• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 11:46 AM
Kiini cha hasira za Ruto kwa majaji

Kiini cha hasira za Ruto kwa majaji

NA LABAAN SHABAAN

PINDI aliponyanyua upanga wa mamlaka na kushika hatamu za uongozi wa taifa mnamo Septemba 13, 2022, Rais William Ruto alianza kazi kwa nguvu akidhihirisha atainua Idara ya Mahakama na kuiheshimu.

Saa moja tu baada ya kuapishwa, aliidhinisha uteuzi wa majaji 6 ambao Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta alikuwa amekataa kata kata kuwaajiri.

Majaji wa Mahakama Kuu Joel Ngugi, George Odunga, Aggrey Muchelule na Weldon Korir, waliteuliwa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) kujiunga na Mahakama ya Rufaa.

Nao Judith Omange na Evans Makori walipendekezwa na JSC kujiunga na Mahakama ya Ardhi na Mazingira.

Mnamo Juni 5, 2021, Rais Uhuru Kenyatta alisimamia hafla ya kiapo cha majaji 34 baada ya kudinda kuidhinisha uteuzi wa majaji hao 6 waliofaa kupandishwa vyeo na JSC.

Rais mstaafu Uhuru Kenyatta alisema alichukua hatua hiyo kwa manufaa ya taifa bila kufafanua madai aliyotoa ya utovu wa maadili.

Wanasiasa na mawakili walioegemea mirengo pinzani wakati huo, waliungana kumkashifu Rais kwa kukosa kuidhinisha baadhi ya majaji walioteuliwa na JSC.

Walisema Bw Kenyatta ameweka mfano mbaya kwa marais watakaofuata kuwa wanaweza kuhitilafiana na uhuru wa Mahakama.

Hali hii imeanza kushuhudiwa kutoka kwa uhusiano ambao umeingia doa kati ya Rais Ruto na Idara ya Mahakama.

Inakisiwa Rais Kenyatta aliwatema majaji sita sababu Majaji George Odunga na Joel Ngugi walikuwa kwenye jopo lililoangusha mpango wa upatanishi wa BBI uliosukumwa na Bw Kenyatta na Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga.

Naye Rais William Ruto, aliyekosana na ‘ndugu hao wa handisheki,’ aliidhinisha uteuzi wao Septemba 14, 2023.

Kuonyesha kupiga jeki haki, Rais Ruto alitangaza kuzidisha bajeti ya Idara ya Mahakama kwa Sh3 bilioni kila mwaka katika muhula wake wa kwanza (2022 – 2027)

Alisema nia yake ni kuifanya Mahakama iwe thabiti na yenye kujitegemea kifedha ili ifaulu kutekeleza majukumu yake.

Na katika makadirio ya bajeti ya kwanza ya mwaka wa 2023/2024 ya Sh3.6 trilioni iliyosoma na Waziri wa Fedha Prof Njuguna Ndung’u mnamo Juni 15, 2023,  Rais alitimiza ahadi akaongeza kibaba cha Mahakama kwa Sh4.1 bilioni na kufika Sh22.9 bilioni kutoka Sh18.8 bilioni za mwaka wa 2022/2023.

Mnamo November 4, 2022 katika hafla ya kuzindua Ripoti ya Kila Mwaka ya Hali ya Mahakama na Utekelezaji wa Haki iliyofanyika katika Mahakama ya Upeo jijini Nairobi, Kiongozi wa Taifa alisema atadumisha utawala wa sheria.

“Ninasisitiza ahadi yangu kwa Wakenya kuwa nina nia ya kustawisha idara ya mahakama kwa mujibu wa katiba na kuheshimu maamuzi na amri za korti,” alisema Rais akimiminia sifa asasi za sheria.

Matamko ya Rais yaliyojaa sifa kedekede kwa Mahakama yalianza kusawiriwa kuwa ameiteka idara ya korti.

Lakini, sasa mambo yameenda kombo na mgogoro mkali unatokota kati ya matawi haya mawili ya serikali.

Kiongozi wa Nchi analaumu baadhi ya majaji akisema ni wafisadi na wanapokea rushwa ili kuvuruga miradi ya maendeleo ya serikali yake anayoamini italeta mageuzi ya kiuchumi.

“Haiwezekani mipango ambayo imeidhinishwa na bunge na Wakenya waliopigia kura manifesto yangu ipingwe na watu wawili/watatu wakihongana kortini kusimamisha miradi ya ushuru wa nyumba, ujenzi wa barabara na afya kwa wote,” alisema Rais akidai kuwa bado anaheshimu uhuru wa Mahakama alipozungumza mnamo Januari 2, 2024 katika mazishi ya baba yake Seneta wa Nyandarua Methu Muhia.

