Jamvi La Siasa

Kilichomfanya Jimmy Kibaki kujiuzulu The New Democrats

June 2nd, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

WIKI mbili baada ya Jimmy Kibaki, mwanawe Rais wa Tatu wa Kenya, Hayati Mwai Kibaki, kujiuzulu wadhifa wa Naibu Kiongozi wa chama cha The New Democrats (TND) imefichuka kuwa alifanya hivyo ili kutomkwaza Rais William Ruto.

Katibu Mkuu wa chama hicho David Musembi juzi alitoboa kwamba Jimmy alijiondoa kufuatia mpango wa washirika wa Naibu Rais Rigathi Gachagua kutaka ushirikiano na chama hicho.

“Washirika wake (Gachagua) walikuja kwetu wakitaka tuanzishe mazungumzo kwa lengo la kubuni ushirikiano. Jimmy Kibaki alipofikiwa na habari hizo, alivunjika moyo na kutujuza kwamba anajiuzulu na kujiondoa siasani,” Bw Musembi akanukuliwa akisema.

“Jimmy hakutaka kuhusishwa katika migongano na mivutano ya kisiasa kati ya Rais Ruto na naibu wake. Hii ni licha ya kwamba maafisa wa chama chetu walikutana na ‘wajumbe’ wa Gachagua bila idhini kutoka kwa Baraza Kuu la Kitaifa (NEC)” akaongeza.

Bw Musembi alidai kuwa mkutano huo ulifanyika katika kaunti ya Kiambu.

Hata hivyo, kauli yake ilionekana kutofautiana na ile ya kiongozi wa TND Thuo Mathenge aliyesema hivi: “Sina habari kwamba Naibu Rais Rigathi Gachagua anapanga kutwaa chama chetu. Hata hivyo, tunawakaribisha wote ambao wanataka kujiunga nasi, akiwemo yeye Gachagua, kwa sababu kufikia sasa TND ndicho chama asili katika Mlima Kenya na chenye ushawishi mkubwa zaidi”.

Aidha, Bw Gachagua mwenyekiti amekana ripoti kwamba anasaka chama kipya kufuatia dharuba zinazomgonga katika chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Kumeibuka mpasuko ndani ya chama hicho tawala kati ya wanasiasa washirika wa Rais Ruto kwa upande mmoja na wale ambao ni wandani wa Bw Gachagua, wakizozania usemi na mipango ya kisiasa kuelekea chaguzi za 2027 na 2032.

“Habari hizo sio sahihi na zinasheheni porojo na nia mbaya,” akasema Bi Njeri Rugene, ambaye ni Mkuu wa Kutengo cha Habari katika Afisi ya Naibu Rais.

Mnamo Mei 16, 2024, Jimmy alisema kuwa aliamua kujiondoa kama Naibu Kiongozi wa chama cha TND kutokana na nia ya kutaka kuelekeza nguvu na muda wake katika usimamizi wa biashara zake na shughuli nyingine za kilimo.

“Kwa miaka 33 iliyopita, nimejihusisha katika shughuli mbalimbali za kisiasa katika nchi hii, ikiwemo uundaji na usimamizi wa vyama kadhaa vya kisiasa. Mnamo 1991 nilishiriki katika kuundwa kwa chama cha Democratic Party of Kenya (DP). Aidha, nilijihusisha na muungano wa NARC ambao ulitwaa mamlaka ya kuongoza nchini mnamo 2002. Aidha, nilishiriki katika uundwaji na usimamizi wa chama cha PNU,” akasema.

“Kwa hivyo, baada ya kutafakari kwa kina na kujisaili, nimeamua kujiuzulu wadhifa wa Naibu Kiongozi wa chama cha The New Democrats. Huu sio uamuzi rahisi, lakini imebidi kwani utaniwezesha kupata muda wa kuendesha na kusimamia biashara zangu,” Jimmy akaeleza kwenye taarifa hiyo aliyoituma kwa vyombo vya habari.

Tofauti na watoto wa marais wa zamani Jomo Kenyatta na Daniel Moi, watoto wa Mwai Kibaki walijitenga na siasa. Ni Jimmy pekee aliyejaribu lakini hakuwania kiti chochote cha kisiasa nyumba kwao Nyeri au Nairobi ilivyotarajiwa.