Jamvi La Siasa

Mashambulizi dhidi ya Gachagua yameibua maswali 8 tata: Haya hapa majibu yake

Na MWANGI MUIRURI January 28th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

MASHAMBULIZI ya mara kwa mara dhidi ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, yanayodaiwa kutekelezwa kwa ushirikiano wa maafisa wa polisi wanaopotoka na magenge ya wahuni, yameibua maswali mazito kuhusu siasa na maadili nchini.

Aliyekuwa afisa wa utawala, Bw Joseph Kaguthi, aliambia Taifa Leo kuwa kuelewa mashambulizi hayo ambayo yamedumu kwa zaidi ya mwaka mmoja na yanaonyesha dalili zilezile za polisi kufanya kazi bega kwa bega na wahalifu, kunahitaji kurejelea maneno ya aliyekuwa Rais Daniel arap Moi.

“Rais Moi alikuwa akituambia kwamba iwapo kuna jambo la uhalifu linaloendelea licha ya kilio cha umma, basi ujue kuna mtu au watu walio karibu sana na mamlaka walio nyuma yake,” alisema Bw Kaguthi.

Kwa mujibu wake, hali hiyo imeibua maswali nane muhimu yanayohitaji majibu ya wazi.

Kwa nini Gachagua?
Bw Gachagua, aliyeng’olewa madarakani Oktoba 2024, ameibuka tena kisiasa kwa kasi ambayo haikutarajiwa. Baada ya kutabiriwa “kuisha kisiasa” na wapinzani wake, amefanikiwa kuunda chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) na ndani ya miezi saba akashinda chaguzi ndogo katika Kariobangi, Kisa East na Narok Town.

Aidha, amejijengea ushawishi mkubwa katika Mlima Kenya na kuunda muungano mpana wa upinzani unaojumuisha Kalonzo Musyoka, Eugene Wamalwa, George Natembeya na Seneta Kenar Seki. Hatua hiyo imemfanya kuwa tishio kubwa kwa mamlaka kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Kwa nini Mlima Kenya?
Mlima Kenya ni kitovu cha siasa za Gachagua, eneo alilosaidia Rais William Ruto kupata asilimia 87 ya kura mwaka 2022. Amefanikiwa pia kuwaunganisha vigogo wa eneo hilo akiwemo Mithika Linturi, Justin Muturi na Martha Karua. Wachambuzi wanasema eneo lolote analotembelea Gachagua hubadilika ghafla na kuwa ngome yake ya kisiasa.

Je, ni Mlima Kenya dhidi ya Mlima Kenya?
Mchambuzi wa siasa Profesa Macharia Munene anasema Gachagua anaweza kupingwa kikamilifu tu na watu wanaoelewa siasa za Mlima Kenya na wanaohofia kupoteza endapo umaarufu wake utaendelea kukua. Anaonya kuwa endapo busara haitatumika, jamii inaweza kugawanyika vibaya kwa misingi ya tamaa ya kisiasa.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Gikuyu Wachira Kiago, alikiri kuwa wanajua wanaopigana ni nani, akionya kuwa mashambulizi dhidi ya wanawake, watoto, wazee na hata maeneo ya ibada ni kichaa kisiasa kisichokubalika.

Nini kinapiganiwa?
Kwa mujibu wa mtaalamu wa siasa Gasper Odhiambo, kinachopiganiwa ni kura na mamlaka. Mlima Kenya una idadi ya kura inayoweza kuamua urais, naibu wa rais na hata nusu ya serikali. Ndani ya eneo hilo kuna makundi yanayomuunga mkono Rais Ruto, Gachagua na mvutano wa chini kwa chini unaomhusisha Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Nani anafaidika?
Gachagua mwenyewe anasema mashambulizi yanamjengea umaarufu. “Yanalenga kunitisha na kunizuia kuunganisha watu wangu. Kama kuondolewa serikalini hakukunimaliza, vurugu hizi hazitanimaliza,” alisema Januari 25, 2026. Alikiri kuwepo kwa magenge ya kulipwa, maafisa wa polisi waliopotoka na wafadhili wa vurugu wanaonufaika kifedha.

Nani anapoteza?
Mchambuzi Festus Wangwe anaona Rais Ruto ndiye anayepoteza zaidi. “Hawezi kunufaika kuongoza nchi inayoonekana kusimamiwa kwa vurugu,” alisema, akionya kuhusu athari za kimataifa na kumbukumbu za ICC.

Itamalizikaje?
Mchanganuzi wa siasa Mixson Gitau anasema Rais Ruto ana chaguo mbili: kuvaa kofia ya kampeni au taji la mamlaka. Anamtaka Rais atoe tamko la hadharani kupinga vurugu, awawajibishe wanaohusika na kuonya maafisa wa usalama.

Je, itaathiri 2027?
Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya anaonya kuwa vurugu huwa na tabia ya kujirudia kwa wale wanaozianzisha.