KINAYA: Nakuombea mateso ikiwa bado unasubiri kuunganishwa kikabila
CHAKULA ni kitamu. Kizuri kwa afya pia. Kinajenga mwili. Lakini Wakenya hawapendi kula kabla ya viongozi wao.
Si heshima eti kula kabla ya wakubwa, na ndiyo maana jamii nyingi nchini zinawalaumu viongozi wazo kwa kutokaa mkao wa kula, wapakuliwe minofu na mapochopocho.
Ili viongozi wetu waonyeshe kwamba wana nia ya kula na kushiba, sharti kwanza watuunganishe, au wajifanye kama wanatuunganisha, kisha watupige mnada kwa atakayekuwa na mabunda ya noti.
Tuna hasira nyingi tunapowauliza kwa nini hawataki kuunganisha jamii zetu kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027. Utadhani kura zinapigwa kwa makundi, hazipigiki mtu binafsi akijiunga na foleni na kutia kura ndani ya debe.
Labda viongozi wanaolaumiwa kwa kutounganisha jamii zao wameshiba, sisi pekee ndisi tunaongurumwa na matumbo, hivyo tunajitetea kijanja huku tukijifanya tunawajali.
Ikiwa muungano wetu ni muhimu sana, mbona tusiungane kwa hiari yetu wenyewe, tukatae kutengana, tuishi kwa amani bila kuwahitaji viongozi wa kijamii?
Tena, katika karne hii, kuna umuhimu gani kujitenga kijamii? Mbona wanaotafuta vyeo wasije kwetu moja kwa moja? Tunataka tutengezewe njia za kula tu!
Miungano hiyo ingekuwa na manufaa zaidi tungeifanya ya wananchi wa taifa moja, bila kutengana kijamii, tuwape viongozi masharti ya kuwapigia kura, sote tusaidike.
Tayari tumetangamana, tukaoana na kuzaliana kwa njia changamano hivi kwamba maslahi yetu yamekuwa mamoja. Siku hizi ukirusha mawe kiholela unamgonga ndugu yako.
Ajabu, makabwela wanaolilia miungano ya kijamii huenda miayo kwa njaa, lakini bado wanaamini viongozi wao wa kijamii wakila, hata nao wameshiba.
Miungano hiyo huwa njama za kuwapumbaza wananchi wa kiwango cha chini ili wawe na matumaini kwamba siku moja bahati itasimama waishi maisha ya raha na starehe.
Pepo wa mauti naye anafuata ratiba yake bila kukosa, hivyo anafika kwa wakati kabla ya matamanio hayo kuafikiwa.
Makabwela wanaosazwa wanabaki wakisubiri, lakini matokeo ni yale-yale ya viongozi wao kunufaika, nao kukaukiwa.
Ikiwa hali yako ndiyo hiyo, nilaumu kwa kuwa mwenzako nikitia dua tangu mwanzo ili uendelee kuumia kwa kuwahimiza viongozi wako eti waunganishe jamii kana kwamba Kenya ni yenu peke yenu.
Hiyo hadithi ya muungano huwa tamu sana hadi pale kinamwana wa mlimani wanaposema hata nao wataungana. Mara nyingi jamii nyingine huwajia juu na kusema huo ni ukabila.
Kila ninapoona hivyo najiuliza: ni sehemu gani ya akili yako inayotambua ukabila katika jamii moja na muungano mwema katika jamii nyinginezo?
Ikiwa kuwashibisha viongozi wa kikabila ni muhimu kuliko maendeleo, basi na tuendelee kuwahimiza watuunganishe. Tutakula mwata milele. Isiwe vigumu kutumia akili ndugu yangu.