KINAYA: Mzoa-taka wa Nairobi sasa mateka wa Kasongo na Babu!
PALE Mlimani – ambapo tohara inachukuliwa kama nishani ya dhahabu – pana vichekesho vingi, ila kipo kimoja ambacho nusra kinitegue mbavu kila ninapokikumbuka.
Kinahusu tohara. Ikiwa hukukutana na kisu cha ngariba, machoni pao bado wewe si mwanamume kamili.
Anaimba rafiki yangu, Kamande wa Kioi, kuhusu kisa ambapo bwana fulani alitoroka kisu cha ngariba na kwenda kuishi mbali.
Alipotimu umri wa kuoa, alipata mrembo fulani na akafanikiwa kumshawishi asiwahi kutoboa siri hiyo.
Mrembo aliridhia, lakini akamfanya yule bwana mateka wake hivi kwamba kila wakikosana, mke anamwambia mume: “Thubutu kunigusa tu, nitawaambia watu bado hujakatwa!’ Kila wakati mume akinywea na kujishika tama kwa huzuni.
Kichekesho kingine (au labda ni tusi?) kilichokuwa maarufu sana utotoni kilitania kuhusu umaskini: “Kwenu ni maskini sana, mnaishi nyumba ya nyasi, kwa hivyo wezi wakiwavamia wanawatishia ‘fungueni mlango au tuwalete ng’ombe!’”
Sijui maisha yangekuwaje bila vichekesho. Kimoja kati ya vingi vilivyowahi kunichekesha mpaka nikajisahau kilikuwa kwenye kipindi cha ‘Vioja Mahakamani’ ziku zile.
Mhusika Makokha ameambiwa na mwenzake: “Wewe una sura mbaya hivi kwamba mtoto wa jirani akisusia chakula anaambiwa ‘kula au nimwite Makokha!’”
Hakuna kitu kibaya kama kujipata katika hali ambapo una siri au udhaifu ambao kwao watu wanaweza kukutishia ukafanya mambo yao shingo upande.
Hiyo ndiyo hali aliyo mzoa-taka wa Nairobi ambaye wakati mwingine akikasirika huzimwaga taka zenyewe mlangoni pako, hasa ikiwa hujamlipa ada za umeme.
Juzi ameponea kung’atwa na wawakilishi wa wakazi wa Nairobi waliolilia maini yake. Walitaka kumrarua kama tambara bovu au kumnyofoa kama mnofu wa karamu, lakini alijaliwa na nyota ya jaha.
Naambiwa alinusurika kwa hisani na jitihada za Kasongo na Babu wa Bondo; wawakilishi hao waliambiwa waache kiherehere kingi, wakaukalia mswada wa kumtimua mzoa-taka.
Kuponea ni kuzuri, hasa kwa kuwa hakuna mtu anayependa kuangamia, lakini kuna madhara yake.
Anayekusaidia kunusurika akitaka anaweza kukufanya mateka wake hivi kwamba utatii kila neno litokalo kinywani mwake.
Siasa zina siri nyingi, na wanasiasa wenyewe wanajuana. Kasongo na Babu wa Bondo wanaweza kutumia siri na madhaifu ya mzoa-taka kumhangaisha kati ya sasa na uchaguzi mkuu ujao.
Cha muhimu sasa hivi ni kwamba ameponea, lakini wawili hao wana ukiritimba wa kutunza au kufichua siri zake za ndani, kuwaleta ng’ombe wale paa la nyumba yake, au wamwite mpinzani wake, Babu Owino, amkoseshe usingizi. Siasa wewe!
mutua_muema@yahoo.com