Jamvi La Siasa

Kalonzo, Matiangi, Karua wahepa urejeo wa Gachagua

Na BENSON MATHEKA August 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KATIKA tukio lililotarajiwa kuwa la kishindo na kuonyesha mshikamano wao wakati wa kurejea nchini kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua viongozi wengine wa upinzani walikosa kufika katika uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) kumpokea.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Fred Matiang’i, Justin Muturi na Mithika Linturi, kiongozi wa Liberation Party of Kenya (PLP) Martha Karua na Eugene Wamalwa wa DAP-K hawakujitokeza katika uwanja huo.

Kukosekana kwao kunaibua maswali kuhusu umoja wa upinzani, huku wachambuzi wakitafsiri hali hiyo kama dalili ya mivutano ya ndani na kutoaminiana kuhusu nani anayestahili kumenyana na Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu ujao.

“Hii ni ishara kuwa upinzani haujawa na msimamo mmoja. Kuna wanaomuunga mkono, na wengine wanaona hafai kuwa kiongozi wa kitaifa,” alisema Dkt Joshua Wamwere, mchambuzi wa siasa.

Baadhi ya duru zasema viongozi hao hawakualikwa rasmi, huku wengine wakidokeza kuwa huenda walijitenga kimakusudi kwa sababu za kimkakati wasionekane kumuidhinisha kama mgombea urais wa upinzani.

Gachagua mwenyewe hakuzungumza katika hafla hiyo, wala kutoa mwelekeo wa kisiasa, hali ambayo iliibua maswali zaidi kuhusu nia yake na mpango wa kisiasa alio nao.

Katika hali ya kushangaza, baada ya kutoka uwanjani na kujiunga na msafara wa magari, Gachagua alikumbana na mashambulizi kutoka kwa wahuni katika eneo la Cabanas, ambapo mawe yalirushwa, magari kuvunjwa vioo, na walinzi wake kulazimika kumlinda vikali.

Viongozi waliokuwepo, akiwemo naibu kiongozi wa chama chake cha DCP, Cleopas Malala, walimlaumu Rais Ruto kwa kupanga vurugu hizo na kujaribu kumdhalilisha Gachagua.

Lakini ni kukosekana kwa vigogo  wa vyama vya upinzani ambao wamekuwa wakisisitiza kwamba wanaunda muungano wa kisiasa  kuteua mgombea mmoja wa urais kushindana na Rais Ruto kuliibua wasiwasi kuhusu mshikamano wao .

Kwa sasa, Gachagua anaonekana kuwa na ufuasi mkubwa wa wananchi wa kawaida hasa Mlima Kenya, lakini bila baraka na ushirikiano wa vinara wenzake wa upinzani, safari yake kuelekea 2027 inaweza kuwa  milima pia.