Jamvi La Siasa

KINAYA: Tunakoenda, tutahitaji mtu akijiuzulu atuonyeshe ithibati

Na DOUGLAS MUTUA July 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

UTAJIFUNZA kuniamini. Nilikwambia Kenya ni jukwaa kubwa la sarakasi. Waigizaji ni wachache, lakini watazamaji ni 50 milioni na ushei!

Mkuu wa sakafu, anayeamua taa zitamulika wapi, na wapi kuwe na giza nene, ni serikali yenyewe. Na anaelekeza vipindi akiwa nyuma ya pazia. Tunashuku yupo, lakini hatumuoni.

Serikali si mtu binafsi. Ni kama jini au pepo, humgusi akagusika, lakini anafanya mambo mpaka mwenyewe unashuhudia ni mjanja, hawezekani.

Labda kizazi kipya cha Gen – Z hakijui, lakini tuliwahi kuwa na waziri fulani jeuri kweli, marehemu John Michuki, aliyetwambia serikali inaweza kukung’oa meno yote, uwe kibogoyo, kisha ikwambie uende ukashtaki unakojua!

Hivi majuzi tumemwagika barabarani kwa fujo ili kumshinikiza Naibu Spekta Mkuu wa Polisi, David Lagat, ajiuzulu, na tukaambiwa amefanya hivyo.

Kumbe mwanaume alikwenda likizo yake ya kila mwaka, akawa yuapokea mshahara kama kawaida, wajinga tukabaki barabarani tukikimbia kutoka kona moja hadi nyingine kama tuliochomekwa mzizi na mchawi akafa!

Kwani jini aitwaye serikali anatuonaje? Labda anadhani tunatumia ukamasi kufikiria, lakini nadhani tungali werevu kwa kiwango kizuri tu. Makachero wetu wa kujitolea, walio na ofisi mtandaoni, wamegundua tulihadaiwa.

Naam, kama walivyogundua kuwa baaadhi watu tulioandamana nao walinunuliwa kwa bei ya kitunguu (hata hicho nasikia kinauzwa bei ghali) na kutuacha kwenye mataa tukinusa moshi wa vitoa-machozi.

Kasamweli, yule jombi aliyelinganishwa na marehemu Tom Mboya kwa ufasaha wa kunena Kiingereza na ujasiri wa kuikabili serikali, yuko Amerika ambako anasoma masuala ya uongozi kwa ufadhili wa serikali. Kumbe?

Pamoja na usaliti wote huo, usikate tamaa. Sasa tumejua si lazima mapambano yaongozwe na watu maarufu ili yafaulu, viongozi si muhimu, mradi vijana watajitokeza panapo haja.

Kila mtu anajua Gen – Z wametetemesha ardhi inayokanyagwa na jini aitwaye serikali bila kuongozwa na Babu RAO. Huo ni ufaulu mkubwa, na labda unaikosesha serikali usingizi.

Tangu hapo serikali huingia wasiwasi mkuu inapokabiliana na kundi la watu wasio na kiongozi. Haijui kwa kuanzia wala kwa kuishia. Naam, hasa ikiwa kundi hilo limekataa kugawanywa kwa misingi ya kikabila.

Huwezi kuwachezea watu wanaojasiria kuelezea tatizo lao na Kasongo kwa maswali rahisi: “Mambo tuliyokubaliana (wakati wa kampeni za uchaguzi), ameyafanya? Na anayofanya, tulikubaliana?”

Nadhani tunakoelekea, hatutakubali ahadi za kisiasa ambazo hazijaandikwa popote, zikasainiwa na kupigwa mhuri. Hata watu wakijiuzulu, tutawalazimisha watuonyeshe ithibati kwamba hawalipwi mishahara.

Na mtu asithubutu kuwalipa kwa M-Pesa, tutachunguza hata miamala ya kifedha inayofanyika kwa simu zao. Hili ndilo tatizo la kuelimisha watu bila ada na kutowabunia fursa za kazi. Tutabanana papa hapa mpaka kieleweke.

mutua_muema@yahoo.com