MAONI: Newton Karish aendelea kuonyesha umuhimu wa kujiamini hata unapotiliwa shaka
UKIMWONA msanii wa Benga, Newton Kariuki ‘Karish’, niombee msamaha.
Hivi umewahi kuambiwa kitu na mtu ukamjibu kimoyomoyo ‘acha uongo’? Au pengine kutokana na ustaarabu wako ukajiuliza ‘unatarajia nikuamini?’
Nimejipata katika hali hiyo mara nyingi sana, na, makinika nikupe siri yangu – ukinisemesha na badala ya kuchangia mazungumzo, niko kimya tu, ninachokupa ni tabasamu, basi jua natia dua kimyakimya ufyate ulimi, uache kunidanganya.
Hivyo ndivyo nilivyofanya takriban miaka 25 iliyopita nilipomhoji ‘Karish’ kinara wa Gangara Boys’ Band, ambaye sasa anatamba si haba kama mwanasiasa.
Siku hizo aliniambia eti alitamani sana kuwania ubunge wa Runyenjes, ila akaelewana na Bw Njeru Ndwiga, akaamua kumwachia fursa hiyo, naye akarejea kwenye sanaa kwa nia ya kujaribu tena baadaye.
Ingawa sikuwa na hakika na kauli hiyo, katika makala niliyoandika nilijumuisha sentensi moja hafifu sana kuhusu dai hilo, na nadhani mhariri wangu na akili zake razini pia alidhani hiyo ilikuwa ‘jaba’ akaiondoa! Haikutokea popote. Nilifurahi ajabu.
Nina mzio wa watu wanaojikweza, sikwambii na tabia hiyo hunisababishia upele. Na nadhani maskini Karish alielewa tu kwa kuwa alionyesha heshima na uungwana, hakuniuliza chochote. Labda hiyo ni ithibati kwamba nia haikuwa kujikweza.
Tuliendelea kuwa na uhusiano bora, kila wakati tukitaniana na kucheka sana kutokana hadithi na mbwembwe tele za msanii huyo aliyenyamazisha bendi nyingi za Benga kutoka Ukambani siku hizo.
Kutokana na historia hiyo, juzi sikushangaa hata kidogo niliposikia kuwa Karish, maarufu zaidi kaskazini mashariki mwa nchi, ameteuliwa kuwania ubunge wa Mbeere Kaskazini.
Ndoto yake inaelekea kutimia, lakini katika mazingira tofauti na yale niliyodhania mwanzoni, ya motokaa kujikanyaga mafuta kwenye mlima.
Kumbe mimi na mhariri wangu hatukutambua moyo wake wa kuijituma?
Ona, Karish anateuliwa kuwania ubunge ilhali tayari anahudumu muhula wake wa tatu kama mwakilishi wa wadi ya Muminji – amechaguliwa tangu mwaka 2013.
Kwani mambo huendaje? Unataka kuniambia mwenyekiti matata wa chama cha Democratic Party (DP) na aliyekuwa Spika wa Bunge la Kitaifa, Justin Muturi, ametafuta mtu mwingine wa kumpa fursa hiyo akakosa?
Sina ubaya na Karish, lakini mbona apewe fursa ya kuwania ubunge ilhali ana kazi tayari? Kumbe shilingi inajua kwao, lazima ifuate ndugu zake waliko?
Si siri, anatosha mboga. Naamini angechaguliwa mbunge kitambo, lakini wakati wake haukuwadia. Sina hakika ndio huu, lakini kuna uwezekano mkubwa sana kwamba atachaguliwa katika uchaguzi mdogo unaokuja. Umaarufu katika sanaa na siasa ni wasifu tosha.
Natamani kuwa kama Karish, kujituma kikweli hata usiponiamini. Tutakutana huko mbele ndoto zangu zikitimia, nikucheke kidogo kisha nikununulie kopo la uji wa mgando. Ipo siku.
mutua_muema@yahoo.com