Jamvi La Siasa

Marais wa Afrika kuchagua mwenyekiti wa AUC leo

Na CECIL ODONGO, DUNCAN KHAEMBA February 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

RAILA Odinga, mwanasiasa jasiri ambaye amegombea urais kwa miaka mingi Kenya, kwa mara nyingine amedhihirisha hulka yake kama kigogo asiyeogopa kutafuta wadhifa wowote, wakati wowote na mahali popote.

Na sasa, analenga cheo cha hadhi kuu barani-uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) katika uchaguzi unaofanyika leo Addis Ababa, Ethiopia.

Kwa muda wa miezi kumi na miwili iliyopita, Odinga amezunguka bara zima, akiomba kura kutoka kwa wakuu mbalimbali wa nchi na serikali ambao watakuwa waamuzi ya mwisho leo, Februari 15, 2025, uchaguzi utakapofanyika.

“Niko hapa kama simba wa Afrika. Nimekuwa nikilala katika misitu ya Congo, lakini sasa nimeamka!” lilikuwa tamko la kijasiri na la kishujaa la Odinga alipozinduliwa rasmi kuwa mgombeaji wa Kenya wa uenyekiti wa AUC.

Mnamo 2017, Kenya ilimteua Balozi Amina Mohamed kwa wadhifa huo lakini hakufaulu. Wakati huu, nchi inaamini ni wakati wake wakiweka matumaini kwa uzoefu wa Bw Odinga.

Sekretarieti ya kampeni ya Odinga kwa wadhifa huo, inayojumuisha wajumbe kutoka kanda zote tano za AU, inaongozwa na Katibu Mkuu wa Masuala ya Nje wa Kenya Korir Sing’Oei na Balozi Elkana Odembo..

Kwa waziri mkuu huyo wa zamani, leo ni siku muhimu katika maisha yake marefu ya kisiasa. Iwapo atanyakua kiti hicho, atakuwa amefanikiwa pakubwa huku akijiandaa kuondoka kwenye jukwaa la siasa baada ya miongo minne.

Kura hiyo itafanyika kuanzia saa sita mchana jijini Addis Ababa. Bw Odinga anamenyana na wapinzani wake wawili; Waziri wa Masuala ya Nje wa Djibouti Mahmoud Ali Youssouf wa Djibouti na aliyekuwa waziri wa masuala ya nje wa Madagascar, Richard Randriamandrato.

Watatu hao watakuwa wakilenga kurithi nafasi ambayo inashikiliwa na Moussa Faki, raia wa Chad ambaye amehudumu kwa mihula miwili.

Kando na mwenyekiti wa AUC, Marais pia watakuwa na fursa ya kuwachagua naibu mwenyekiti na makamishina wanane ambao watakuwa wakihudumu kwa muhula wa miaka minne kabla ya kujitokeza kuchaguliwa tena.

Mshindi wa AUC atalazimika kupata thuluthi mbili ya kura na iwapo hilo halifanyika hadi raundi ya tatu, mwaniaji ambaye atamaliza katika nafasi ya tatu atajiondoa.Kutakuwa na duru ya pili ya kura ambayo itashirikisha mwaniaji atakayemaliza wa kwanza na wa pili.

Kura hiyo ikiisha baada ya raundi ya tatu bila yeyote kupata thuluthi mbili za kura, atakayemaliza wa kwanza atatangazwa mshindi. Kwenye uchaguzi wa leo, Bw Odinga, na wapinzani wake watalazimika kupata kura kutoka mataifa 33 kuwahi ushindi wa moja kwa moja.

Niger, Mali, Guinea, Gabon, Burkina Faso na Sudan hazitashiriki uchaguzi huo kwa sababu zimepigwa marufuku kutokana na kuwa chini ya uongozi ambao ulitokana na mapinduzi ya kijeshi.

Viongozi nchini wakiongozwa na Rais William Ruto, Kinara wa Mawaziri, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua ni miongoni mwa waliomtakia heri Bw Odinga.

“Raila Odinga ndiye bora zaidi kwa wadhifa wa AUC barani Afrika. Sina shaka kuwa Raila ataendeleza ajenda ya Afrika na atasaidia kuunganisha mataifa yanayozungumza Kiingereza na Kifaransa,” akasema Bw Gachagua.

“Ushindi wake Afrika utahakikisha anaendeleza ndoto yake ya kubadilisha bara hili. Ushindi wake utakuwa ushindi kwa Kenya na bara zima,” akaongeza Bw Gachagua kwenye mtandao wake wa X.

Wabunge 100, maseneta na magavana ni miongoni mwa marafiki wa waziri huyo mkuu wa zamani walio Addis Ababa.Jijini Nairobi, katika bustani ya Jevanjee, makundi ya vijana yamekuwa yakidadavua jinsi kura itakavyopigwa huku wakibashiri ushindi wa Raila.

Katika ngome ya Nyanza, Pwani, Kisii na Magharibi, wengi pia wamekuwa wakitarajia ushindi wa Raila.Makundi yanayounga Raila yamepanga kusherehekea ushindi wake kwa kuandaa tafrija katika mikahawa na maeneo ya burudani na umma kumwombea.Usiku wa kuamkia leo, mamia walikesha na maombi makubwa kuandaliwa makanisani katika ngome za Raila huku dua yao ikiwa ni ‘Agwambo’ afanikiwe mara hii.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati hata hivyo, anasema kuwa huenda mambo yatakuwa magumu sana kwa Bw Odinga hasa baada ya mataifa ya kusini mwa Afrika (SADC) kutangaza kuwa yatamuunga mkono Bw Randriamandrato.

“Sisi tumewajaza watu huko na kampeni yetu imekuwa ya mayowe. Baada ya tangazo la SADC haitashangaza iwapo Raila atakosa hata kura ya Tanzania,” akasema Bw Andati.“Hata wakati wa Amina aliwania, Tanzania, Uganda na Burundi zilibadilisha nia na kukosa kumpigia Amina kura kwenye raundi ya mwisho,” akaongeza.

Bw Andati anasema kelele na kuangaziwa kwa kampeni za Raila hakumaanishi ameshinda kiti hicho jinsi ambavyo umma nchini umelazimika kuamini.“Mwaniaji wa Djibouti ni mwanadiplomasia, aliendesha kampeni zake kimya kimya na hata ameenda Addis Ababa na ujumbe wa watu wachache. Raila ana kibarua,” akasema.

Mchanganuzi mwingine Javas Bigambo naye anasema matokeo ya leo yataonyesha iwapo wanaheshimu uhusiano na utawala wa Rais Ruto.

“Matokeo haya, yawe ya ushindi au ya kupoteza yataonyesha jinsi uongozi wa Kenya unaheshimiwa Afrika ua kuchukiwa,” akasema Bw Bigambo.Alikiri kuwa jinsi ambavyo mambo yalivyo Addis Ababa, kwa sasa hakuna uhakika wowote kuhusu ushindi wa Bw Odinga.