Maamuzi magumu ya Kalonzo akiwaniwa kama mpira wa kona kwa ajili ya 2027
KIONGOZI wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, amejipata tena katika hali tata ya kisiasa anapojiandaa ama kuwania urais au kuamua ni nani ataingia mamlakani mnamo 2027.
Leo chama chake kinatarajiwa kuandaa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC) katika bustani ya Uhuru Park, Nairobi, ambapo anatarajiwa kuidhinishwa rasmi kuwa mgombea urais wa chama hicho.
Hata hivyo, Kalonzo anakabiliwa na shinikizo kali kutoka kwa pande mbili hasimu: wapo wanaotaka aunge mkono azma ya Rais William Ruto kwa muhula wa pili, na upinzani unaomsihi aunge mkono mgombeaji mwingine wa upinzani.
Hili linamuweka kwenye njia panda kisiasa, akihitaji kuchukua hatua ya busara ili kutimiza ndoto yake bila kujitenga kisiasa.
Kalonzo, 71, aliwahi kuwa Makamu wa Rais chini ya hayati Mwai Kibaki kati ya mwaka 2008 na 2013.
Amekuwa akisisitiza kuwa 2027 ni fursa yake ya mwisho ya kuwania urais, akitaja umri wake kuwa sababu kuu. Amesema iwapo hatakuwa debeni, basi atastaafu siasa.
Katika mahojiano ya hivi karibuni, Kalonzo alisema: “Hakuna shaka kuwa nitakuwa debeni mwaka wa 2027. Mnaangalia Rais wa Sita wa Jamhuri ya Kenya. Uongozi ni wito, na nimevumilia mengi. Nafikiri wakati wangu umefika.”
Iwapo atatekeleza hilo, basi litakuwa jaribio lake la pili kuwania urais. Alijaribu mara ya kwanza mnamo 2007, ambapo alimaliza wa tatu nyuma ya Kibaki na Raila Odinga.
Baada ya mvutano wa matokeo ya kura hiyo, aliteuliwa Makamu wa Rais.
Kwenye chaguzi za 2013, 2017 na 2022, alijiondoa katika kinyang’anyiro hicho ili kumpa nafasi Bw Odinga.
Kwa sasa, Bw Odinga anaonekana kujiunga na Rais Ruto katika ushirikiano serikalini, hali inayomuweka Kalonzo katika hali tata.
Ripoti zinaashiria kuwa Odinga ni miongoni mwa wale wanaomshawishi Kalonzo kujiunga na kambi ya Ruto kwa ahadi ya cheo kikubwa serikalini na nafasi ya kuwania urais mwaka wa 2032.
Lakini wafuasi wa Kalonzo wanaamini huu ndio wakati wake wa kung’aa. Wanatumai umaarufu wake, uzoefu mkubwa serikalini, na ukarimu wake wa kisiasa alipomuunga mkono Odinga mara kadhaa, utawavutia wapigakura – hasa wale wa ODM ambao bado hawajamkubali Ruto. Kalonzo pia anaungwa kwa dhati katika ngome yake ya Ukambani.
Kulingana na washauri wake, iwapo atapata uungwaji kutoka maeneo jirani kama Mlima Kenya, atakuwa na nafasi nzuri ya kuibuka mshindi.
Prof David Monda, mchambuzi wa siasa anayeishi Amerika, anasema wafuasi wa Kalonzo wanahisi huu ndio wakati wake.
“Ukambani iko karibu na Mlima Kenya, hivyo kupata uungwaji kutoka Mlima si jambo gumu. Rigathi Gachagua tayari ameashiria kuwa yuko tayari kumuunga mkono Kalonzo.”
Wanaowania kiti hicho kutoka upinzani ni pamoja na Martha Karua, Eugene Wamalwa, Fred Matiang’i na Gachagua mwenyewe.
Hata hivyo, wafuasi wa Kalonzo wanasema ni yeye pekee anayeweza kumshinda Rais Ruto katika raundi ya kwanza.
Seneta wa Kitui, Enoch Wambua, anasisitiza kuwa Kalonzo ndiye mgombea anayefaa zaidi kuongoza Kenya, akirejelea sifa zake na tajriba yake katika uongozi wa taifa.
Naibu Gavana wa Machakos, Francis Mwangangi, naye anasema Kalonzo ana uwezo wa kuunganisha taifa, kurekebisha sekta ya elimu na afya, na kupunguza ushuru.
“Tunahitaji kiongozi atakayesikiliza wananchi, kusaidia ugatuzi na kuleta maendeleo katika maeneo yote ya nchi bila upendeleo,” alisema.
Hata hivyo, wakosoaji wake wanasema Kalonzo hana dira thabiti za sera na hata ushawishi mkubwa wa kisiasa.
Pia, suala la ufadhili wa kampeni linaonekana kama changamoto kuu kwake katika mazingira ya kisiasa ya Kenya ambapo fedha hushika usukani.
Profesa Monda anaongeza kuwa Kalonzo ana mzigo mkubwa wa kisiasa kutokana na muda wake mrefu serikalini, kuanzia enzi za chama cha KANU.
“Kizazi cha Gen Z huenda kisiwe na imani naye. Wengine wanaweza kumuona kama mwanasiasa wa zamani – aliyepitwa na wakati. Wengine humuita ‘tikitimaji’ – mtu asiyeweza kufanya maamuzi makubwa wakati wa dharura,” anasema.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa upinzani tayari wameashiria kuwa wako tayari kumuunga mkono Kalonzo kama mgombea wa urais mwaka wa 2027.
Akizungumza katika mkutano mkubwa Kitui, Naibu Rais Gachagua alisema “Wakati wa mwana wenu Kalonzo kuongoza nchi hii umefika. Amedhulumiwa kwa miaka mingi kisiasa lakini amebaki na heshima.”
Profesa Monda anahitimisha kwa kusema kuwa iwapo Kalonzo atajiondoa kutoka kambi ya upinzani na kujiunga na Ruto, au kuwania kama mgombea huru, atakuwa amebadilisha kabisa mwelekeo wa siasa za 2027.
Na iwapo ataamua kumuunga mkono mgombea mwingine, ataweza kuamua atakayetawala.