• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 5:50 AM
Masharti ya Agikuyu kumkubali Gachagua kuwa msemaji wao

Masharti ya Agikuyu kumkubali Gachagua kuwa msemaji wao

NA MWANGI MUIRURI 

NAIBU Rais Rigathi Gachagua amekuwa akitatizika kuafikia lengo lake la kuwa msemaji wa eneo la Mlima Kenya licha ya kuwa msaidizi wa Rais William Ruto kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.

Katika mbinu zake kadha za kujaribu kukubalika, amekuwa akiandaa mikutano ya wadau akiwarai wamuunge mkono, lakini matokeo yakiwa ni kuzuka kwa pingamizi zaidi kutoka hata kwa wanasiasa limbukeni.

Mrengo huo wa mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro tayari umependekeza Bw Gachagua atemwe 2027 na asiwe mrithi wa ikulu 2032.

Kilele cha mikutano hiyo ya Bw Gachagua ya kujinusuru kinatazamiwa kuwa cha kumsaka Rais mstaafu Uhuru Kenyatta ili waridhiane baada ya mwaka mzima wa siasa za washirika wa Bw Gachagua kumshambulia kwa cheche za maneno.

Katika harakati hizo, Bw Gachagua ametangaza kwamba anasaka kikao na wazee wa kijamii ndio wawe daraja la kumleta pamoja na Bw Kenyatta ambaye kwa sasa ndiye anatambulika kitamaduni kuwa msemaji wa kisiasa Mlimani.

“Ni ukweli kwamba ninamtafuta Bw Kenyatta kwa kuwa yeye ni kiongozi wetu na ni ndugu yetu. Mimi nimetoa amri kwamba washirika wangu wasiwe wakimrushia cheche za maneno,” akasema Bw Gachagua katika mazishi ya aliyekuwa mkuu wa polisi wa Nairobi na Mombasa, Bw King’ori Mwangi.

Jumapili iliyopita akiwa katika kituo cha TV cha Inooro, Bw Gachagua alisema kwamba atakutana na wazee wa jamii ya Agikuyu ili kupalilia umoja.

Mnamo Alhamisi, mwenyekiti wa baraza hilo Bw Wachira Kiago alilitoa masharti ya kukutana na Bw Gachagua.

“Ni lazima kwanza tuwe na amani ya kimaongezi. Tusiwe wa kusaka amani huku kando bado tunarushiana cheche za maneno,” akasema Bw Kiago.

Alisema Bw Gachagua akiwa katika mahojiano hayo ya runinga aliwadunisha wazee kwa kuwataja kama walevi ambao hawawezi wakaaminiwa upishi wa mvinyo wa kijamii.

“Hawa wazee hawawezi wakaaminiwa kungojea pombe ya kitamaduni ya Muratina iive kwa siku tano. Wataweka kemikali hata za mochari ili iive haraka wakunywe,” akasema Gachagua.

Aidha, Bw Kiago alisema kwamba ni lazima hafla za kitamaduni za wazee hao ziwe zikipigwa msasa wa polisi ili kupambana na upenyo wa kundi haramu la Mungiki.

Bw Kiago alisema sharti lingine la kukubali mkutano na Bw Gachagua ni kuondolewa kwa mwelekeo huo wa polisi kushirikishwa utamaduni wa Agikuyu.

“Sharti lingine ni kwa serikali ilipe vyombo vya habari pesa za matangazo ya kibiashara. Kukataa kulipa madeni hayo ni sawa na kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari na kulemaza juhudi za kuwa macho na sauti ya kijamii,” akasema Bw Kiago.

Bw Kiago alisema baraza hilo limekuwa likifuatilua ripoti za serikali kutoa marufuku ya kuvipa vyombo kadha matangazo ya kibiashara kwa nia ya kuangamiza uwezo wao wa kutekeleza majukumu yao.

Bw Kiago aliongeza kwamba ni lazima serikali itafakari upya baadhi ya mikakati yake ambayo inazua kupotea kwa ajira.

“Vita vinavyoendelezwa Mlima Kenya kwa sasa dhidi ya baa vinasababisha kupotea kwa ajira. Baa sio pahala pekee ambapo pombe huuzwa na tena mbali na vileo huko riziki mbalimbali hunawiri baa zikihudumu,” akasema Bw Kiago.

Hata hivyo, alisema kwamba baraza hilo linaunga mkono kikamilifu vita dhidi ya mihadarati na pombe ya mauti.

Bw Kiago alisema kwamba kwa sasa msemaji wa jamii hiyo kisiasa ni Bw Kenyatta kwa kuwa hakuna hafla ambayo imeandaliwa ya kumpa  mwingine mbadala vifaa vya kitamaduni vya kumtambua kuwa mrithi.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Mnatoza ushuru na hamlipi madaktari, Kalonzo aishangaa...

Si lazima ujengewe nyumba ‘ushago’, mke wa pasta...

T L