Jamvi La Siasa

‘Kizazi cha Kibaki’ kinavyopangua siasa

Na BENSON MATHEKA July 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KUNDI jipya la wapigakura linaendelea kuwakosesha usingizi vigogo wa siasa tunapoelekea katika Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Hili ni kundi la vijana waliolelewa na kukua chini ya utawala wa marehemu Rais Mwai Kibaki, kizazi cha Gen Z na sehemu ya Millennials.

Tofauti na vizazi vilivyotangulia, kizazi hiki hakina uaminifu wa moja kwa moja kwa vyama vya kisiasa au viongozi maarufu. Kinadai sera faafu na zinazotekelezeka, maendeleo yanayoonekana, na uongozi unaojali watu – si ahadi zisizotekelezwa.

“Sisi tunaangalia rekodi ya uongozi, si hadithi za vita vya kisiasa vya miaka ya tisini,” anasema Faith Mwikali, mwanafunzi wa chuo kikuu na mmoja wa washiriki wa maandamano ya Julai 2024.

Katika maandamano hayo ya kitaifa dhidi ya Mswada wa Fedha wa 2024, Gen Z walionyesha uwezo mkubwa wa kujiandaa na kujipanga – wakitumia TikTok, X (Twitter), na Instagram kushirikiana, kuchangisha fedha, na kupitisha ujumbe wa pamoja bila mwongozo wa wanasiasa.

Licha ya juhudi za baadhi ya wanasiasa wa upinzani kujipenyeza katika harakati zao, vijana walitoa msimamo wa wazi wakiwapuuza.Walishinikiza serikali ya Rais William Ruto kukataa Mswada wa Fedha 2027 na wameendelea kuwa mwiba kwa utawala wake licha ya kutumia ukatili kuwanyamazisha.

Wanasiasa wakongwe kama Raila Odinga na Kalonzo Musyoka na sasa Rigathi Gachagua wameshangazwa na mwelekeo huu, huku wakiendelea kupoteza uungwaji mkono miongoni mwa vijana ambao wamechukua mwelekeo wao wenyewe kupigania haki zao.“Raila haeleweki na kizazi cha sasa.

Mara alitetea maandamano, mara anawashauri vijana wasijitokeze barabarani. Kwao, anaonekana mpatanishi wa mfumo aliokuwa akipinga na aliyokuwa akipigania,” alisema Billy Okea, mwanaharakati Gen Z.

Upande wa serikali pia haujaepuka changamoto. Rais William Ruto, licha ya kujiwasilisha kama kiongozi wa masikini kupitia kampeni ya “bottom-up”, sasa anakabiliwa na hasira za vijana kutokana na mzigo wa ushuru, ukosefu wa ajira, na kushindwa kwa serikali kutimiza ahadi zake za kiuchumi.

Ahadi Hewa

“Hauwezi kuongoza vijana kwa lugha ya matumaini pekee. Wanataka matokeo. Wao wanaumizwa na gharama ya maisha kila siku. Hivyo, watapiga kura kwa uchungu,” anasema Joseph Kisilu, mchambuzi wa masuala ya kijamii.

Anasema vigogo wa siasa wanalazimika kufikiria upya siasa zao kutokana na shinikizo za vijana. Ukabila, siasa za ahadi hewa haziwavutii tena Gen Z. Kwao, uhalisia wa maisha, uwajibikaji wa kifedha, na haki za kiraia ni nguzo kuu.

“Gen Z si kikundi cha wafuasi wa kisiasa. Ni nguvu ya kiraia. Wana uwezo wa kubadili mwelekeo wa siasa zote nchini – kuanzia MCA hadi Ikulu,” asema mdadisi wa siasa Peter Katana.

Katika baadhi ya maeneo, mashirika ya vijana yameanza kampeni ya kujisajili kupiga kura kama maandalizi ya uchaguzi wa 2027. Wanapanga kutoa wagombea wao kupitia majukwaa huru, wakikataa kabisa vyama vya kisiasa vinavyoongozwa na wanasiasa wakongwe.

“Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kenya, kuna uwezekano wa uchaguzi kutoweza kutabirika kwa misingi ya vyama na ukabila. Kizazi hiki kilichozaliwa au kulelewa chini ya utawala wa Kibaki wakati Kenya ilikuwa na fursa sawa kwa wote, elimu bora, na maendeleo yasiyobagua ni mwiba kwa vigogo wa kisiasa ambao walizoea kuhadaa wapiga kura,” asema Katana.

Anataja Gen Z kama “watoto wa Kibaki” waliopata elimu, wanaojua kusoma, kufikiri na kuuliza maswali’, jambo linalowafanya kuwa vigumu kushawishi kisiasa.“Gen Z ni kundi la wapiga kura wapya wanaopinga ukabila. Mtu yeyote atakayewapuuza, kuanzia MCA hadi Rais, atashangaa sana,” aliongeza.