Jamvi La Siasa

KINAYA: Hivi wewe, umo kwenye kundi la ng’ombe au lile la watu?

January 19th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

“HII ndiyo wiki ambapo wazazi watauza ng’ombe ili wawapeleke ng’ombe wengine shuleni,” juzi amefoka rafiki yangu wa dhati (jina lake nimelibana) nikamshangaa.

Nimemuuliza iwapo ilikuwa ni lazima atukane watoto wa watu ambao masomo yakiingilia sikio moja yanatokea la pili, akajitetea kwa kuniambia kuwa ng’ombe si mnyama mbaya, anayemfuga huwa tajiri.

Hata watoto wanaochimba masomoni na kutifua vumbi si wabaya eti; werevu wa darasani na mafanikio maishani ni mambo mawili tofauti kabisa.

Hakika ng’ombe ni mali, si wabaya kamwe kama tunavyoona kwa jirani – Uganda.

Kwani kunaendaje? Mzee ‘Msaba’ amewafuga ng’ombe na watu pamoja, tabia zao zikafanana, sasa anahitaji kupiga mluzi tu uone ng’ombe wa kweli na ng’ombe watu wakitunga foleni kuelekea zizini au malishoni.

Tofauti ni pembe ndefu na matuta vichwani, lakini kisiasa na tabia, makundi ya watu na ya ng’ombe nchini humo ni mamoja, yanamtii mfugaji wao bila kusita kama askari waliofuzu jeshini.

Umeonaje uchaguzi wa urais uliofanyika hivi majuzi?

Mzee ‘Msaba’, hata baada ya kuitawala nchi kwa miaka 40, amedinda kung’atuka uongozini, amesema tumwache kwanza atawale kwa muhula wa saba.

Waganda, ambao amezimiwa mtandao wa intaneti, wanamtamani kama biriani, anajiambia.

Kumbuka huyo ni yule-yule kijana aliyeandika sheria iliyosema mtu aliyetimu umri wa miaka 70 hana akili za kuiongoza nchi, eti heri apumzike tu.

Kisha? Alipotimiza yake 70 wakazuka wazee wa kidini kumkumbusha alizaliwa lini, wakamkosoa kwa kudhani alizaliwa mapema kwa miaka kadha, sikwambii wakamwonyesha na ushahidi wa kadi kuukuu ya ubatizo na kumwita ‘kijana wetu’.

Mwenyewe alionekana kushtuka sana alipotanabahi kwamba alikuwa bado kijana wa miaka 60 na ushei… machachari kabisa wa kuiweka Uganda mahali pazuri kwa kila namna.

Kumbe sheria ya miaka 70 ilinuiwa kumzuia Dkt Milton Obote kurejea nchini humo na kumkabili Mzee ‘Msaba’ kisiasa! Kucheza shere ni sawa katika ulingo wa siasa, kawaida refa hupunga mkono na kupuliza kipenga, mchezo uendelee.

Kwa jinsi Mzee ‘Msaba’ alivyo mweledi wa kucheza na sheria za nchi, hasa zinazohusu uchaguzi, ama wewe ni mzee sana au mchanga sana kiasi cha kutomkabili mzee huyo mfugaji!

Usishangae akikataa mwaliko wa kuhudhuria hafla ya kumwapisha Rais wa Kenya mwishoni mwa mwaka ujao kwa kuwa kwake hiyo ni sawa na sherehe ya mazazi ya vitoto vidogo.

Atashirikije mchezo wa ‘cha mama na cha baba’? Anashangaa kwa nini Kenya tunawachagua ‘watoto’ halafu ‘tunawafukuza’ kazi baada ya miaka 10.

Hivi wewe ni ng’ombe au mtu? Ithibati ya kweli kwamba wewe huwi miongoni mwa ng’ombe ni kujiandikisha kupiga kura.

Ukifanya hivyo, unapata uhuru na ujasiri wa kutukana serikali ikikuudhi. Vinginevyo, fyata kabisa!

– Douglas Mutua ni mwanahabari Mkenya anayeishi Amerika ([email protected])