Jamvi La Siasa

Masimba jike watatu kura ya 2027 ikinukia

Na BENSON MATHEKA September 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

Huku uchaguzi mkuu wa 2027 ukikaribia nchini Kenya, ni wanawake watatu pekee wanaooneka kuchangamkia siasa za kitaifa kwa wakati huu.

Wanaoonyesha uthabiti, ujasiri, na weledi wa kisiasa wa hali ya juu ni mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba, kiongozi wa chama cha Peoples Liberation Party Martha Karua, na Gavana wa Homa Bay ambaye ni Mwenyekiti wa chama cha ODM Gladys Wanga.

Wachanganuzi wa siasa wanasema wanawake hao watatu wamejitokeza kwa ujasiri kuwa na ushawishi mkubwa katika mustakabali wa siasa za taifa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 huku wakipamba mirengo mitatu inayotamba kwa sasa: upinzani ulioungana, Kenya Moja na Serikali Jumuishi.

Wamuchomba, ameibuka kama mmoja wa wanawake jasiri zaidi ndani na nje ya Bunge la Kitaifa. Japo alichaguliwa kwa tiketi ya Muungano wa Kenya Kwanza, Wamuchomba hajakuwa na woga wa kukosoa baadhi ya sera za serikali, hasa zile zinazoathiri maisha ya kila siku ya Wakenya wa kawaida – kama vile ushuru, gharama ya maisha, na masuala ya kilimo.

Anapendwa na wengi kwa ujasiri wake wa kuzungumza ukweli, na kwa msimamo wake wa kushikilia maslahi ya wananchi kuliko maslahi ya chama au vyama.“Wamuchomba ameonyesha kuwa mwanamke anaweza kuwa sauti ya uongozi wenye maono na uadilifu hata ndani ya mazingira yenye shinikizo za kisiasa,” asema mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki.

Wakati siasa za Mlima Kenya zinaonekana kupitia kipindi cha mabadiliko, Wamuchomba anajitokeza kama mmoja wa wanaoweza kuelekeza mjadala wa kisiasa katika mwelekeo mpya kuelekea 2027.

Mbunge wa Githunguri, Bi Gathoni Wamuchomba. PICHA|MAKTABA

Kwa sasa, Wamuchoma ni mwanamke wa pekee katika mrengo ibuka wa Kenya Moja unaoleta pamoja wabunge vijana kutoka vyama tofauti na miungano tofauti ya kisiasa nchini.Wanachama wengine wa Kenya Moja ni katibu mkuu wa ODM Edwin Sifuna.

Mbunge wa Kabuchai Majimbo Kalasinga, Jack Wamboka (Bumula), Joshua Kimilu (Kaiti) na Mbunge wa Kitutu Masaba Clive Gisairo (ODM).Martha Karua, aliyewahi kuwa Waziri wa Haki na baadaye mgombea mwenza wa Raila Odinga katika uchaguzi wa 2022, ni miongoni mwa wanasiasa wa kike waliodumu kwa muda mrefu kwenye siasa za kitaifa.

Hadi leo, Karua anaendelea kuwa mfano bora wa mwanamke anayesimamia misingi ya sheria, haki za binadamu na utawala bora.Licha ya kuwa amekuwa kimya kiasi baada ya uchaguzi uliopita, Karua bado ni sauti muhimu ndani ya upinzani na kwa wadau wa mageuzi ya kidemokrasia.

Uaminifu wake kwa maadili ya kikatiba unamfanya kuwa hazina ya kisiasa ambayo inaweza kuamsha ari mpya kuelekea 2027.“Wanawake vijana na viongozi chipukizi wanamtazama Karua kama mfano wa mwanamke asiyelegea na asiyeuza misimamo yake kwa manufaa ya kisiasa – sifa ambayo ni adimu katika siasa za sasa,” asema Dkt Gichuki.

Kwa sasa, Karua ndiye mwanamke wa pekee katika upinzani unaosuka muungano wa kumenyana na Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027. Wengine katika muungano huo ni Kalonzo Musyoka wa Wiper, Rigathi Gachagua wa DCP, Fred Matiang’i na Eugene Wamalwa wa DAP- Kenya na Justin Muturi wa Democratic Party (DP).Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga ni mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kama gavana katika eneo la Nyanza.

Mafanikio yake katika siasa hayajatokana tu na nafasi alizopewa, bali pia kutokana na uwezo wake wa kuongoza, kusimamia maendeleo, na kujenga miungano ya kisias

a.Tangu achaguliwe kama gavana, Wanga ameonyesha uwezo mkubwa wa kiutawala, akijikita katika kuboresha huduma za afya, uwezeshaji wa wanawake na vijana, pamoja na kudumisha uwazi katika matumizi ya fedha za umma.

Hii imemfanya apate heshima hata nje ya Homa Bay na kuanza kuonekana kama sura inayoweza kuchukua nafasi kubwa zaidi katika siasa za kitaifa.Kuchaguliwa kwake kuwa mwenyekiti wa ODM kulimweka katika nafasi nzuri ya kuhusika na siasa za kitaifa.

Huku muungano kati ya ODM na UDA hasa baada ya Serikali Jumuishi kuelekea 2027 ukinukia, Wanga ana nafasi ya kutekeleza jukumu muhimu. Amekuwa akitetea kwa nguvu ukuruba wa kiongozi wa chama hicho Raila Odinga na Rais William Ruto.

“Wamuchomba, Karua na Wanga ni mfano kwamba wanawake wanaweza kuchukua misimamo thabiti na kuwa nguzo muhimu katika mjadala wa mabadiliko ya kitaifa. Huku wakiwa na mitazamo tofauti ya kisiasa, wote watatu wana kitu kimoja cha pamoja kwamba wanawake wanaweza kuwika kisiasa,” asisitiza Dkt Gichuki.

Anasema kama uchaguzi wa 2027 utakuwa na mwelekeo wa kweli wa mageuzi, basi wanawake hawa – na wengine wanaofata nyayo zao – watakuwa na nafasi kubwa katika kuunda sura mpya ya uongozi wa kisiasa.

“ Wanaonyesha kuwa wanawake hawafai kusubiri jamii na vyama vya siasa kuwapa nafasi zaidi, kwamba wanawake si kama mapambo ya kisiasa, bali ni viongozi halisi wanaoweza kubeba taifa mbele kwa maadili, maono, na matendo,” asema.