Matumaini upinzani utaungana Ruto akikaa ng’ang’ari
Kuna dalili kwamba upinzani nchini utaungana kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027, baada ya chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) kuachia Democratic Action Party of Kenya (DAP–Kenya) nafasi ya kugombea ubunge katika uchaguzi mdogo wa Malava unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2025.
Uamuzi huo ulitangazwa rasmi na Naibu Kiongozi wa DCP, Cleophas Malala, katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na maelfu ya wakazi wa Malava. Mkutano huo ulihudhuriwa pia na mgombea wa DCP, Edgar Busiega, ambaye alitangaza kujiondoa kwenye kinyang’anyiro na kumuunga mkono mgombea wa DAP–Kenya, Seth Panyako.
“Tumekubaliana kwamba katika orodha ya uteuzi ya wabunge wa chama cha DCP, Edgar Busiega atakuwa wa kwanza kuteuliwa. Hii ni ishara ya heshima kwa wale wanaoweka maslahi ya umoja juu ya ubinafsi,” alisema Malala huku umati ukishangilia.
Busiega, ambaye amekuwa akizunguka eneo la Malava akitafuta uungwaji mkono, alisema aliamua kujiondoa “kwa hiari kamili” ili kudumisha umoja wa upinzani na kuhakikisha kura hazigawanyiki. Hatua hiyo ilijiri baada ya kikao cha faragha kati ya Malala na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, kilichoafikia umuhimu wa chama hicho kumpa nafasi Panyako.
Seneta wa Kakamega, Boni Khalwale, alisifu hatua hiyo akisema, “Hongera kwa Team Busiega kwa kujiunga na ndoto kubwa na kusimama upande sahihi wa historia kwa kumuunga mkono Seth Panyako. Huu ndio mwelekeo sahihi wa upinzani — umoja badala ya ushindani wa ndani.”
Khalwale, ambaye licha ya kuwa Seneta wa chama tawala cha UDA, amekuwa akimpigia debe Panyako wa DAP–Kenya, alisema kura za Malava ni kipimo cha umoja wa wapinzani dhidi ya serikali ya Kenya Kwanza.
Kwa wakati huu, Muungano wa Upinzani umeleta pamoja Gachagua wa DCP, Jubilee ya Uhuru Kenyatta ambayo imemteua aliyekuwa waziri wa usalama wa ndani Fred Matiang’i kuiwakilisha katika muungano huo, Martha Karua wa Peoples Liberation Party (PLP), Kalonzo Musyoka wa Wiper, DAP- Kenya ya Eugene Wamalwa na Democratic Party ya aliyekuwa waziri Justin Muturi.
Wachanganuzi wa siasa wanasema hatua ya DCP ni ishara muhimu ya mabadiliko ya kimkakati. “Hii ni dalili ya ukomavu wa kisiasa. DCP inatambua kuwa kugawanyika kwa kura za upinzani kutachangia ushindi wa urahisi kwa Kenya Kwanza,” asema mchambuzi wa siasa, Hellen Njeri.
Mfano wa Malava unafuata wa Mbeere Kaskazini, ambako DCP iliwahi kumuachia mgombea wa Democratic Party (DP) wa Justin Muturi, na hatua hiyo kufanikiwa kuimarisha ushirikiano wa vyama vya upinzani.
Chama cha Jubilee ambacho kinasisitiza kingali katika Muungano wa Upinzani pia kiliunga mgombeaji wa DP katika Mbeere Kaskazini.
Kwa sasa, Cleophas Malala anapanga mikutano mikubwa zaidi ya kampeni inayojumuisha vyama vya Muungano wa Upinzani, huku akitangaza kuwa Seth Panyako ndiye mgombea rasmi wa upinzani katika kinyang’anyiro hicho.
Eugene Wamalwa, Kiongozi wa DAP–Kenya, alitaja hatua hiyo kuwa “ishara ya mwanzo wa Muungano wa Upinzani.” “Tukiacha kugawanyika, tutaonyesha Kenya nzima kuwa upinzani unaweza kufanya kazi pamoja kwa maslahi ya wananchi,” alisema.
Lakini upande wa serikali unakejeli upinzani, ukisema utaibuka na ushindi ukisisitiza umoja wa vinara hauna nguvu.
Hata hivyo, wachanganuzi wanaonya kuwa kauli kama hizo zinadhihirisha hofu ya Kenya Kwanza. “Kama vinara wapinzani wataendelea na mikakati ya kuachiana maeneo kulingana na nguvu za vyama, 2027 haitakuwa rahisi kwa serikali,” asema Dkt Daniel Wabwire, mchambuzi wa siasa za magharibi.
Kwa sasa, hali ya kampeni Malava imepamba moto. Panyako wa DAP–Kenya atakabiliana na David Ndakwa wa UDA katika kinyang’anyiro kinachotazamiwa kuwa kipimo cha nguvu kati ya Kenya Kwanza na Muungano wa Upinzani.
“Hatua ya DCP kuachia DAP–Kenya ni zaidi ya makubaliano ya kisiasa — ni ujumbe wa wazi kwamba upinzani umeanza kujifunza kutokana na makosa ya zamani. Ikiwa mikakati kama hii itaendelezwa kote nchini, huenda uchaguzi wa 2027 ukaleta changamoto kubwa kwa serikali ya sasa,” asema Njeri.
Kwa sasa, asema, kuna dalili za matumaini kwamba vyama vya upinzani vinatambua umuhimu wa umoja.
“Mfano mzuri ni ule ulioshuhudiwa katika Eneo Bunge la Mbeere Kaskazini, ambako chama cha Jubilee kilionyesha ukomavu wa kisiasa kwa kuachia mgombeaji wa DP, kuepusha mgawanyiko wa kura za upinzani. Uamuzi huo ulionyesha kwamba umoja ni silaha kuu dhidi ya mgawanyiko unaonufaisha Kenya Kwanza,” asema.
Vyama vinaposhirikiana kwa nia moja, asemaWabwire, vinawapa wananchi matumaini kuwa kuna mwelekeo mpya wa kisiasa unaozingatia maslahi ya pamoja badala ya tamaa binafsi.
“Hata hivyo, changamoto kuu inayokabili upinzani ni ile ile iliyoathiri miungano ya kisiasa nchini — usaliti, ubinafsi, na tamaa ya mamlaka. Mara nyingi, wanasiasa wamekuwa wakitumiwa na wapinzani wao wa kisiasa kama “fuko” za kudhoofisha umoja wa upinzani. Wengine hupewa nyadhifa, fedha, au ahadi za vyeo serikalini ili kuvuruga mikakati ya kisiasa ya upinzani. Tabia hii ya usaliti imekuwa kama saratani inayoharibu misingi ya demokrasia ya kweli,” asema Wabwire
Anasema kile kinachohitajika sasa ni umoja wa dhati unaozingatia maslahi ya wananchi, si makubaliano ya muda mfupi ya kisiasa.