Jamvi La Siasa

Matiang’i afichua atakavyomenyana na Ruto kuwania Ikulu

Na JUSTUS OCHIENG’, WYCLIFFE NYABERI August 31st, 2025 Kusoma ni dakika: 3

ALIYEKUWA Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, ameanza kuandaa mkakati wa kisiasa wa kuwania urais mwaka wa 2027 kimyakimya lakini kwa kina kupambana na Rais William Ruto huku akichanganya ahadi za sera, mikakati ya miungano na ujumbe wa mageuzi.

Matiang’i ambaye kwa muda mrefu amekuwa kimya kwenye siasa, alijitokeza tena hivi majuzi akisema kuwa Kenya inahitaji ukombozi kutoka kwa kile anachotaja kama utawala uliofeli.

Waziri  huyo aliyekuwa na ushawishi mkubwa katika serikali ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, sasa anajiwasilisha kama mzalendo, anayelenga mabadiliko, mwenye tajriba, busara na mitandao ya kutosha kuokoa nchi.

Akizungumza katika mazishi kijijini Nyasore, eneobunge la Kitutu Masaba, Kaunti ya Nyamira, Ijumaa iliyopita, Dkt Matiang’i alitoa shutuma kali zaidi dhidi ya serikali ya Rais Ruto, akisema kuwa imejaa ufisadi, utepetevu wa kiutawala na vipaumbele visivyolenga mwananchi.

“Tunachoshuhudia si kingine ila ulafi usio na aibu na uporaji wa rasilmali. Kuna mtu anayeelekeza taifa kuporomoka” alisema, akiwataka Wakenya kujiandaa kwa mabadiliko ya uongozi ifikapo mwaka wa 2027.

Lakini chini ya maneno yake makali, kuna mpango wa kitaalamu na wa kimkakati.

Mikutano ya vyama, kamati za siri za kiufundi, na juhudi za kuwafikia wananchi mashinani zinadhihirisha kuwa Matiang’i si mkosoaji wa serikali tu, bali pia ana mikakati ya kuelekea Ikulu.

Kwa mujibu wa wasaidizi wake, ajenda yake kuu inajikita kwenye nguzo tatu: kurejesha uadilifu serikalini, kufufua uchumi wa taifa, na kuwekeza kwa watu kupitia elimu, afya na ajira.

Akiwa maarufu kwa utendakazi wake uliojaa nidhamu alipokuwa serikalini, Matiang’i ameahidi kukomesha ufisadi serikalini.

Anasema atamaliza “wazimu wa uporaji wa mali ya umma” na kuleta tofauti kati ya uongozi wake wa kiufundi chini ya Rais Kenyatta na kile anachokiita “utamaduni wa wizi” katika serikali ya Kenya Kwanza.

Katika kipindi hiki ambapo Wakenya wanalalamikia ushuru wa juu na deni la taifa linalozidi kuongezeka, Matiang’i ameahidi mkataba wa kiuchumi kwa wananchi  anaoita “Dira ya Kiuchumi ya Wakenya” – ambao unalenga kupunguza deni, kuzuia ubadhirifu na kuimarisha viwanda vya ndani.

Kama Waziri wa Elimu wa zamani, ameahidi kufanyia mabadiliko mfumo wa elimu anaosema “umevurugika” na kuimarisha Hazina Bima ya Afya ya Jamii (SHIF) ambayo ameitaja kuwa “mpango mzuri uliogeuka kuwa utapeli.”

Katika kampeni yake, amekuwa akiwahimiza vijana wajitokeze kujiandikisha kama wapiga kura, akisema wao ndio msingi wa mabadiliko ya kweli. Timu yake inatengeneza sera zinazolenga vijana kupitia ajira, teknolojia ya kidijitali na vituo vya ubunifu.

Akitumia mizizi yake ya Kisii lakini akilenga kujenga daraja la kisiasa kitaifa, Matiang’i anasema uongozi wa Kenya unahitaji “nidhamu, mpangilio na hadhi.”

Tayari kampeni yake inashika kasi. Mnamo Agosti 21, aliongoza mkutano wa viongozi wa vyama sita vya UPA, Jubilee, DEP (Bus), PDP, KSC na PNU ambapo walijadili uwezekano wa kuunda chama cha pamoja au muungano mpya kwa uchaguzi wa 2027. Kamati ya kiufundi iliundwa kuchunguza mwelekeo bora.

Ripoti pia zinaonyesha kwamba Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta anaweza kujiuzulu kama kiongozi wa chama cha Jubilee kumpa nafasi Matiang’i wakati wa Mkutano wa Kitaifa wa Wajumbe (NDC).

Matiang’i ameamua kuiga mtindo wa “Hasla” aliotumia Rais Ruto  2022 kwa kuandaa mikutano midogo mashinani badala ya mikutano mikubwa, jambo linalosaidia kuwasiliana moja kwa moja na wananchi.

“Wanaouliza kwa nini niko kimya na si kwenye kampeni, waambie najua ninachofanya. Nitawashangaza,” alisema alipokuwa Nyamira.

Pia anatumia sifa yake kama mtaalamu mwenye nidhamu kuendesha kampeni inayoangazia hoja badala ya matusi.

Kazi yake katika Benki ya Dunia pia imempa mitandao ya kimataifa, na kuvutia wawekezaji wanamsawiri kama mbadala thabiti kwa Ruto na vinara wengine wa upinzani.

Kwa sasa, anashirikiana na vyama vingine vya upinzani – ikiwa ni pamoja na DCP ya Gachagua, Wiper ya Kalonzo, PLP ya Martha Karua, DAP-K ya Eugene Wamalwa, Jubilee ya Uhuru Kenyatta, DP ya Justin Muturi, na vyama vya ukanda wa Kisii.

Hata hivyo, mchakato wa kuunda muungano unakabiliwa na changamoto. Mvutano mkubwa ni kuhusu nani anafaa kuwa mgombea urais.

Jubilee ya Uhuru imemtaja Matiang’i kuwa chaguo lao, lakini Gachagua anamuunga mkono Kalonzo. Baadhi ya wanachama wa Wiper wanamtazama Matiang’i kama “mradi wa Uhuru” nembo ambayo amekana vikali.

Wengine kama Gachagua wamemtaka Matiang’i kuunda chama chenye mizizi ya Kisii badala ya kutegemea Jubilee, wakisema kila mgombea wa kweli anapaswa kuwa na msingi wa nyumbani.

Changamoto nyingine ni ushindani wa kisiasa miongoni mwa vyama vinavyoshirikiana naye – ikiwemo PLP, Tawe Movement ya Natembeya, na mvutano kati ya Uhuru na Gachagua kuhusu udhibiti wa miundo ya upinzani.

Licha ya hayo yote, vyama vya upinzani vinakubaliana kwa kauli moja kwamba Rais Ruto anapaswa kushindwa 2027.