Mbadi aunda mbinu ya kuwatuliza Gen Z anaposuka Mswada wa Fedha 2025
WIZARA ya Fedha imepanga mikutano katika kaunti mbalimbali nchini ili kukusanya maoni kuhusu bajeti ya 2025-2026 hatua ambayo inanuiwa kuepuka ghadhabu za vijana zilizoshuhudiwa mwaka jana.
Waziri John Mbadi Jumanne alisema mikutano hiyo ya hadhara ni sehemu ya uhusiano wa serikali na watu wa kawaida kuwasikiliza kuhusu kile wanachotaka na wasichotaka kijumuishwe katika bajeti ya mwaka ujao wa kifedha.
Waziri anatarajiwa kuwasilisha Taarifa ya Sera ya Bajeti (BPS) katika Bunge la Kitaifa kabla ya Februari 14, ikielezea makadirio ya matumizi ya serikali kwa mwaka wa kifedha wa 2025-2026 ambao utaanza Julai.
Lakini hata kabla ya Bunge kuanza kushirikisha umma, Bw Mbadi alisema yeye binafsi ataenda kwa wananchi na kuwasikiliza na kujibu maswali yao kuhusu hatua mbalimbali za ushuru za serikali kama alivyofanya Jumatatu katika bustani ya Jevanjee.
Waziri huyo alikiri kwamba, hatua ya serikali kutosikiliza wananchi ndiyo sababu kuu iliyofanya Mswada wa Fedha wa 2024-2025 kukataliwa na Rais William Ruto baada ya vijana wa Gen Z kuandamana.
Kulingana na mpango huo, baada ya mkutano wa Nairobi uliofanyika katika bustani ya Jevanjee Jumatatu, Waziri atafanya mikutano kama hiyo Pwani, kisha kaskazini mwa Kenya, atafanya mkutano mmoja Magharibi na Nyanza kabla ya kumalizia Mashariki na Kati.
Tarehe na maeneo ya mikutano hiyo bado zinashughulikiwa kabla ya kutolewa kwa viongozi wa kaunti husika kuipanga na kuiratibu.
“Mimi binafsi nitahudhuria mikutano hii isiyo rasmi na kuwasikiliza watu mashinani kuhusu kile wanachotaka au wasichotaka kijumuishwe kwenye bajeti ya mwaka ujao. Ninaamini kuwa ni sehemu ya mchakato ambayo iliepukwa na upande wa serikali katika Mswada wa Fedha wa mwaka jana ambao ulikataliwa,” Bw Mbadi alisema.
“Tunataka kufanya mambo kwa njia tofauti mwaka huu na sehemu yake ni pamoja na kubeba kila mtu katika hatua ya awali ya kuandaa bajeti. Kama serikali, hatuna chaguo ila kuwasikiliza wananchi.”
Mkakati wa pili ambao wizara inataka kutumia ni marekebisho ya makadirio ya mapato yalingane na takwimu halisi zaidi.
“Lazima tuwe na mjadala wa ukweli kuhusu makadirio ya mapato yetu na kuyafanya yawe ya kweli iwezekanavyo. Nikikutana na kamati ya bajeti kuhusu hili, tutalijadili na kuamua njia ya kusonga mbele,” Bw Mbadi alisema.
Waziri huyo alisema ni lazima serikali itafute jinsi ya kuongeza mapato, jambo linalosababisha ongezeko la kodi.
Alisema mpango wa kukusanya mapato kama inavyoelezwa katika bajeti huweka presha kwa Mamlaka ya Ushuru ya Kenya (KRA).
Ripoti ya hivi punde inaonyesha kuwa, KRA ilikosa kutimiza lengo lake la kukusanya ushuru katika robo ya kwanza iliyoishia Desemba kwa Sh163 bilioni kutokana na kukataliwa kwa Mswada wa Fedha wa 2024.
Mamlaka hiyo ilikusanya Sh1.07 trilioni katika kipindi hicho ambacho ni chini ya ilizopaswa kukusanya kuelekea Sh2.47 trilioni zinazolengwa mwaka mzima wa fedha unaoishia Juni 2025.