Jamvi La Siasa

Kenya humuenzi Tom Mboya kwa mengi aliyofanyia taifa

Na KWA HISANI YA KENYA YEAR BOOK September 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 4

Thomas Joseph Mboya atakumbukwa kama mmoja wa mawaziri waliovutia sana waliowahi kuhudumu nchini Kenya.

Wakati wa uhuru mwaka 1963, aliteuliwa kuwa Waziri wa Sheria na Masuala ya Katiba. Mnamo 1965, alihamishiwa Wizara ya Mipango ya Kiuchumi.TJ, kama alivyokuwa akijulikana, alizaliwa Agosti 15, 1930, akiwa mtoto wa kwanza wa Leonard Ndiege na Marcela Awuor kutoka Kisiwa cha Rusinga katika Mkoa wa Nyanza.

Wazazi wake walithamini elimu, na ingawa walikuwa wafanyakazi katika shamba la mikonge Kilimambogo, karibu na Thika, walihakikisha mtoto wao anapata elimu katika shule za misheni ya Kikatoliki.Mboya alianza shule akiwa na miaka tisa.

Baba yake alimtuma katika shule ya msingi ya misheni huko Machakos ambapo alisoma kwa miaka mitatu. Mnamo 1942, alijiunga na Shule ya Misheni ya St Mary’s, Yala, Nyanza. Hapo ndipo alianza kujifunza Kiingereza na historia. Kauli mbiu “Hakuna ushuru bila uwakilishi” ilimvutia akiwa mdogo.

Alifaulu mtihani mwaka 1945, na mwaka uliofuata akajiunga na Chuo cha Holy Ghost (Mangu), mojawapo ya shule bora za Kikatoliki katika Mkoa wa Kati. Mboya alikuwa mmoja wa wanafunzi bora wa mijadala na uigizaji.

Alivutiwa sana na hotuba za viongozi wa Magharibi, na aliwaenzi sana Napoleon Bonaparte, Abraham Lincoln na kiongozi wa haki za Wamarekani Weusi, Booker T. Washington.

Alisoma tena na tena hotuba za vita za Waziri Mkuu Winston Churchill. Kwa bahati mbaya, hakumaliza masomo kwa sababu ya ukosefu wa fedha, na hivyo hakuweza kufanya mtihani wa kitaifa wa kujiunga na chuo kikuu. Hata hivyo, hali hiyo haikumvunja moyo.Mwaka 1948, alijiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ukaguzi wa Usafi cha Royal Sanitary Institute na kufuzu mwaka 1950.

Alifanya kazi katika Halmashauri ya Jiji la Nairobi kwa miaka miwili na nusu. Alijiuzulu ili kuwa Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi wa Serikali ya Kenya, ambao yeye mwenyewe aliuanzisha.Baadaye alijiunga na Chama cha Watumishi wa Serikali za Mitaa za Kiafrika Nairobi, na ndani ya mwaka mmoja alichaguliwa kuwa Makamu wa Rais.

Mnamo Novemba 1953, aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Kenya (KFL), akihudumu hadi 1962 alipojiuzulu kujiunga na baraza la mawaziri kama Waziri wa Kazi.

Katika miaka ya 1950, Mboya aliamua kuanza kazi yake ya uanaharakati kupitia vyama vya wafanyakazi. Mnamo 1952, alianzisha Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa za Kenya, wakati serikali ya kikoloni ilikuwa imetangaza hali ya hatari na kuwakamata viongozi na wafuasi wa Mau Mau kama vile Kenyatta na Achieng’ Oneko.

Umaarufu wake ulienea kitaifa na kimataifa kupitia nafasi yake katika harakati za vyama vya wafanyakazi wakati wa hali ya hatari – moja ya vipindi vya giza zaidi katika historia ya Kenya.

Baadaye aliteuliwa kuwa mwakilishi wa Kenya katika Shirikisho la Kimataifa la Vyama Huru vya Wafanyakazi (ICFTU), nafasi aliyoitumia kukuza taaluma yake.Uamuzi wake wa kwanza wa kisiasa ulitokana na hali ya hatari.

Inasemekana alitembea hadi ofisi za chama cha Kenya African Union (KAU) na kujiunga nacho. Aliteuliwa kuwa mweka hazina na akaongoza upinzani wa wazalendo dhidi ya utawala wa Uingereza.

