KINAYA: Gen Z wanajua wewe ‘umefanikiwa’ kupitia wizi
SASA nimeelewa kwa nini kizazi kichanga cha Gen – Z kinaonekana kama kinapenda kuanzisha ugomvi na vizazi vingine vilivyokitangulia!
Akili za Gen – Z ziko mbele ya umri wao, wanatamani maisha mazuri, na kabisa hawaelewi kwa nini baadhi ya watu ambao wamefikisha umri wa miaka 40 wana ‘utoto’ mwingi hivi.
Mathalan, nimetokea kukinai tabia ya watu waliozaliwa miaka ya sabini na themanini kupakia picha zao kwenye mitandao ya kijamii, kutangaza umri wao na kuandika orodha ndefu ya watoto na wajukuu wao!
Watu wazima wanatoa nguvu za utoto huu wapi? Picha hizo zinasaidia nchi na nini wakati huu ambapo bado tunanusa harufu ya mabomu ya machozi yaliyorushwa na polisi wa Kasongo wakati wa maandamano ya Saba Saba?
Hebu ingia mtandaoni, uchukue mifano kadha, uhesabu na miaka ya watu wanaojianika huko, utoe na umri wa watoto wao, uone baadhi yao walishakuwa wazazi hata kabla ya kufikisha miaka 16!
Ikiwa bado unasisitiza kuwa watu wanapaswa kujipa raha wenyewe wanavyotaka bila kuingiliwa na mtu, niambie ni akili za kuku, ngiri au msongareli ambazo zinamsababisha mtu kusifia ukora wake wa utotoni.
Gen – Z wanajifunza nini kutokana na mazao ya tabia mbovu ya kuonja matunda mabichi, yakiwa bado mtini, ambayo vizazi vilivyowatangulia vinasifia?
Hivi, huko si kutumia akili kama kofia, pengine kutumia kamasi badala ya ubongo, au kufikiria kwa makalio kama nyigu chambilecho bibi mzaa mama?
Huku vijana wa jana wanapojianika mtandaoni na jamaa zao, Gen – Z wana dai moja pekee: Tuonyesheni mnakotoa pesa, nasi tuzipate, tuishi maisha mazuri pia!
Gen – Z wako radhi kufanya kazi, kula jasho lao hasa, mradi kazi yenyewe ni halali, haihusishi kuibia umma au kuvunja sheria za nchi na hatimaye kujitokeza mtandaoni na kudanganya watu ‘ni neema za Mungu tu’.
Unakufuru sana unapopora mali ya umma, kumwibia mwajiri wako au kushiriki ufisadi wowote kisha unakuja mtandaoni kuturingia ulivyofanikiwa, huku ukitaja jina la Mungu kana kwamba ni hirimu wako.
Ikiwa huamini Gen – Z wanatamani kufanya kazi halali ili watie riziki ya Mungu vinywani, waajiri au uwatafutie kazi, wakishindwa uwaanike mtandaoni na kuwaita wazembe.
Kuwadharau na kuwatukana eti wanatokea jijini huku kavalia champali na soksi chafu kabla hujawapa mtihani wa kazi wakafeli ni kuwachukia bure. Adui hana sababu eti. Usiwe adui uchwara!
Gen – Z wameerevuka kiasi kwamba wanajua ugumu uliopo nchini Kenya: Mtu hawezi kufanya kazi au biashara halali na kuunda milioni nzima kwa mwezi.
Na wanajua huwezi kuwaringia mtandaoni kwa mamilioni ya kukopa, kwa hivyo unapojishaua na kuwafanya kujihisi wamefeli kimaisha, haikosi wewe ni mwizi!
Uhasama kati ya Gen – Z na vizazi vingine utaisha watu wakizoea kufanya mambo wakizingatia sheria.
mutua_muema@yahoo.com