KINAYA: Turuhusiwe ‘kuvuna’ figo zetu kisheria
HIVI mbona tusionyeshe heshima, angaa kidogo tu, hata ‘tunapovuna’ na kuuza figo za watu?
‘Unapoivuna’ yangu bila kuniambia, halafu unaipandikizia mgonjwa asiyejua ni ya kuibwa, umeniachaje?
Angalau ungeniachia mwanya mdogo wa kujua ‘umenipunguza’ ili nami nitafute huko mitaani ni nani anayetembea na figo ya kuibwa bila taarifa.
Nikipata fursa ya kukutana na aliyenufaika na figo yangu ninaweza ama kuamua kumwachia, hasa kwa kuwa moja inanitosha, au nimfunze kikwetu.
Ninakotoka, na hapa nazungumza kama mjukuu wa mfugaji, tukipata mtu na ng’ombe wa kuibwa, kawaida tunamswaga ng’ombe huyo hadi zizini mwetu, kesi baadaye!
Fikra hii inatokana na ukweli kwamba mwizi wa ng’ombe amenichosha sana nikimtafuta, hivyo wewe uliyeuziwa unaweza nawe kuchoka ukimfuata aliyekuuzia ili akurejeshee pesa zako.
Muhimu zaidi ni ujifunze kuthibitisha vitu kabla ya kuvinunua kwa sababu vikiwa vya kuibwa, wewe na mwizi mnanyolewa kwa wembe mmoja.
Hata kisheria, anayepatikana na mali ya wizi huchukuliwa kuwa mwizi pia na kuadhibiwa ipasavyo kwa maana ndiye anayembunia mwizi soko.
Hata hivyo, kwa kuwa tumeumbiwa utu, katika kisa cha figo na sehemu nyinginezo, nawasihi wezi wazingatie kwamba hata nikikutana na mtu akiwa na figo yangu, siwezi kuing’oa kama mche na kwenda nayo nyumbani.
Nitamrai anirejeshee, na akinisadikisha kwamba anaitegemea sana, labda nitamwambia anunue chai tu tumalize maneno hayo badala ya kuwahusisha polisi.
Makubaliano ya aina hii humsaidia aliyeathiriwa na wizi, na aliyenufaika na wizi pia. Mwizi naye? Laana anayo tayari kwa sababu sehemu hizo muhimu hazipandwi shambani, ni zawadi ya Mungu.
Kisa cha Hospitali ya Mediheal kushukiwa kwamba inaiba na kuuza figo za watu kimenikumbusha kitu nilichoambiwa na rafiki yangu wa dhati nilipohamia Amerika.
Nilitahadharishwa kwamba nikijaza fomu ya kuomba leseni ya kuendesha gari, nisijaze chochote katika sehemu inayokuomba uwaruhusu ‘kuvuna’ sehemu zako za mwili.
Alinishtua aliponieleza kuna matajiri wengi ambao wamelazwa hospitalini wakisubiri kupandikizwa sehemu kadha, kama vile moyo na figo, kwa hivyo ajali ikitokea, nionyeshe dalili za kutaka kutangulia ahera, ‘nitavunwa’ upesi!
Tangu hapo, kila nikijaza fomu hiyo, kitu cha kwanza huwa kuziba sehemu inayoniomba nikubali ‘kuvunwa’ ili nisiijaze kimakosa nikaishia kuwa bidhaa. Watu si wema aisee!
‘Wavunaji’ wa Kenya wanapaswa kuwa na fomu za kujazwa, angaa tujue wanahitaji vitu hivyo ili tuwe waangalifu zaidi, tusiibiwe.
Wakenya wengi wanauliza: Katika uchumi uliozorota hivi, kuna haja gani kuwa na figo mbili, mapumbu mawili, macho mawili na kadhalika ikiwa sehemu moja ya hizo inaweza kutumika bila matatizo?
Tunapaswa kuwaita watu kama hao wafadhili uchumi, si wahujumu uchumi. Kwa hivyo? Haidhuru kuwatungia sheria ya kuwadhibiti na kuwasaidia ‘wasijivune’ wakiwa hai mpaka waishe.