• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:55 AM
Kivuli cha Uhuru kilivyo tishio kwa Gachagua Mlima Kenya

Kivuli cha Uhuru kilivyo tishio kwa Gachagua Mlima Kenya

NA MOSES NYAMORI

MKONO wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kwenye harakati za kisiasa zinazoendelea katika eneo la Mlima Kenya, unatishia kuvuruga hatua za kisiasa alizopiga Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Bw Gachagua amekuwa akijaribu kuliunganisha eneo hilo , kwenye juhudi zake za kumrithi Bw Kenyatta kama kigogo wake mkuu wa kisiasa.

Hata hivyo, mwaka mmoja baada ya kustaafu kama Rais, Bw Kenyatta amerejea tena kupitia chama chake cha Jubilee.

Chama hicho kinapanga kujifufua kisiasa kupitia usajili mkubwa wa wanachama wake katika eneo hilo, kikilenga uchaguzi mkuu wa 2027.

Bw Kenyatta pia amekuwa akirusha makombora yake ya kisiasa katika ulingo wa kitaifa, hali ambayo imemfanya Rais William Ruto na washirika wake kuongeza ukosoaji wa kisiasa dhidi yake.

Viongozi hao wamekuwa wakidai Bw Kenyatta amekuwa akijaribu kuvuruga mipango muhimu ya maendeleo ya utawala wa Kenya Kwanza, kama vile mpango wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu na afya bora kwa wote.

Bw Kenyatta na washirika wake wanadaiwa kukita juhudi zao kwenye ghadhabu inayokisiwa kuwepo miongoni mwa wapigakura, kutokana na hatua ya Rais Ruto kushindwa kutimiza ahadi nyingi alizotoa kwao wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa Agosti 2022.

Sababu nyingine ambazo kundi hilo linalenga kukita ukosoaji wao dhidi ya uongozi wa Rais Ruto na Bw Gachagua, ni kiwango cha juu cha ushuru ambacho serikali imekuwa ikiwatoza wafanyabiashara na kupanda kwa gharama ya maisha.

Eneo hilo pia limeshuhudia urejeo wa kiongozi wa zamani wa kundi la Mungiki, Bw Maina Njenga, licha ya maafisa wa serikali kudai kuna njama za kulifufua upya kundi hilo haramu.

Kwenye mahojiano ya awali na Taifa Leo, Bw Njenga, alisema kuwa lengo lake kuu ni kuliunganisha eneo hilo ili kuhakikisha linazungumza kwa sauti moja. Bw Njenga ameibukia kuwa mpinzani mkubwa wa kisiasa wa Bw Gachagua katika ukanda huo.

Bw Njenga alidai amekuwa akifanya mazungumzo ya mara kwa mara na Bw Kenyatta, kiongozi wa Narc-Kenya, Bi Martha Karua na Katibu Mkuu wa Jubilee, Bw Jeremiah Kioni, kuhusu juhudi za kuvumisha Vuguvugu la Kisiasa la Kamwene. Vuguvugu hilo ni kundi linalowaleta pamoja viongozi wa kisiasa katika eneo hilo, hasa wale walio katika upinzani.

Wadadisi wanasema kuwa Bw Kenyatta bado ni tishio kubwa kwa Bw Gachagua, kutokana na umaarufu wake na uwezo mkubwa wa kifedha alio nao.

Shughuli zake alizofanya juzi—kwa mfano kufanya mkutano na viongozi wa Jubilee—zinaonekana kama juhudi za kulikomboa tena eneo hilo kisiasa.

Wadadisi pia wanaeleza kuwa dhana ya utendakazi duni wa serikali ya Kenya Kwanza unaonekana kumpunguzia ushawishi Bw Gachagua huku ukimjenga Bw Kenyatta.

  • Tags

You can share this post!

Nimekubali kifo cha Fidel, asema Ida Odinga akiadhimisha...

Mvua kuendelea kushuhudiwa maeneo mengi nchini –...

T L