Jamvi La Siasa

KINAYA: Uchaguzi wa Mbeere umefichua siri nyingi

December 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SIASA zina maneno, hutaka moyo wa chuma. Wako wa karatasi au plastiki ukalishe nyumbani kwa mama yako; ukiuleta huku nje tutaurarua bila huruma kisha tukucheke, ukija juu tukwambie ukashtaki unakojua.

Ama unafikiri kulia na kusaga meno unakosikia kuhusiana na uchaguzi wa ubunge wa Mbeere kunatokana na sherehe za mazazi ya watoto?

Watu wameshikwa mashati, wakakabwa koo, wakatemewa mate usoni, kufumba na kufumbua wakazabwa makofi ya kope, maskini wakaona vimulimuli!

Binafsi Mbeere imenifunza mengi, lakini muhimu zaidi imenifichulia siri za watu. Hivi unaelewaje mtu anapofoka hadharani kwamba kwa kuwa Wambeere wamekataa kumchagua mgombea aliyempenda, yeye na marafiki zake wataacha kununua uchawi Mbeere?

Mwingine anazuka na kuuliza swali ambalo kwangu lina mantiki ya hakika: Ikiwa kweli Wambeere walimchagua Wa Muthende, kwamba kamwe hakujaziwa kura na wahuni waliovamia vituo viwili vya kupigia kura, mbona mpaka sasa hawajamwagika mitaani kushangilia ushindi wake?

Wambeere wachache ninaoona mitandaoni wakisema waache kutukanwa na kila mtu aliyetarajia Newton Karish ashinde hawatoshi kumpitisha mtu akapata ubunge.

Hata hivyo, wapo wanaosema mambo ya maana kweli! Mathalan, mmoja aliwaambia wakazi wenza wa mlimani ambao hawakurithika na matokeo hayo wamwambie kuna milima mingapi Kenya!

Kisa na maana? Mbeere hakuna kahawa wala majani-chai, kilimo ambacho kimetajirisha maeneo mengine ya Mlima Kenya.

Aliwauliza: “Hivi mlima wenu huu una manufaa gani kwetu? Tutajiitaje watu wa mlima mmoja ilhali hamjawahi kutusaidia katika umaskini wetu huu?”

Maneno hayo yalinifungua mawazo nikaona ukweli fulani: ni rahisi mno kuugawa Mlima Kenya mara mbili kisiasa! Labda hata umegawanyika.

Kasongo anajua ametalikiana na Mlima, nikaha yao ya mwaka 2022 imegeuka kisirani, lakini hataki kutoka bure, hivyo atakata angaa kipande kidogo cha blanketi ili ajifunikie uso.

Kipande hicho kidogo kikienda na Kasongo kitamwacha Wamunyoro katika hali mbaya zaidi kwa kuwa tangu hapo akitwambia ana mamilioni ya kura.

Zikipunguzwa, washirika wake katika muungano wa upinzani watamwambia aache kiburi na kiherehere, kila mtu ana kura.

Bila shaka Wamunyoro hatukanwi akafyata, lazima atoe jibu la cheche za moto! Atawakumbusha ndiye naibu rais wa wananchi, tena wa kwanza kuchaguliwa, hivyo waliomchagua wanaweza kufuta neno ‘naibu’, wakaacha ‘rais’ kwa kuwa wanampenda, hivyo atawania urais ifikapo 2027.

Uamuzi huo utamuatua moyo Mzee Wiper, ambaye anasubiri kukabidhiwa kigoda cha ikulu na wenzake katika upinzani kwa kuwa ndiye mzee kabisa, hivyo hana fursa nyingine ya kuwania urais.

Kwa hivyo? Wasipompa atawania urais kwa tiketi ya Wiper, na liwe liwalo! Wiper na Wamunyoro wakitengana, Kasongo atapigia gitaa mfukoni kwa raha zake kwani muhula wa pili utakuwa umeiva.

Hilo likitokea, watu wa kutukanwa watakuwa wengi kuliko watukanaji. Wagonjwa wa msongo wa mawazo wataongezeka maradufu pia.

Chaguo ni lako; unataka kutukanwa, kutukana, kurukwa na akili au kuwa mshirikina! Kwa vyovyote vile, utasalia Mkenya.

Douglas Mutua ni mwanahabari Mkenya anayeishi Amerika

([email protected])