Jamvi La Siasa

Kalonzo ajizatiti sasa kukubalika eneo la Mlima Kenya

April 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

KIONGOZI wa Wiper anapojizatiti kuwa mrithi wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuboresha azma yake ya kuwania urais 2027, anaonekana kulenga zaidi uungwaji mkono katika eneo la Mlima Kenya.

Ni eneo hilo lenye kura nyingi ambako Bw Odinga amekuwa akijaribu kuvutia kwa miaka mingi ikiwemo 2022 ambapo alifaulu kuongeza kura alizopata licha ya kushindwa na mgombeaji wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), Dkt William Ruto.

Na sasa Bw Musyoka anamezea mate kura za eneo hilo la Mlima Kenya kiasi kwamba ameunda kundi linaloshirikisha wanasiasa, wanahabari na wafanyabiashara kumsaidia kufikia lengo hilo.

Aidha, amekuwa akifanya mikutano na viongozi wa eneo hilo wanaojumuisha wanachama wa Baraza la Wazee na waliokuwa wagombeaji viti kwa tiketi ya chama cha Jubilee.

Bw Musyoka, ambaye ni makamu wa rais wa zamani, vile vile katika siku za hivi karibuni amekuwa akifanya ziara kadhaa katika eneo la Mlima Kenya.

Anaonekana kulenga kuunganisha kaunti za Meru, Tharaka Nithi na Embu na zile za Ukambani (Machakos, Kitui na Makueni) ili kuweka msingi wa kampeni ya urais.

Bw Musyoka amefanya mashauriano na gavana wa zamani wa Meru Bw Kiraitu Murungi na viongozi wengine akijaribu kupata uungwaji mkono kama mrithi wa Bw Odinga na mgombeaji bora wa urais kumfanya Rais Ruto kuwa rais wa muhula mmoja 2027.

Kiongozi huyo wa Wiper, pia anapania kuonyesha kuwa ngome yake ya Ukambani inaweza kubuni muungano na Mlima Kenya.

Mnamo Februari 12, alizuru Kaunti ya Meru na kuwasihi wakazi kuungana na Ukambani kama eneo la Mashariki ili wajikomboe kisiasa.

Aliandamana na gavana wa zamani wa Meru, Bw Peter Munya, aliyetangaza kuwa “Kalonzo akaribia kuwa Rais.”

Bw Musyoka alisema eneo hilo la Mashariki mwa Kenya hutumika kuunga mkono wagombeaji kutoka eneo la Kati mwa Kenya na baadaye kutengwa wakati wa ugavi wa nyadhifa serikalini.

Wakati huo huo, wanasiasa wa muungano wa Kenya Kwanza wameanzisha juhudi za kuhimiza wakazi wa Mlima Kenya kumuunga mkono Rais Ruto kwa muhula wa pili na hivyo kutoa changamoto kwa mikakati ya Bw Musyoka.

Lakini Seneta wa Kitui, Bw Enoch Wambua, anasema: “Watu wa Mlima Kenya na Ukambani wamekuwa marafiki kwa muda mrefu na ni mashemeji.

Akaongeza: “Bw Musyoka anasifika kama mwanadiplomasia na hawezi kuwa tishio kwa uthabiti na biashara za wakazi wa Mlima Kenya na Wakenya kwa ujumla.”

Wadadisi wanasema kiongozi huyo wa Wiper anakabiliwa na kibarua kikubwa kuvutia wakazi wa Mlima Kenya upande wake, ikizingatiwa kuwa tangu mfumo wa vyama vingi urejelewe, hawajawahi kuunga mkono kambi yake (Musyoka).