Kilichofanya Raila na Ruto kuparamia kumuokoa Sakaja
JUHUDI za pamoja za Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga zilizomwokoa Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja dhidi ya kutimuliwa zimeanika mikakati ya kisiasa ya hali ya juu inayoendelea jijini Nairobi kuelekea uchaguzi wa 2027.
Hofu ya kufanyika kwa kampeni za uchaguzi mdogo endapo Gavana Sakaja na Naibu wake James Muchiri wangetimuliwa, pamoja na juhudi za kuonyesha mamlaka katika siasa za jiji na kuzima tishio lolote kwa serikali jumuishi, zilikuwa kiini cha msukumo mkubwa wa viongozi hao wawili kuhakikisha hoja ya kumtimua Sakaja inazimwa.
Pia kulikuwa na hofu kuwa jiji lingeingia katika mgogoro wa uongozi kama ulivyoshuhudiwa mwaka 2020 baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Naibu Gavana Polycarp Igathe na kutimuliwa kwa aliyekuwa Gavana Mike Sonko. Bw Sonko alitimuliwa na nafasi yake kuchukuliwa mwaka 2021 na Bi Ann Kananu, aliyesaidiwa kuendesha jiji na Huduma ya Jiji la Nairobi (NMS).
Kutimuliwa kwa Bw Sakaja na Bw Muchiri kungekuwa faida kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, kwani ingekuwa nafasi yake kupimana nguvu kisiasa na Rais Ruto na kuonyesha ushawishi wake kisiasa jijini Nairobi kuelekea uchaguzi wa 2027.
Kwa kuwa Nairobi ni mji mkuu wa nchi na wa makabila mbalimbali, uchaguzi mdogo kama huo ungekuwa kiashiria cha mwelekeo mpya wa miungano ya kisiasa, hali ambayo ingeathiri mkakati wa kisiasa wa serikali jumuishi.
Zaidi ya hayo, kwa kuwa Sakaja ni gavana aliyechaguliwa kwa tiketi ya UDA, kutimuliwa kwake kungekuwa pigo kubwa kwa Rais Ruto na chama tawala, ikizingatiwa nafasi ya kimkakati ya kaunti hii kama makao ya mamlaka kuu.
“Mwelekeo wa kisiasa huwa ni mawimbi. Endapo Sakaja atatimuliwa, hii itakuwa mfano mbaya. Ruto/Raila hawakupaswa kufeli katika kumwokoa Sakaja kwa sababu upinzani ungeweza kupata viti. Kwa hivyo, siasa za Nairobi zina athari kubwa kitaifa. Kumuokoa Sakaja ilikuwa lazima kwa Ruto na Raila,” asema Profesa David Monda, mhadhiri wa chuo kikuu nchini Amerika na mchambuzi wa siasa.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 182(4) cha Katiba, Spika wa Bunge la Kaunti huchukua nafasi kama kaimu gavana kwa muda wa siku 60 endapo gavana na naibu wake watatimuliwa. Ndani ya siku hizo, uchaguzi mdogo lazima ufanyike kumpata gavana na naibu mpya.
Uamuzi wa Madiwani wa Kaunti ya Nairobi kupendekeza kuondolewa kwa gavana na naibu wake pia umeonyesha mgawanyiko wa kisiasa kati ya kambi mbalimbali katika bunge la kaunti
Kwa kawaida, madiwani huwinda tu gavana, na naibu hunufaika moja kwa moja. Lakini kwa kutaka kuwaondoa wote wawili, bunge lenye madiwani wengi kutoka ODM linaonekana kutokuwa na imani na msimamo wa kisiasa wa Bw Muchiri.
Wachambuzi wanasema uamuzi wa Rais Ruto na Bw Odinga kumwokoa Sakaja ni sehemu ya mkakati wa kulinda mshikamano kati ya UDA na ODM, pamoja na kuimarisha ushawishi wao wa pamoja jijini Nairobi.
Baadhi ya wafuasi wa serikali jumuishi wamedai kuwa hoja ya kumtimua Sakaja ilikuwa njama ya wapinzani wao kuvuruga mkataba wa ushirikiano kati ya Dkt Ruto na Bw Odinga.
“Kuna watu ndani ya ODM na UDA ambao hawajakubali serikali jumuishi na wamekuwa wakitafuta migogoro kati ya vyama hivyo viwili. Wengine wanatumika na mahasimu wa nje wanaotaka kushawishi siasa za Nairobi,” alisema Mbunge wa Makadara George Aladwa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa ODM tawi la Nairobi.
Mbunge wa Kibra Peter Orero, mshirika wa karibu wa Bw Odinga, alisema hoja ya kumtimua gavana inaendeshwa na maslahi binafsi na tamaa ya kulipiza kisasi cha kisiasa.
Bw Orero alisema kuwa madiwani wanapaswa kudai huduma bora badala ya kutumia hoja ya kumtimua ambayo inaweza kuvuruga shughuli jijini.
“Lingekuwa janga kwa Nairobi. Jiji la Nairobi halijawahi kuwa na utulivu wa kisiasa unaohitajika kwa maendeleo ya maana. Wakati wa Sonko, huduma zilikwama kutokana na vurugu za kisiasa,” alisema Bw Orero.
“Wanaokasirishwa na uongozi wa sasa wasubiri uchaguzi ujao badala ya kuvuruga huduma kupitia hoja ya kumtimua,” aliongeza.
Kwa kuhakikisha Sakaja anasalia afisini, Dkt Ruto na Bw Odinga pia wanatafuta utulivu wa kisiasa jijini huku wakijiandaa kuhifadhi ushawishi wao kwenye uchaguzi ujao.
Mbunge wa Embakasi Central Benjamin Gathiru, mshirika wa Bw Gachagua, alisema kuwa ni ajabu kwa Ruto na Odinga kutumia muda mwingi kumlinda Sakaja bila kusikiliza malalamishi ya wakazi wa Nairobi.
Bw Gathiru alisema hakuna njia ambayo gavana na naibu wake wangetimuliwa kwa pamoja, kwani lawama kubwa inapaswa kumwangukia gavana.
Aliongeza kuwa juhudi za pamoja za viongozi hao wawili zinaonyesha wanahofia kupoteza ushawishi wao kisiasa jijini Nairobi.
“Hata wakimlinda sasa, bado atakutana na wananchi mwaka wa 2027. Ikiwa ningekuwa wao, ningemwacha abebe msalaba wake kwa makosa aliyowatendea wakazi wa Nairobi,” alisema mbunge huyo.
Prof Monda aliongeza kuwa Bw Odinga na Rais Ruto wamewekeza kwenye serikali jumuishi na hawangekubali hoja kama hiyo kutikisa mshikamano wao.
“Aliyekuwa Naibu Rais (Gachagua) aliwahi kupinga Sakaja kwa madai ya kubana biashara ya watu wa kutoka Mlima Kenya kati kati ya jiji na kudhibiti matatu. Hoja yoyote ya kisiasa kama ya kumtimua Sakaja ambayo inaweza kumfaidi Gachagua itaangaliwa kwa tahadhari si tu na Ruto, bali pia na Raila,” akaongeza Prof Monda.
Akiwa amechaguliwa kwa tiketi ya UDA iliyo na madiwani 52 pekee katika bunge lenye wanachama 125, Bw Sakaja amekuwa akitegemea ushirikiano na ODM iliyo na madiwani wengi ili kutekeleza ajenda yake, ikiwemo kupitisha bajeti.
Hata hivyo, uamuzi wake wa kushirikiana na ODM ya Bw Odinga pia umeibua ukosoaji, hasa kutoka kwa Bw Gachagua.