KINAYA: Ni afueni vita Iran-Israel vimenyamaza kwa sababu tungepika uji tule nao ugali
NAJUA vita vinaendelea kati ya Israel na Iran, lakini sharti niseme siwezi kuzuia kicheko kila wakati taifa la Iran linapotajwa.
Linanikumbusha ziara ya aliyekuwa rais wake, Mahmoud Ahmadinejad, nchini Kenya mnamo mwaka 2009.
Kwa dharura, alitafutwa mkalimani kwa ajili ya kufanikisha mawasiliano kati ya Rais Mwai Kibaki na mgeni wake huyo kutokana na uhaba wa Wakenya waliofahamu lugha ya Kiajemi (Kifarsi) wakati huo.
Bahati ilimwangukia barobaro wa kawaida ila aliyesafiri sana, tena rafiki yangu, tuliyezoea kupiga gumzo naye nje ya Msikiti wa Jamia, Nairobi, akachangamka ajabu kwa tafsiri ya kueleweka!
Ingawa alifanya kazi vizuri, malipo hayakuwa mazuri kama tulivyotarajia, kwa hivyo, ziada ya kumhongera kwa kuonekana kwenye runinga, hakutununulia chai wala kutuandalia sherehe aliyotuahidi kabla ya kuchukua jukumu hilo.
Hata hivyo, alituchekesha sana kwa kusema jinsi alivyotamani Rais Ahmedinejad amsalimu kwa kumkumbatia ili apate fursa ya kumwambia kwa matao ya chini: “Mzee, maisha ni magumu Kenya hii, niachie donge nono nijisaidie kimaisha au unibebe twende nawe Tehran.”
Maisha yangali magumu nchini Kenya, labda kwa kiasi fulani kwa kuwa makubaliano ya ushirikiano wa kibiashara ambayo marais hao wawili waliafikiana hayakutimizwa.
Ahadi ya Iran kuiuzia Kenya mafuta kwa bei nafuu, sikwambii na nyingine ya kujenga kiwanda cha kuzalisha nishati ya nyuklia mjini Thika, ilisalia ahadi tu na kuvunjika kabisa mnamo mwaka 2012.
Matumaini yangu kwamba vijana wetu wangepata kazi kiwandani humo, na, bora zaidi, kiburi na ule ukiritimba wa kampuni za uzalishaji na usambazaji umeme nchini Kenya uishe ghafla, yalididimia pakubwa.
Je, vita vya Israel na Iran vitaathiri maisha ya Mkenya wa kawaida vipi? Iran iko mbali na Kenya kiasi kwamba yanayoendelea huko hayatuhusu? Bila shaka mfumko wa bei za bidhaa utazuka. Uchumi wa dunia utadorora.
Nauli za usafiri wa umma nchini Kenya zitaongezwa kwa kisingizio kwamba mafuta yamekuwa ghali. Kumbuka tatizo likitokea tu, wafanyabiashara wa Kenya hawakosi kuligeuza kuwa fursa ya kujinufaisha.
Hata usafirishaji wa mazao na bidhaa utakuwa wa gharama ya juu, kwa hivyo bidhaa zenyewe zitamfikia mteja wa mwisho zikiwa ghali zaidi. Huenda tukalazimika kupika uji ili tulie ugali.
Ni jambo la busara kwa watu kujizuia kuwa wabadhirifu wakati huu, watumie pesa na bidhaa walizonazo kwa vipimo kama dawa, kwa kuwa kesho haijulikani. Hata uhaba usipotokea, akiba yetu itakuwa palepale, na kamwe haitaoza.
mutua_muema@yahoo.com