• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 11:30 AM
Matamshi ya Uhuru kuhusu usaliti ishara angali na machungu ya 2022

Matamshi ya Uhuru kuhusu usaliti ishara angali na machungu ya 2022

KAULI ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kwamba ulingo wa siasa umesheheni wasaliti imetajwa kama ishara kwamba bado anapania kushawishi siasa za taifa hili kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Kwa kuwashambulia, kwa maneno, wanasiasa kama hao, wadadisi wanasema, Bw Kenyatta ameonyesha kuwa hayuko tayari kuridhiana na baadhi ya viongozi aliowasaidia lakini wakamgeuka kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa 2022.

“Uhuru ameonyesha dalili kwamba bado anapania kuendelea kuwa na usemi fulani katika siasa za taifa hili licha ya kwamba amestaafu. Anaonekana kama mtu ambaye bado ni mwenye hasira kuu haswa kufuatia matukio ya baada ya uchaguzi mkuu 2022, ambapo wengi wa wandani walimtelekeza na kujiunga na mrengo wa Kenya Kwanza,” anasema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Reuben Nasibo.

Gachagua

Kulingana na Profesa Nasibo, ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Amerika (USIU)-Nairobi, kauli ya Bw Kenyatta pia sio habari njema kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua ambaye anapania kuridhiana na familia yake.

“Juhudi za Gachagua za kutaka kufanya maridhiano na familia ya Kenyatta huenda zisifanikiwe hivi ikiwa hisia kama zile ambazo rais mstaafu alidhihirisha juzi bado zinamsonga,” anaeleza.

Kulingana na msomi huyo, wakati kama huu ambapo joto la siasa za kampeni za uchaguzi mkuu zimetulia, Bw Kenyatta alipaswa kuonekana akitoa kauli zinazopalilia umoja katika ulingo wa siasa bali sio utengano.

Shambulia vikali

Akiongea Jumamosi iliyopita, alipohudhuria hafla ya kutawazwa kwa maaskofu wasaidizi wa Kanisa Katoliki, Simon Peter Kamomoe na Wallace Ng’ang’a Gachihi, Bw Kenyatta aliwashambulia vikali wanasiasa ambao aliwataja kama “wasaliti”.

“Askofu ameongea kuhusu wasaliti kanisani, lakini ninataka kusema kuwa siwaoni wasaliti kanisani. Usaliti uko upande ule mwingine (akielekeza kidole upande walikoketi wanasiasa),” akasema.

Hafla hiyo ilifanyika katika uwanja wa Kanisa Katoliki la St Mary’s Msongari, jijini Nairobi.

Miongoni mwa wanasiasa waliohudhuria sherehe hiyo walikuwa Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja, Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na wabunge Beatrice Elachi (Dagoretti Kaskazini) na Timothy Wanyonyi (Westlands).

Pia walikuwepo maafisa wa serikali kama vile; Jaji Mkuu Martha Koome na mawaziri Moses Kuria (Utumishi wa Umma) na Susan Nakhumicha (Afya).

“Kwa wasaliti, ninataka kuwaambia kuwa hata Judas (Iscariot) alimsaliti Yesu, lakini baadaye aliacha pesa alizopewa na akajitia kitanzi. Kila kitu kina mwisho,” Bw Kenyatta akaongeza.

Rais huyo mstaafu aliendelea kusema ni makosa kwa watu kudhani kuwa uongozi ni “nafasi yao kuwahangaisha walio chini yao.”

“Lakini jinsi Askofu ametukumbusha leo (Jumamosi, Aprili 7, 2024) kazi ya kiongozi sio kuamuru bali ni kuelekeza, kuongoza na kuwashirikisha watu wote,” Bw Kenyatta akaeleza.

Wasaliti wenyewe

Baadhi ya wanasiasa ambao inasemekana walimsaliti Bw Kenyatta ni wabunge 26 kati ya 28 waliochaguliwa kwa tiketi ya chama chake cha Jubilee lakini sasa wanashirikiana, kisiasa na mrengo wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Rais William Ruto.

Tangu mwaka jana, wabunge hao wakiongozwa na Mbunge Maalum Sabina Chege wamekuwa wakiendesha kampeni ya kumtimua Bw Kenyatta kama kiongozi wa Jubilee.

Hata hivyo, kampeni hizo ambazo zinaonekana kupigwa jeki na serikali ya Rais Ruto, zimekwamishwa na hatua ya mrengo wa Bw Kenyatta kuwasilisha kesi kortini.

Wanasiasa wengine ambao inadaiwa wamemsaliti rais Rais Ruto mwenyewe, naibu wake Bw Gachagua ni viongozi mbalimbali walioko serikalini.

  • Tags

You can share this post!

Baada ya msoto, Colonel Moustapha atamani kurudi soko,...

Rotterdam Marathon, mbio alizosubiria kwa hamu kubwa Kiptum...

T L