KINAYA: Kiburi cha Krismasi kimeisha huku vijijini, nina hakika uko tayari kurejea mjini!
HIVI umeacha kuteuka ovyo kama mtoto akimaliza kunyonya? Naambiwa siku tatu zilizopita ulirarua chapati na nyama kweli-kweli, hata labda ukanywa na ule ‘uji’ wa Ouru, lakini sasa mambo yameanza kubadilika.
Nasikia juzi ulisema ugali ulikuwa na ladha ya matope, nazo mboga-mboga kama sukumawiki, kabichi na mchicha nusra zikutapishe kwa ladha ya mwarubaini.
Hebu niambie, pombe za chupa ambazo hata ukiwa huko unakoishi huzikaribii zilifikaje kijijini kwa hisani yako? Ulienda kuonyesha nani kwamba hata nawe haya mambo si mageni kwako?
Kila ulipopata kiu ya maji ulikunywa pombe eti, mikono nayo ulinawa kwa pombe ya kienyeji ili kuua viini vya maradhi usifie kijijini siku chache ambazo ulinuia kukaa huko.
Uliwaambia wenyeji ulishangaa wamesalia hai vipi kwa muda mrefu hivyo ilhali jirani zao ni nzi, viwavi na funza ambao hawakuacha utafune nyama yako kwa amani.
Ulipopewa majani kuwafukuzia wadudu hao na kujipepetea ili joto lipungue, ulisema hujazoea miti-shamba, huenda ukaambukizwa ugonjwa wa pumu kutokana na harufu ya ‘vitu’ vya porini usivyojua manufaa yake ya kisayansi. Daktari wako hajapendekeza uyatumie eti.
Hukutaka watoto wako watangamane na wa ndugu zako wanaoishi kijijini kwa kuwa washamba wasiojua kuzungumza ‘sheng’ wangeshawishi kuiga ndimi za kishamba, zaida wafunzwe utundu.
Sasa ona, ulivyovidharau vimeanza kupendeza baada ya siku tatu pekee. Sukuma-wiki na mboga-mboga nyinginezo zina ladha ya kipekee, hata umekumbuka ushauri wa daktari kwamba kisukari hakiendani na vyakula vya wanga kama vile chapati na wali.
Ugali unalika vizuri, una ladha ya keki, ni wanga ila haujakudhuru tangu utotoni, na ukishamaliza kuula unajiuliza iwapo kuna haja ya kunawa mikono ambayo umekwisha kutakatisha kwa kuiramba!
Tayari umejua kwa ‘mama pima’, kileo chake kimegeuka bora kuliko hivyo vilivyopikwa kwa kemikali za Wazungu, nayo makopo ya plastiki unayonywea yanapendeza kuliko chupa za baa kwa kuwa ni makubwa, unatosheka haraka.
Sasa umefanana nasi, hata si lazima unawe mikono ukila kwa sababu huku kwetu kijijini hakuna viini vibaya vya maradhi, uchafu ni udongo tu, ambao hauna hatari yoyote.
Watoto wako, ambao hukutaka wafunzwe ushamba, sasa wanatema lugha ya bibi yao vizuri, umekubali wacheze na washamba, na umegundua hawawezi kuambukizwa maradhi.
Hawaogi kila siku, na bado hawajaanza kunuka. Wamezoeana na nzi pia.
Gari ulilokodi linahitaji kurejeshwa. Mwenyewe anadai malipo kila siku. Unasema utalirejesha kesho likishakufikishia unakoishi gunia la mahindi, mikungu 10 ya ndizi na magunia matatu ya mboga-mboga za kienyeji.
Tayari pakiti mbili za unga wa ngano ulizoleta zimekwisha. Unakorejea hukuacha kitu. Ni lazima wewe na watoto wako mlishwe na hawa washamba kwa mazao ambayo hamtaki kujua yanakuzwa vipi, kwa gharama gani.
Mtu mzima unaogopa kurejea unakoishi kwa kuwa umekumbuka shule zitatoza karo kuanzia mwaka ujao, hali unadaiwa kope si zako. Unajuta.
Hutarudia kosa hili la ubadhirifu eti, lakini uliapa hivyo mwaka jana wakati kama huu.
Utakopa ulivyokopa mwaka jana, lakini tafadhali kumbuka kulipa madeni kwa kuwa mpaka sasa uliowakopa wanakudai, tena unawapiga chenga kila ukiwaona.
Omba Mungu akutoe kwenye shimo hili, na umwahidi hutajirudisha humo. Kwako azimio pekee la mwaka mpya liwe uwajibikaji.