Jamvi La Siasa

Jumwa asema ameacha UDA na kuhamia ‘chama cha pwani’ PAA ili kupigania ugavana kiurahisi

Na ANTHONY KITIMO December 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

CHAMA cha UDA mwezi huu kimepata pigo eneo la Pwani baada ya mmoja wa viongozi ambao walitumika kukipigia debe katika uchaguzi mkuu uliopita; Bi Aisha Jumwa kuhama na kujiunga na chama cha Pamoja African Alliance (PAA).

Kujiunga na PAA; chama ambacho kinahusishwa na Spika wa Seneti Amason Kingi na kutangaza kuwania kiti cha ugavana, kumevuruga siasa za kaunti hiyo na kutetemesha gavana wa sasa Bw Gideon Mung’aro.

Kutokana na hatua hiyo, vita vya ugavana Kilifi kwa sasa vitaonekana kuwa kati ya Bw Kingi ambaye ashampendekeza Bi Jumwa kuwania kupitia chama chake na Bw Mung’aro ambaye atatumia umaarufu wa chama cha ODM kuhifadhi kiti hicho.

Huku wanasiasa wakijipanga wakilenga uchaguzi mkuu wa 2027, chama cha PAA kinaonekana kuvuna vilivyo baada ya Spika Kingi kudinda kushurutishwa kuvunjilia mbali chama chake kama viongozi wengine waliojiunga na serikali walivyofanya.

“Tayari tumepata viongozi wengi ambao wanataka kujiunga na chama cha PAA si tu Bi Jumwa. Tutawajulisha hivi karibuni. Kwa sasa tunanuia kupata viti katika nyadhifa mbalimbali kuanzia kwa gavana hadi madiwani, ila kwa kiti cha uraisi, tutaunga mkono Rais Ruto,” alisema Bw Sammy Nyundo, kiongozi wa vijana wa PAA.

Mchakato wa Wapwani kuwa na chama chao sasa unaonekana kuchukua mkondo mpya kwani viongozi wameanza kuasi vyama vinavyoonekana kuwa si vya eneo hilo.

Bi Jumwa ambaye alikuwa na wakati mgumu kupigia debe chama cha UDA eneo la Pwani kuvunja ngome ya ODM, alisema hatua yake ilisababishwa na kimya cha Rais William Ruto kuhusu chama hicho alipozuru Pwani majuzi.

Wakati wa ziara yake, Rais Ruto alionekena kupigia debe muungano wa UDA na ODM wala si chama chake.

“Nilibaki na maswali kuhusu kwa nini Rais Ruto hakuongelea cha UDA alipokuwa huku. Nilionelea kujiunga na PAA ambacho ni kimoja cha vyama tanzu serikalini,” alisema Bi Jumwa.

“Wanasiasa kuhama chama ni jambo la kawaida. Hata Rais Ruto amefanya hivyo mara kadhaa. Hata hivyo, chama cha PAA kiko katika serikali na hakuna kosa lolote nimefanya,” alisema Bi Jumwa.

Waziri huyo wa zamani anatarajiwa kuteuliwa naibu wa chama na kugombea kiti cha ugavana mwaka wa 2027 baada ya kupoteza nafasi hiyo mwaka wa 2022 ambapo alipata kura 65,893 dhidi ya Bw Mung’a ro ambaye aliibuka mshindi kwa kura 143,773.

Bi Jumwa ambaye alikuwa Waziri wa masuala ya jinsia kabla ya kufutwa kazi katika serikali ya Rais Ruto alisema aliona heri kuhamia chama kinachohusishwa na wenyeji anapolenga azma yake ya kumng’oa gavana wa sasa Bw Mung’aro.

Kujiunga kwake na PAA na iwapo atapata uungwaji mkono kutoka kwa aliyegombea kiti cha ugavana msimu uliopita kwa tiketi ya chama hicho Bw George Kithi na kupata kura 64,326 kutakuwa tishio kubwa kwa Bw Mung’aro ambaye chama hicho kinaonekana kuyumba baada ya kuaga dunia kwa kinara wake Raila Odinga.

Katibu mkuu wa UDA Hassan Sarai alisema tofauti na uchaguzi mdogo ambapo vyana tanzu vya serikali viliunga mkono ODM eneobunge la Magarini, mwaka wa 2027 kila chama kitawasilisha mgombeaji wake.

“Baada ya kuondoka kwa Bi Jumwa, tumemteua Bw Kahindi kuongoza chama hicho Kilifi na baadaye kumuunga mkono kuwania kiti cha ugavana,” alisema Bw Omar.

Bw Kahindi alihama ODM mwaka wa 2022 baada ya chama hicho kuteua Bw Mung’aro kuwa mgombeaji wake wa ugavana.

Katika uchaguzi wa Novemba 27, PAA na UDA kiliunga mkono mgombea wa ODM Bw Harry Kombe ambaye aliibuka mshindi dhidi ya Stanely Kenga wa DCP.