuu katika utawala wa sasa wa Rais William Ruto pamoja na Spika wa Seneti Amason Kingi na Waziri wa Michezo Salim Mvurya ambaye kama Joho na Kingi, alihudumu kama gavana wa Kwale kwa mihula miwili.

Licha ya Joho kufurahia wadhifa huo uliomkweza hadhi, hatua hiyo ilionekana kama sehemu ya Rais Ruto kuvunja nguvu ya ODM eneo la Pwani ambalo washirika wake walioshikilia nyadhifa za juu serikalini walikuwa Kingi na Mvurya.
Wachanganuzi wanasema Joho anaonekana kulenga kudumisha nafasi yake kama msemaji wa eneo hilo kwa kusisitiza kuwa atagombea urais.
“Tutamuunga William Ruto mkono na kumpigia debe. Akitimiza mwaka 2032, basi tutakuwa tukisubiri hicho kiti,” Joho alisema akiwa Garsen, Tana River mapema wiki hii. Kauli hii ilituma ujumbe mzito kuwa bado anajiona kama msemaji wa eneo lake, licha ya ushirikiano kati ya ODM na serikali ya Kenya Kwanza.
Kwa upande mwingine, Amason Kingi, Spika wa Seneti na kiongozi wa chama cha PAA (kilichoungana na UDA), amejiimarisha kisiasa kupitia wadhifa wake kitaifa.
Akiwa Spika, ana ushawishi mkubwa bungeni, na ni mmoja wa viongozi wachache wa Pwani walioko kwenye mstari wa mbele katika utawala wa sasa. Ingawa haonekani mara kwa mara kwenye majukwaa ya kisiasa ya Pwani, nafasi yake serikalini inampa uzito wa kipekee.
“Tofauti na Joho, Kingi ana chama cha kisiasa ambacho alitumia kujadiliana kupata wadhifa wake wa sasa. Hata hivyo, ODM ambayo Joho ni mwanachama na ambayo alikuwa naibu kiongozi ni maarufu Pwani, ikiwemo Kilifi anakotoka Kingi na ambako alihudumu kama gavana kwa miaka kumi,” asema mchanganuzi wa siasa za pwani Paul Katana.
Anasema kuwa ushirikiano wa ODM na UDA umezidisha ushindani huku chama cha chungwa kikijitahidi kulinga ushawishi wake katika eneo la Pwani.

Ushirikiano wa ODM na serikali umeibua ushindani viongozi wakiwania kuwa msemaji. Wale wa ODM wanataka kudumisha ushawishi wao wakihisi UDA, kikiwa chama tawala, kinaweza kuufifisha, asema Katana.
ODM kina magavana watatu wa kaunti za eneo la pwani ambao ni Gedion Mung’aro wa Kilifi, Abdulswamad Nassir wa Mombasa na Dhadho Gaddae Godhana wa Tana River huku UDA ikiwa na mmoja ambaye ni Fatuma Achani wa Kwale.
“Kwa kuzingatia uzoefu, nafasi serikalini, na ushawishi kitaifa, Joho anaongoza kwa kuwa na sifa za msemaji wa siasa za Pwani. Kauli zake kali, uaminifu kwa chama chake, na dhamira ya kuwania urais vinamweka juu katika nafasi hiyo. Hata hivyo, Amason Kingi anaweza kuwa chaguo la kisiasa la serikali, akiwa na nafasi rasmi serikalini lakini akihitaji kuimarisha uhusiano wa karibu na wananchi wa kawaida wa Pwani,” asema Katana.
Anasema ikizingatiwa uaminifu na ushirika wake wa karibu na Rais Ruto, Waziri Mvurya ni mmoja wa wanaoweza kuwa sauti ya pwani.
Katika mazingira haya, msemaji halisi wa Pwani lazima awe mtu mwenye mizizi ya kweli miongoni mwa wananchi, lakini pia mwenye sauti inayosikika kitaifa na kwa sasa, Joho, Kingi na Mvurya ndio wanabaki kuwakilisha eneo hilo huku ushindani wa vyama ukionekana kuamua anayefaa kuwa msemaji wa Pwani.