Jamvi La Siasa

KINAYA: Katika lile suala la kofi, nahisi ingekuwa Riggy G, mpiga na mpigwa wote wangeokotwa chini!

Na DOUGLAS MUTUA January 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HIVI umewahi kujipiga kofi kimakosa? Ulihisije?

Kinahadithiwa kisa cha mvuvi aliyevalia kaptula, akaketi kando ya ziwa huku kashikilia ndoano akisubiri samaki mjinga athubutu kula chambo, jioni hiyo awe kitoweo.

Ghafla alihisi mwasho fulani kwenye paja, alipoangalia akamwona nzi mkubwa aliyefanana na mbung’o. Wakati uo huo, ndoano yake ikatikiswa kidogo, kwa maana samaki akijaribu kula chambo.

Mwasho kwenye paja nao ukageuka kung’atwa, hivyo mvuvi akawa katika hali ya kukanganyikiwa: “Nimvue samaki kwanza, au nimwangamize nzi msumbufu?”

Hatimaye aliamua kuyafanya yote mawili wakati mmoja, akautumia mkono mmoja kuvuta ndoano kwa kasi, nao mkono wa pili akautumia kumpiga kofi la mwaka yule nzi.

Kwa bahati mbaya, kwa kuwa macho yake yaliangazia ndoano ili asikose kitoweo, kofi lake lilimkosa nzi likaangukia sehemu nyeti, akapiga mayowe na kuitupa ndoano ziwani! Siku hiyo alilalia mate.

Hata hivyo, hiyo haikuwa shida kubwa ikilinganishwa na maumivu ya kujipiga kofi mwenyewe. Hangalimlaumu yeyote. Hasira zilimpanda na zikajishukia zenyewe.

Alipata somo kwamba kofi halitoki kiholela, mtu anaweza kuihini jamii nzima bila kukusudia. Nzi ni wa kupuliziwa au kupepetewa tu akajiondokea na kujiendea zake.

Katika msimu huu wa kudai na kukanusha kwamba wapo watu wanaowapiga wengine makofi, binafsi nausikitikia uwezekano wa mtu mzima kupigwa kofi bila kutarajia.

Kofi la aina hiyo, kwanza la nyuma ya kiganja, hasa likiwa la usoni, huingia vizuri tu aliyepigwa ama akatokwa na mate mazito pamoja na kamasi, yote yakachora ramani isiyoeleweka au kibonzo ukutani!

Hilo linaitwa kofi la mwaka, na anayepigwa hana jibu hata akijaribu mara ngapi. Nimekueleza hali inavyokuwa, hivyo chukulia maelezo haya kama mafunzo ya kujikinga dhidi ya kofi lisilotarajiwa. Ukiduwaa litakupata. Usinilaumu.

Mjomba Abrah amekanusha kwamba alipata kofi, akajaribu kutusahaulisha uvumi huo kwa kufoka kwamba pale mlimani atapita na mtu.

Amemtishia eti Riggy G ataona cha mtema kuni. Labda amesahau kuongeza na kilichomtoa kanga manyoya.

Natumai hajipalii makaa kwa maana katika mambo hayo ya matumizi ya nguvu, hasa kwa kuwa hakuna aliye na ukiritimba wake, haitabiriki mwisho utakuwaje.

Vitisho vya Mjomba Abrah vimenichochea kutafakari kuhusu kisa hicho cha kofi: Hivi ingekuwa Riggy G, angelipokeaje kofi hilo? Nadhani angekufa mtu! Au, bora zaidi, mpiga na mpigwa kofi wangechukuliwa chini! Vumbi lingetifuka!

Na hatungesubiri uvumi, hizo zingekuwa habari ibuka, bila shaka za kugonga vichwa vya habari. Nina hakika mpiga watu kofi alijua ukweli huu, ndiyo sababu jeuri ya Riggy G haikuzaa kofi.

Kumbe siri ya kuzuia kofi ni kuigiza mambo, kama vile utundu na kutojali? Usitabirike. Igiza kichaa ikibidi. Utasazwa wengine wakizabwa vibao.

[email protected]