Jamvi La Siasa

WALIOBOBEA: Mbiyu Koinange ndiye Mkenya wa kwanza kusomea Amerika

Na BENSON MATHEKA January 11th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

PETER Mbiyu Koinange, aliyezaliwa mwaka wa 1907, alikuwa miongoni mwa kundi la kwanza la wanafunzi wa Shule ya Alliance ilipoanzishwa 1926.

Mwaka 1938, aliweka historia kwa kuwa Mkenya wa kwanza kupata shahada ya uzamili (MA).

Baba yake, Chifu Mkuu Koinange wa Mbiyu, alimpeleka Amerika mwaka 1927 kumalizia elimu ya sekondari na kujiunga na masomo ya juu, hivyo kuwa Mkenya wa kwanza kusomea Amerika.

Mbali na kusomea Ulaya kwa miaka mingi, Koinange alikuwa mtu mwenye sifa bora za kielimu na kijamii.

Baadaye alikuja kuwa mshirika wa karibu sana wa Rais wa kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta, katika kipindi chote cha uongozi wake, kiasi cha kupewa jina la utani “Kissinger”, akilinganishwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Amerika wa wakati huo, Henry Kissinger.

Alianza masomo katika Chuo cha Hampton, West Virginia, kisha akaendelea na masomo katika Chuo Kikuu cha Ohio Wesleyan ambako alipata shahada ya kwanza (BA).

Baadaye alisomea shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Columbia.

Aliporejea Kenya, yeye na babake walianzisha Chuo cha Ualimu cha Kenya huko Githunguri, Kiambu, ambacho kilikuwa msingi wa shule huru katika Kenya wakati wa ukoloni.

Taasisi hizi zilikuwa nguzo muhimu katika harakati za kupigania uhuru.

Kati ya 1938 na 1947, Koinange alikuwa mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Ualimu Kenya, Githunguri, na kati ya 1951 na 1959 aliwakilisha chama cha Kenya African Union (KAU) barani Ulaya.

Mwaka 1947 alimkabidhi Kenyatta usimamizi wa shule hiyo na akaenda Uingereza kusomea stashahada katika Taasisi ya Elimu ya Chuo Kikuu cha London, kisha masomo ya juu katika Shule ya Uchumi ya London (LSE).

Koinange na Kenyatta walikuwa wamekutana awali Uingereza na waliendelea kuwasiliana hata baada ya Koinange kuondoka nchini humo.

Hata hivyo, kutokana na vita vya Mau Mau na kutangazwa kwa Hali ya Hatari mwaka 1952, Koinange hakuweza kurejea Kenya kwa miaka mingi.

Babake na jamaa zake wengi walikamatwa au kuwekwa vizuizini. Akiwa Uingereza, mbali na kuiwakilisha KAU, Koinange alishiriki mikutano na maandamano ya kupigania uhuru wa Afrika.

Alikutana na Kwame Nkrumah wa Gold Coast, ambaye baadaye alimpa kazi kama Mkurugenzi wa Ofisi ya Masuala ya Afrika mjini Accra kati ya 1959 na 1961 baada ya nchi hiyo kupata uhuru na kujulikana kama Ghana.

Akiwa London, aliwasiliana pia na viongozi wengine mashuhuri wa kupigania uhuru wa nchi za Afrika kama Nnamdi Azikiwe wa Nigeria, George Padmore wa Trinidad na Fenner Brockway wa Uingereza.

Nyaraka za siri za idara ya usalama ya Uingereza (MI5) zilizotolewa baadaye zinaonyesha alivyopokea barua nyingi sana kutoka kote duniani kiasi kwamba ni vigumu kuelewa aliwezaje kuzishughulikia katika enzi hiyo ambayo hakukuwa na teknolojia ya kielektroniki.

Hii inaonyesha mtandao wake mpana wa kimataifa.

Mpiganiaji uhuru Oginga Odinga, ambaye baadaye alikuwa makamu rais wa kwanza Kenya ilipopata uhuru, alimwalika Koinange kushiriki mkutano wa kwanza wa Lancaster House wa kuandaa Katiba mwaka 1960.

Alirejea Kenya mwaka 1961, akachaguliwa Mbunge wa Kiambaa mwaka 1963 na Kenyatta akamteua Waziri wa Masuala ya Afrika katika Baraza la Mawaziri la kwanza.

Baadaye alihudumu kwa muda mfupi katika wizara ya elimu kabla ya kuhamishiwa Ofisi ya Rais kama Waziri wa Nchi anayesimamia Utawala wa Mikoa kuanzia 1966 hadi kifo cha Kenyatta mwaka 1978.

Licha ya elimu na uhusiano wake, Koinange aliamini Kenyatta alikuwa na sifa bora za uongozi. Ushirika wao ulikuwa mkubwa kiasi kwamba waliitana “Ngorobi” inayomaanisha mtu mbishi.

Wengine walidai Koinange ndiye aliyekuwa na mamlaka halisi nyuma ya pazia, lakini aliyekuwa Mkuu wa Utumishi wa Umma, Geoffrey Kareithi, alipinga madai hayo.

Maisha ya Koinange yalizunguka kazi na urafiki wake na Kenyatta, hadi akasahau familia yake.

Wakati wa kifo chake, hakuwa na mali nyingi, na aliacha madeni kuliko mali. Alifariki mwaka 1981, miaka mitatu baada ya Kenyatta, akiwa na umri wa miaka 74.