KINAYA: Anayehonga wabunge ajue kina cha ufisadi urefu wake haujulikani
NASIKIA nyama ya binadamu ni tamu sana, anayeionja ataendelea kuitamani.
Usishtuke, sijawahi na sitawahi kuionja kamwe, ningali mpenzi wa nyama ya kuku, ng’ombe, mbuzi na kondoo.
Pia naambiwa pesa ni tamu zaidi, aliyezizoea kwa wingi akizikosa huingiwa na pepo mchafu kama kahaba, uroho ukamlemea, akazitafuta kokote na kwa vyovyote.
Aliyesema kuhusu nyama ya binadamu ni Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mwanzilishi wa taifa la Tanzania, akieleza kwamba tabia aliyoizoea mtu hugeuka uraibu, ni vigumu kuiacha.
Ikiwa mtu amewahi kuwa na ushirika na wabunge, akawahonga kwa mamilioni ili wamfanyie kazi fulani, kama vile kumfurusha msaidizi wake msumbufu, basi ni lazima aendelee kuwapa pesa mpaka mwisho wa utawala wake.
Kisa na maana? Wamezoea pesa, na kwa kuwa kama umeme unaouzwa kwa vipimo pesa hazidumu milele, mifuko yao ikitoboka ana jukumu la kuishona na kutia kitu humo ili urafiki wao udumu.
Vinginevyo, atazuka mtu mwingine aliye na pesa awaonyeshe tu kisha wamfuate kokote aendako ili awagawie. Hilo ndilo tatizo la kuwazoesha watu, hasa wanasiasa, pesa.
Watazipokea kutoka kokote na kukusahau ghafla, ikibidi walipwe ili wakukumbushe huwi chochote wala lolote bila pesa, nawe utulize boli kwa kuwa unajua mmetoka mbali nao katika kamari hiyo.
Wafugaji wa mbwa watakwambia huwezi kuwalisha wanyama hao nyama isiyopikwa, kisha ukawaacha kutangamana na mifugo wako kwa raha zao.
Ukifanya hivyo, umewaruhusu mbwa kujichagulia aina ya chakula saa za mlo zikifika. Wakiamua mchana ni kuku na jioni ni mbuzi, basi inakuwa hivyo, nawe huwezi kulalamika kwa kuwa mali na mali haziumizani.
Unapowashawishi wanasiasa kufanya chochote, kama vile kutunga na kupitisha sheria kandamizi kwa kuwalisha unono kwa kisingizio cha kuwahamasisha, subiri wakati wako wa kuliwa, unakuja upesi.
Lipo shimo liingiamo pesa ambalo urefu wa kina chake haujawahi kujulikana. Halijai, kila unavyolipa linatamani zaidi.
Ushirika wowote uliojengwa kwa msingi wa hela utabomolewa kwa nguvu za hela.
Pesa, ambazo tangu hapo hujulikana kama mvunja mlima, hazijui uzalendo au urafiki wa aina yoyote ile. Hata mtaani unaambiwa uongee lugha ya pesa au ufyate domo ‘watu wazima wakiongea’.
Ngoja aje mwenye pesa, ambaye mara ya mwisho kupiga mswaki ni Krismasi mwaka jana. Hata akipanua domo kiasi gani na kuteuka uvundo, ataambiwa linanukia marashi freshi.
Mama aliyemficha fisi mtoro kwake ili watu wanaomkimbiza wasimnase hafai kuomboleza wanawe wakiliwa na hayawani huyo.
Njia ya pekee ya kujiliwaza ni kumsihi mumewe asiangike jembe kwani bado kazi ingalipo, arejee shambani kabla ya kiangazi kubisha hodi, aanze malezi upya.
mutua_muema@yahoo.com