Kilichomchongea Gavana Nyaribo madiwani Nyamira wakimtimua kwa mara ya tatu
HATIMA ya Gavana Amos Kimwoni Nyaribo sasa imo mikononi mwa Bunge la Seneti baada ya kuondolewa madarakani na Bunge la Kaunti ya Nyamira jana kwa mara ya tatu.
Spika Thaddeus Nyabaro aliongoza kikao ambapo madiwani 23 wa Bunge la Kaunti ya Nyamira walipiga kura kumuondoa madarakani gavana huyo.
“Jumla ya madiwani 23 wamepiga kura ya kutokuwa na imani na uongozi wake. Sheria inahitaji idadi hiyo kuwa thuluthi mbili na imetimizwa,” akasema Bw Nyabaro.
Spika huyo alisema madiwani wanne ambao hawakuwa bungeni waliomba wawakilishwe na madiwani wenzao na wakawapigia kura.
Ni madiwani 19 walikuwa bungeni wakati huo.
Bw Nyaribo alikuwa amenusurika mara mbili kung’atuliwa huku hoja ya pili ya kumbandua ikiwasilishwa mnamo Septemba 2024.
Hoja hiyo ya pili ilifeli baada ya kuungwa mkono na madiwani 22 huku sheria ikisema madiwani 23 walihitajika. Iliwasilishwa na Diwani Evans Matunda.
Baada ya kungátuliwa kwa Bw Nyaribo, spika alisema kuwa afisi yake itamuarifu Spika wa Seneti Amason Kingi kuhusu hatua hiyo.
Katika kikao cha jana, madiwani walipiga kura kwa njia ya siri kutokana na ombi la Kiongozi wa Wengi George Abuga. Gavana naye aliwakilishwa bungeni na mawakili wake Ombui Ratemo na Zelmer Bonuke.
Wakimtetea Bw Nyaribo, mawakili hao walisema madiwani hao walikuwa wamekosa ushahidi na pia walipuuza amri ya korti.
Diwani wa Bonyamatuta Julius Kimwomi Matwere aliwasilisha hoja ya kumbandua gavana madarakani kwa ukiukaji wa katiba na sheria nyingine pamoja na kutumia afisi yake vibaya.
Hoja hiyo iliungwa mkono na Diwani Maalum Evans Juma Matunda. Kwenye hoja yake, Bw Matwere alidai gavana amekiuka katiba kimakusudi.
Mashtaka makuu dhidi ya Bw Nyaribo ni kwamba alikiuka katiba na sheria za serikali ya kaunti kwa kuegemea mrengo wa spika wa zamani Enock Okero na kundi lake la madiwani wakati wa jaribio la kwanza la kumtimua.
Bw Okero aliondolewa na madiwani ambao wanamuunga mkono spika wa sasa. Mrengo wa spika huyo wa zamani ulikuwa ukiandaa vikao vya Bunge Mashinani maeneo mbalimbali ya kaunti hiyo huku wakihepa majengo ya bunge la kaunti.
Bw Nyaribo alinukuliwa mara si moja akiunga mkono mrengo wa Bw Okero. Hoja ilisema gavana alifanya hivyo ilhali alijua kwamba Bw Okero alikuwa ameondolewa madarakani.
Uamuzi wa Mahakama Kuu mnamo Juni 2025 ulithibitisha kuwa Bw Okero alipoteza wadhifa wake kama spika mnamo Oktoba 2024 na vikao alivyokuwa akiongoza vilikuwa kinyume cha sheria.
Seneti pia ilikuwa imeharamisha maamuzi yote yaliyotangazwa na mrengo wa Bw Okero. Uamuzi wa korti ulimchongea Bw Nyaribo kisiasa kwa sababu madiwani mahasimu sasa walikuwa na nafasi ya kumwandama.
“Uongozi wa Nyaribo ukiendelea, utahatarisha hali ya baadaye ya kaunti hii na unakiuka nguzo za utendakazi katika utumishi wa umma,” akasema Bw Matwere.
Pia, gavana huyo alijipalilia makaa kwa kumteua Peris Oroko kama Waziri wa Utumishi wa Umma kwenye kaunti bila kuidhinishwa na bunge la kaunti.
Bi Oroko aliidhinishwa na mrengo wa madiwani wanaoegemea Bw Nyaribo waliokuwa wakiandaa vikao vya bunge la mashinani.
Hatua hii, hoja iliyowasilishwa jana inasema ilikuwa ukiukaji mkubwa wa sheria na matumizi mabaya ya mamlaka.
Gavana pia alishutumiwa kwa kukosa kuwasilisha stakabadhi za kila mwaka za fedha na pia kukosa kuhutubia bunge miaka ya kifedha ya 2023/24 na 2024/25.
Hoja iliyowasilishwa inasema hatua hiyo inakiuka hitaji la uwazi na uwajibikaji.
Isitoshe, hoja ya kumtimua gavana ilisema kuwa alikiuka amri ya Mahakama ya Uajiri na Leba ya Kisumu na kumteua Clive Ogwora kama waziri wa kaunti.
Hatua hiyo iligharimu kaunti kwa sababu ilipoteza Sh4.4 milioni na ukiongeza riba, ilipanda hadi Sh6.9 milioni.
Pia anashutumiwa kwa kuwaajiri wafanyakazi bila bajeti iliyoidhinishwa akiwemo maafisa 49 kati ya Februari na Aprili 2021.
Kati ya maafisa hao ni Naibu Katibu wa Kaunti, Mwanasheria wa Kaunti, wafanyakazi wadogo na wale wa kusimamia wadi na kaunti ndogo.
Madai mengine ni kuwaajiri Geodfrey Kiraiago na Elmeda Nyaberi katika idara ya uajiri kwa njia ya mapendeleo.
Pia Bw Nyaribo hakuponyoka kutokana na madai ya kupokea Sh5.6 milioni kama mshahara na ulipaji haramu wa mishahara kwa kima cha Sh32 milioni pamoja na teuzi nyingine zisizofuata sheria.
“Huu ni usaliti kwenye uaminifu ambao umma ulizingatia kabla ya kumchagua na adhabu kali zaidi ni kuondoka kwake afisini,” akasema Bw Matwere.