Itakumbukwa kwamba Rais alifoka siku mbili kabla ya Makahakama ya Rufaa kusikiliza ombi la Mwanasheria Mkuu Justin Muturi kuamua iwapo serikali itaendelea kutoza wananchi ushuru wa makazi Januari 4, 2024 au la.

Majaji Lydia Achode, John Mativo na Mwaniki Gachoka waliruhusu serikali iendelee kukata wafanyakazi kodi ya ujenzi wa nyumba hadi uamuzi utakapotolewa Januari 26, 2024.

Rufaa hii ilijiri baada ya Mahakama Kuu kuzima ushuru huo mnamo Desemba 28, 2023 kwa msingi kuwa ulikuwa baguzi na kuahirisha utekelezaji wake hadi Januari 10, 2024.

Seneta wa Busia Okiya Omtatah ambaye aliwasilisha kesi dhidi ya makato ya nyumba, sasa analilia vyombo vya usalama akidai maisha yake yako hatarini.

Mpango mwingine wa serikali uliopigwa breki na mahakama ni ule wa ubinafsishaji wa mashirika 11 ya umma baada ya kesi kuwasilishwa na Chama cha Orange Democratic Movement (ODM).

Baadhi ya mashirika ambayo serikali imepanga kuuza ni Jumba la Mikutano ya Kimataifa (KICC), Kampuni ya kuhifadhi na kusafirisha bidhaa za petroli nchini Kenya Pipeline Company (KPC) na kiwanda cha nguo cha Rivatex East Africa Limited (REAL).

Serikali ya Kenya Kwanza inaamini ubinafsishaji kampuni hizi, utaleta faida nyingi na kusaidia kustawisha uchumi wa nchi uliodumaa.

Mahakama Kuu ilitakabali ombi la ODM ambapo Jaji Chacha Mwita alizuia utekelezaji wa sheria ya ubinafsishaji hadi uamuzi utolewe Februari 6, 2024.

Mahakama ilisema suala hilo limeibua masuala muhimu ya kuzingatiwa kikatiba huku ODM ikitaka Wakenya wapigie kura mabadiliko haya.

Mpango mwingine ambao umekutana na matuta barabarani ni ule wa Bima ya Afya ya Jamii (SHIF).

Matukio haya yamempandisha mori Kiongozi wa Taifa aliyeanza kazi kwa moto.

Moto huu umepozwa na pingamizi za upande wa Upinzani na maamuzi ya Idara ya Haki.

Utawala changa wa Rais Ruto umekumbana na vizingiti tangu alipotangazwa Rais Mteule.

Kiongozi wa Upinzani alienda Mahakama ya Upeo kupinga ushindi wake lakini korti ikatupilia mbali rufaa yake kwa kukosa mashiko mnamo Septemba 5, 2022.

Baada ya Rais kuwaka moto na kutema cheche kali kwa mahakama, Jaji Mkuu pia akarusha miale mikali kwa tawi tendaji (executive) la serikali akisema wote wana nguvu sawa na mahakama haiwezi kufanya kazi kwa neema ya Rais na Baraza la Mawaziri.

“Tume ingependa kusisitiza kuhusu uhuru wa Mahakama kama mojawapo ya nguzo kuu za serikali ilivyonakiliwa kwenye Katiba na inawapa shime majaji na maafisa wake wote kuendelea kutekeleza majukumu yao bila woga wala mapendeleo,” alisema Jaji Mkuu baada ya mahakama kushutumiwa.

Kadhalika, Bi Koome alimtaka Rais kuwasilisha ushahidi kwa JSC iwapo ana ushahidi kuhusu majaji fisadi.

Yamkini uhakika wa madai ya Rais dhidi ya Mahakama unaweza kupigwa muhuri kwa tukio la kutimuliwa kwa aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu Said Chitembwe.

Mahakama ya Upeo ilitupilia mbali rufaa yake baada ya Mahakama Kuu kupendekeza kutimuliwa kwa Bw Chitembwe kwa kushiriki rushwa wakati wa uamuzi wa kesi mbalimbali.

Iwapo Rais atawasilisha ushahidi dhidi ya majaji, ni tukio la kusubiriwa tu.

Makabiliano kati ya Rais na Idara ya Haki yanatarajiwa kuendelea kushika kasi ndani ya hatamu yake ya uongozi katika muhula wa kwanza.

Kama moto huu utapoa na matawi haya mawili kufanya kazi kwa manufaa ya taifa, ni muda tu utabaini kutegua kitendawili hiki.

  • Tags

You can share this post!

Sachang’wan mpya? Eneo la ajali barabara ya...

CDF isipodunda kwa akaunti zetu katika saa 48 patachimbika,...

T L