Jamvi La Siasa

KINAYA: Ajabu ya Wakenya kuchukia wenzao walio ughaibuni ila pia wanataka kwenda majuu

Na DOUGLAS MUTUA May 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MKENYA ni kama maini, hatulii kiganjani. Leo anatukana wenzake wanaoishi ughaibuni, kesho analia kwamba amenyimwa fursa ya kwenda kuishi na kufanya kazi ughaibuni.

Leo ataitukana Amerika, aseme si mbinguni, lakini kesho ataingia mtandaoni kimya-kimya na kujaribu bahati yake katika ule mchezo wa bahati nasibu, almaarufu Green Card, wa kupeleka watu Amerika.

Unaposoma makala hii, kuna watu wanaofurahi kwani matokeo ya kamari hiyo ya Green Card yalitangazwa jana, baadhi wakabahatika, wengine wakaambulia patupu.

Waliotoka bila wamenuna, hata labda wanasema huo ni mchezo wa mjini tu, watu walichanguliwa kitambo.

Bure tu tunachafulia sifa kitu tulichotafuta tukakosa. Ni sawa na ng’ombe au punda kuchafua na kukojolea maji wenzake wasinywe.

Waliobahatika watakwambia wanatafuta kila mbinu ya kuondoka, Kenya hakuwakai tena. Hawangesema hivyo kama wangekosa bahati hiyo.

Usiwachukulie uzito, maringo ni hulka ya Mkenya. Atasimama kando ya gari la watu, apige picha na kukuwekea mtandaoni ili uamini maisha yanamwendea mnyooko, lakini wapi! Amelalia mate jana.

Ikiwa ulibahatika, tunza siri hiyo. Hujakamilisha mchakato mzima mpaka uingie Amerika. Kuna kuomba kibali cha kusafiria, viza, ambacho huna hakika utapata.

Watu hunyimwa hata baada ya kufaulu katika mchezo huo, wakaishia kurejea kwao mashambani kulima viazi na maharagwe.

Hata ukiingia Amerika, bado usipige picha za kuringia wenzako ulioacha Kenya kwa kuwa tunajua maisha hayakunyookei ghafla.

Wajanja wa mjini wanadanganya kwamba ukipata Green Card na kuingia Amerika unakuta ukisubiriwa na jumba la kifahari, gari kubwa na kazi nzuri. Nacheka!

Ndugu yangu, ikiwa hutaki kupata msongo wa mawazo, usiamini hekaya hizi. Marekani nguvu ya mtu huliwa! Unaweza kutoka Kenya ukiwa mwanasheria, ukifika kule ukaendesha teksi au hata kuwaoshea watu magari.

Kazi zipo za kila aina, ikiwa ni pamoja na kuyatembeza majibwa ya watu, na yakinya unaokota kinyesi hicho kwa sandarusi! Lazima tusafishe mazingira.

Paka pia hutunzwa kama watoto, hasa wenyewe wakiwa shughulini. Nyasi pia hufyekwa. Na kusugua bafu na vyoo.

Ukitaka kuvuma kikweli, ikiwa ni lazima ujianike mtandaoni kama mjusi akiota jua, basi piga picha na paka na majibwa hayo, uandike hapo kwamba wewe ni yaya wa wanyama. Huo ndio uhalisia wa maisha.

Ukifanya hivyo, utakuwa maarufu na bado utalipwa, tena vizuri. Si kama Kenya ambako unakuwa maarufu huku ukipiga miayo ya njaa.

Amerika hakuna ahadi za uongo kama zinazotolewa na somo wangu wa Maendeleo Chap-Chap. Tafuta ajira, ila jihadhari na matapeli kwa kuwa wamejaa ndani na nje ya serikali ya Kenya.

[email protected]