Jamvi La Siasa

Kufurusha mbunge mzembe sasa kuwa rahisi

Na DAVID MWERE January 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

UTARATIBU wa kumwondoa ofisini mbunge asiyefanya kazi yake ipasavyo sasa umerahisishwa.

Kwenye sheria inayopendekezwa, bunge sasa limo mbioni kufanikisha hukumu ya Mahakama Kuu iliyotangaza sehemu za kifungu cha Sheria ya Uchaguzi kuwa kinyume cha katiba.

Mswada wa Sheria ya Uchaguzi (Marekebisho) wa 2024 ulioandaliwa na kiongozi wa wachache katika Seneti, Stewarts Madzayo (Kilifi), unalenga kufuta vifungu vya 45 na 48 vya Sheria ya Uchaguzi huku ukifanyia marekebisho kifungu cha 46 ili kutii agizo la Mahakama Kuu.

Mswada huo hata hivyo, unapendekeza kukiacha kifungu cha 47 cha Sheria kinachotoa nafasi ya kutimua wanaochaguliwa.

“‘Sheria Kuu inarekebishwa kwa kufuta vifungu vya 45 na 48,” vinasema vifungu vya 25 na 27 vya Mswada huo.Kifungu cha 104 cha katiba na kifungu cha 45 cha Sheria ya Uchaguzi, kinawapa haki wapiga kura kuwapokonya Wabunge na Maseneta viti vyao.

“Wapiga kura wana haki ya kumtimua Mbunge anayewakilisha eneobunge lao kabla ya mwisho wa muhula wa Bunge husika,” inasema ibara ya 104 ya katiba.Ibara hiyo inaendelea kuliagiza Bunge kutunga sheria itayofafanua misingi ambayo itamfanya mbunge avuliwe wadhifa wake na utaratibu wa kufuatwa.

Kifungu cha 45 cha Sheria hiyo, ambacho kilitangazwa kuwa kinyume cha katiba na Mahakama Kuu katika kesi iliyowasilishwa na Katiba Institute, kiliweka masharti ambayo chini yake mbunge anaweza kuondolewa baada ya kuchaguliwa.

Kifungu cha 48 cha Sheria hiyo kilisema kuvuliwa wadhifa wa kuchaguliwa kutakuwa halali ikiwa idadi ya wapigakura wanaokubali kufanya hivi ni angalau asilimia 50 ya jumla ya wapigakura waliojiandikisha katika kaunti au eneo bunge lililoathiriwa.

Kifungu cha 46 (1) (b) (ii) na (c) cha Sheria hiyo kilisema kwamba, ombi la kutaka kuondoa mbunge ni lazima litiwe saini na muasisi ambaye ni mpiga kura katika eneo analotaka mbunge kufurushwa.

Sheria pia ilipendekeza kwamba, ombi hilo lazima liambatane na amri ya Mahakama Kuu, na hivyo kufanya iwe vigumu kuanzisha mchakato wa kuvua mbunge wadhifa wake.

Hata hivyo, Mahakama Kuu, katika hukumu yake, ilikubaliana na Katiba Institute kwamba, wabunge hao walitunga sheria hiyo ili iwe vigumu kuwaondoa katika viti vyao, jambo ambalo ni kinyume cha Katiba.

Tangu Sheria ya Uchaguzi ianze kufanya kazi mnamo 2012, hakujawa na jaribio hata moja la kutaka kuondoa mbunge, jambo ambalo wakili David Ochami anasema wabunge walitumia sheria kujikinga. “Jambo zuri kuhusu katiba yetu ni kwamba, inatoa hatua za kuzuia maovu.

Iwapo wabunge walifikiri walikuwa wakijikinga, basi walikosea kwa sababu mahakama zipo ili kutathmini sheria wanazotunga,” asema Bw Ochami.Bw Ochami alibainisha kuwa kilichosalia ni kuhakikisha wabunge hao wanatunga sheria jinsi mahakama inavyoelekeza na kwa haraka.

“Tusichoke kuwawajibisha wabunge wetu. Kuna haja ya kuhakikisha mabadiliko wanayofanya kwa sheria yanawiana na katiba,” asema Bw Ochami.

Kifungu cha 45 cha Sheria kilichopingwa kinatoa masharti kwamba, wapiga kura katika kaunti au eneo bunge wanaweza kumvua ubunge wadhifa wake kabla ya mwisho wa muhula wa ‘Bunge husika.’

Sheria hiyo iliendelea kutaja sababu ambazo ni pamoja na iwapo mbunge atapatikana, baada ya kufuata taratibu za sheria, amekiuka uongozi na uadilifu chini ya Sura ya Sita ya katiba na iwapo atapatikana na hatia kwa kosa, kwa mujibu wa sheria ya Uchaguzi.

Hata hivyo, Wabunge waliweka katika sheria kwamba, kupokonywa wadhifa wao ‘kutaanzishwa tu baada ya hukumu au matokeo ya Mahakama Kuu kuthibitisha sababu za kufutwa,’ na hivyo kufanya iwe vigumu kuwarejesha.

Sheria hiyo ilibuniwa ili kuhakikisha mchakato huo utaanzishwa tu angalau miezi 24 baada ya uchaguzi wa mbunge na sio zaidi ya miezi 12 kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Hii ina maana kwamba, kulingana na uamuzi wa mahakama, mbunge anaweza kuvuliwa wadhifa wake na wapigakura wakati wowote ilmradi sababu hizo zinafaa na hakuna nia mbaya.

Kulikuwa pia na sharti kwamba, ombi la kuwatimua wabunge kutoka wadhifa wao halitawasilishwa dhidi ya mbunge zaidi ya mara moja katika kipindi chake.

Sheria hii iliibua hisia ikizingatiwa kuwa Magavana wa Kaunti wanaweza kutimuliwa zaidi ya mara mbili katika kipindi cha miaka mitano.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA