Jamvi La Siasa

KINAYA: Heri hili pendekezo la hospitali ya Gen Z kuliko siasa za kale

Na DOUGLAS MUTUA October 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

UMESIKIA pale Tiktok, Gen Z wanachanga pesa ili wajenge hospitali yao ambapo wagonjwa hawatalipia matibabu?

Mambo yanavyokwenda mbio Kenya, unaweza kulala, hata kabla ya kuota ndoto ya kwanza, usikie ukiamshwa eti hapo ulipo pamenunuliwa!

Wakenya hatulali, tunafikiria usiku na mchana. Wakati mwingine hatuaminiki, lakini historia ya Gen Z na fujo za kufanya mambo yanyooke inasababisha niangalie M-Pesa yangu ina kiasi gani ili niwarushie kitu.

Au unataka kuniambia hutamani kuona hospitali mpya, tena inayotibu watu bila malipo, ikishindana na nyingine kubwa nchini?

Natabiri hilo likitokea, hali itakuwa kama iliyoitokea kampuni ya kamisi na sidiria wakati watu walipoanza kuvaa vitu vingine au kutembea bila.

Hiyo hadithi ya Gen Z inaaminika kwa urahisi kuliko nyingine inayokaa ya kutungwa, ‘jaba’ hasa, ambayo inaturudisha kwenye siasa za mgawanyiko. Labda tumejipata katika hali tuliyomo kutokana na fikra za siasa za mgawanyiko.

Mwanangu shika hili: Usiwaamini wajanja wa mjini wanaokwambia Mlima umegawanyika. Labda wametumwa kukukoroga akili ili wakucheze shere. Mlima gani? Wa nani? Kwani wana mlima wao?

Ikiwa ni ule-ule mmoja Mlima Kenya ninaoujua, waambie walale waote ndoto nyingine, hii ni ya kitoto, sawa na uliyoota zamani ukiwa mdogo, ukaona maji yakitiririka mtoni polepole, ukaamua kuyaongeza ili yaende kasi, ghafla ukaloa na kujiuliza imekuwaje kukanyesha kitandani!

Ikiwa wajanja wa mjini hawajatumwa wakukoroge akili, wanataka kumkanganya na kumzuga akili Kasongo, mja anayewaza kuhusu uchaguzi wa mwaka 2027 saa zote.

Wamkanganye kwa manufaa gani? Ili aamini eti mlima ukigawanyika, hana haja kujali kitu, anaweza kujipenyeza na kupita katikati yao hao wanaogombana na wasimwone.

Hiyo nayo itakuwa danganya-toto kubwa mno. Kasongo ni mjanja, na bila shaka anajua mambo mengi ambayo hawezi kukwambia.

Anajua Mlima haujagawanyika, adui wao wa kisiasa ni mmoja: Kasongo. Naam, nimesema na nitarudia, huyo ndiye adui wa pekee wa kisiasa pale Mlimani.

Hivyo? Mlima uwe umegawanyika, au umegandana kama uliotiwa gundi, mradi kura zao haziingii kwenye kikapu cha Kasongo, wako sawa kabisa.

Nimewasikia watu wakisema hawajali ugomvi kati ya Jomo mdogo na mwenyeji wa Wamunyoro, ukweli utajulikana tukifika kwenye debe.

Kuhusu mgawanyiko unaosikia, zingatia kuwa mkondo wa siasa za Mlimani unawategemea zaidi watu wa kawaida kuliko viongozi. Hivyo? Mvutano kati ya viongozi haufai kukukosesha usingizi.

Usingizi na umpotee aliye na hakika ya kupata kura zao nyingi. Mshindi wa urais sharti apate jumla ya asilimia 50 ya kura, na angaa kura nyingine moja ya ziada. Usipotimiza hilo, nyumbani kunakuita!

Ukiwaza hayo, kumbuka hospitali ya Gen Z haitegemei kura za mtu, hivyo wao ni kusema na kutenda. Heri hao!

mutua_muema@yahoo.com