Kupitia uhusiano wake wa kimataifa, hasa na Chama cha Labour cha Uingereza, Mboya aliunganisha vyama vitano vya wafanyakazi chini ya KFL baada ya KAU kupigwa marufuku, na kufanya KFL kuwa taasisi kubwa ya wenyeji nchini.

Alijipatia sifa kubwa kutokana na ujasiri wake katika kupinga hatua za ukandamizaji wa serikali ya kikoloni kama vile uhamishaji wa raia, kambi za mateso na kesi za siri. Mnamo 1955, Chama cha Labour kilimteua kwa ufadhili wa mwaka mmoja kusomea usimamizi wa viwanda katika Chuo cha Ruskin, Oxford. Aliporudi Kenya 1956, Mau Mau walikuwa wamewika, na wengi waliuawa au kufungwa.

Yeye pamoja na wengine waliunda chama cha People’s Convention Party (PCP) mwaka 1957.Akitumia PCP, alichaguliwa kuwa mjumbe wa Legco (baraza la kutunga sheria), akiwa miongoni mwa Waafrika wanane pekee.

Wao walipigania uwakilishi sawa na kufanikisha kuongeza idadi ya Wafrika kutoka wanane hadi 14, sawa na Wazungu, ingawa Wafrika walikuwa zaidi ya milioni sita na Wazungu walikuwa 60,000 pekee.

Alianza uhusiano wa karibu na Kwame Nkrumah wa Ghana. Mwaka 1958, katika Mkutano wa Watu wa Afrika uliofanyika Accra, alichaguliwa kuwa mwenyekiti akiwa na umri wa miaka 28. Alisema baadaye: “Hiyo ilikuwa siku ya kujivunia zaidi maishani mwangu.”Alijulikana kwa utulivu, ujasiri na uwezo mkubwa wa kuhutubia umma.

Umaarufu huu ulimwezesha kushinda kiti cha Nairobi Central (Kamukunji) mara kadhaa. Mwaka 1959, alifanya ziara ya mihadhara Amerika na kutunukiwa shahada ya heshima ya sheria na Chuo Kikuu cha Howard.Alianzisha mpango mkubwa wa elimu – Airlift Africa Project – kupitia taasisi ya African-American Students Foundation.

Mnamo 1959, wanafunzi 81 wa Kenya walielekea Amerika kusoma. Baba yake Rais Barack Obama, Barack Obama Snr, alikuwa mmoja wao.Mwaka 1960, alimuomba msaada Seneta John F. Kennedy, na taasisi ya Kennedy ilifadhili kundi la pili la wanafunzi. Mpango huo ulipanuliwa hadi Uganda, Tanganyika, Zanzibar, Zambia, Zimbabwe na Malawi.

Wanafunzi 230 walifaidika 1960 na mamia zaidi kati ya 1961 na 1963.Januari 1961, Mboya alisafiri hadi India na kukutana na Waziri Mkuu Jawaharlal Nehru, ambaye alishawishi serikali ya kikoloni kumuachilia Kenyatta.Mnamo Agosti 21, 1961, Kenyatta aliachiliwa huru.

Mboya aliendelea kushiriki mazungumzo ya kuunganisha Kanu na Kadu. Mwaka 1963, Kenya ilipata mamlaka kamili ya ndani, na Kenyatta akawa Waziri Mkuu. Mboya alichaguliwa tena kama Mbunge wa Nairobi Central na kuteuliwa Waziri wa Sheria na Katiba.

Alisimamia maandalizi ya sherehe za uhuru zilizofanyika Desemba 12, 1963, kwa bajeti ya pauni 500,000.Mwaka 1964, Kenya ikiwa Jamhuri, Mboya aliteuliwa Waziri wa Mipango ya Kiuchumi na Maendeleo. Aliongoza kuundwa kwa COTU na kuandika Sessional Paper No.10 kuhusu Ujamaa wa Kiafrika na mpango wa kwanza wa maendeleo baada ya uhuru.Mboya alikuwa waziri wa kwanza wa serikali huru kuandika kitabu – Freedom and After – kilichochapishwa Oktoba 1963.

Mnamo Julai 5, 1969, akiwa Waziri wa Mipango ya Kiuchumi, Mboya aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa na umri wa miaka 38. Taifa lilishtushwa na kifo chake na maandamano yalizuka kote nchini.